Habari

Akaunti za 'Tangatanga' zanyemelewa

August 30th, 2020 2 min read

Na ONYANGO K’ONYANGO

BAADA ya kupokonywa nyadhifa za uongozi katika chama cha Jubilee, washirika wa Naibu Rais William Ruto sasa wameingiwa na wasiwasi kwa vile akaunti zao za kibinafsi zachunguzwa kubainisha chanzo cha mapato yao.

Kwenye mahojiano na Taifa Jumapili, wabunge wanaoegemea upande wa Dkt Ruto ulio maarufu kama kikundi cha ‘Tangatanga’ walisema wanashuku hatua hizo ni miongoni mwa juhudi za kutaka kuwazima ili wasimpigie debe anapojiandaa kuwania urais ifikapo mwaka wa 2022.

Mbunge wa Kapsaret Oscar Sudi ambaye ni mtetezi sugu wa Dkt Ruto alidai kwamba serikali imeunda kikosi maalumu cha wapelelezi kinachoshirikisha maafisa wa Huduma ya Taifa ya Ujasusi (NIS) na Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) kuwatisha wandani wa Naibu Rais.

Bw Sudi alidai kwamba kikosi hicho kinaendelea kuchunguza chanzo cha mali yake kibinafsi na shughuli zake.

“Tunatishwa kwa msimamo wetu. Walitaka kuchunguza biashara ninazofanya na kwa kuwa sifanyi biashara yoyote na serikali, kuna shamba nililouza zamani. Sasa wananichunguza na ninasubiri waje kunikamata,” alisema.

Mbunge wa Keiyo Kusini, Bw Daniel Rono, ambaye ni mshirika mwingine wa Dkt Ruto aliambia Taifa Jumapili kwamba mapema Agosti alizimwa kutoa pesa katika mojawapo ya akaunti zake za benki hadi aeleze zilitoka wapi.

“Mimi nimeathiriwa na vitisho vya serikali. Baada ya kuchunguza jinsi miradi ya hazina ya maeneobunge (NG-CDF) inavyotekelezwa katika eneobunge langu na kukosa doa lolote, wameanza kuchunguza mapato yangu ya fedha. Haieleweki kwa nini kuchunguza nilivyopata Sh300,000 pekee… Ingeeleweka kama zingekuwa zaidi ya Sh1 milioni,” alisema Bw Rono.

Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua alijipata katika hali sawa serikali ilipomzuia kutoa zaidi ya Sh200 milioni katika akaunti zake za benki.

Bw Gachagua ni mmoja wa washirika wa Dkt Ruto eneo la Mlima Kenya.

Jumamosi, Dkt Ruto aliendelea kuwahimiza washirika wake wasiogope vitisho vya kila mara. Alitoa wito kama huo mapema wiki hii akisema kwamba watatishwa kwa kila namna wabadilishe msimamo.

“Tusirudi katika mbinu zilizopitwa na wakati za kisiasa. Tunaweka nchi katika hatari ya ghasia,” alisema.

Washirika wengine wa Dkt Ruto wanaomulikwa na serikali ni seneta Susan Kihika (Nakuru), wabunge Kimani Ngunjiri (Bahati), Kimani Ichungwah (Kikuyu) miongoni mwa wengine.

Lakini viongozi wanaomuunga Rais Uhuru Kenyatta wakiongozwa na kiranja wa wengi katika seneti Irungu Kang’ata walipuuza madai ya washirika wa Dkt Ruto wakisema wanaeneza uongo ili wahurumiwe na umma.

“Serikali haitishi yeyote, inaamini katika Uhuru wa kujieleza na makundi ya kisiasa. Italinda haki hizi kila wakati hata wakati uhuru huo unatumiwa kukosoa serikali, hata hivyo uhuru huo sio leseni ya kutenda uhalifu,” alisema Bw Kang’ata.

Jana, akiwa Mombasa, Dkt Ruto aliendelea kuwashambulia mahasimu wake walio katika Chama cha Jubilee akiwataka wahame kwa vile wameonyesha nia ya kuunga mkono azimio la Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga. Msimamo kwamba Jubilee itamuunga mkono Bw Odinga ulikuwa umetolewa na Naibu Mwenyekiti wa chama hicho, Bw David Murathe.