Dondoo

Akemea pasta kanisani kumchochea aachane na mumewe amtafutie bwanyenye

May 6th, 2018 1 min read

Na CORNELIUS MUTISYA

KAVIANI, MACHAKOS

MAMA wa hapa alimkemea pasta wake mbele ya waumini akimshutumu kwa kumchochea amteme mumewe ili amtafutie mume mwingine tajiri.

Kulingana na mdokezi, mama huyo alikuwa muumini katika kanisa la pasta huyo. Ajabu ni kwamba, pasta hakuwa ameoa licha ya kutimu umri wa kuwa na mke.

Tetesi zilitanda mtaani kuwa mama alikuwa mpango wa kando wa Mtumishi huyo wa Mungu.

Siku moja, pasta alimualika katika ofisi yake ili ampatie ushauri wa kiroho kufuatia maono aliyodai yalimjia usiku akiwa usingizini.

“Alimweleza kwamba alifunuliwa kuwa ndoa yake haikuwa shwari na akamwambia roho alimfunulia aondoke katika ndoa hiyo yenye laana mara moja. Alimwambia angemtafutia mume mwingine tajiri,” alieleza mdokezi.

Hata hivyo, mama huyo alitilia maanani ushauri wa pasta na akaenda nyumbani, alifunganya virago vyake na akakodi chumba sokoni hapa akisubiri pasta amtafutie mume mzuri na tajiri.

“Miezi sita ilipita bila pasta kumtafutia mume na akaanza kukata tamaa. Alianza kujuta kwa kuhadaiwa aondoke katika ndoa yake,” alisema mpambe wetu.

Inasemekana siku ya kioja mama alifika kanisani akiwa na hamaki kuu na akaanza kumfokea pasta peupe.

“Kumbuka ulinidanganya niondoke katika ndoa yangu ukidai ulitumwa na roho mtakatifu. Miezi sita imepita na hujanitafutia mume ulivyodai ulifunuliwa,” alifoka mama huyo huku waumini wakibaki vinywa wazi.

Penyenye zaarifu pasta alipata fedheha na akamwambia mama azidi kusubiri miujiza.

Hata hivyo, waumini walishangaa jinsi pasta alivyoweza kuvunja ndoa akidai angemtafutia mwanamke huyo mume mwingine ilhali yeye mwenyewe hakuwa na mke.

…WAZO BONZO…