Makala

AKILIJIBU: Naomba kujua manufaa ya mkojo wa sungura

January 17th, 2019 2 min read

SWALI: Ninaitwa GODWIN BARAKA kutoka Cheptiret, Eldoret. Mimi ni mkulima mdogo na ninahitaji kujifunza kutoka kwenu. Ninafuga sungura na ninapata pia mkojo wake lakini sijui kazi yake. Ninayo pia bustani ndogo ya mboga. Katika bustani yangu ninatumia kemikali. Ninaomba mnishauri.

JIBU: Kwanza nakushukuru kwa kufuatilia makala katika Jarida hili la Akilimali. Ikiwa unawafuga sungura, basi inamaanisha unaweza kupata mbolea utakayoitumia kuongeza rotuba kwenye shamba lako la mboga. Koma kabisa kutumia mbolea za kisasa za madukani zilizojaa kemikali maanake kemikali hizi huyeyusha au kupunguza rotuba ya mchanga ikiwa zitatumiwa kwa kipindi kirefu.

Una bahati sana unawafuga sungura hao kwani wao ndio watakupa dawa madhubuti na halisi isiyo na kemikali yoyote.

SWALI: Mimi ni SARAH MUSUNGU kutoka eneo la Mumias, Kakamega. Naomba kufahamishwa kuhusu mahali nitakapowapata ndege aina ya tombo (quail) kwa minajili ya kuwafuga. Nilivutiwa sana na habari ya mfugaji mmoja kutoka Kaunti ya Vihiga aliyeangaziwa katika jarida hili la Akilimali.

JIBU: Ndege aina ya tombo wanaweza kupatika katika soko la Luanda katika Kaunti ya Vihiga. Kwa habari zaidi, anaweza kuwasiliana na mfugaji James Makate kupitia nambari ya simu 0711572890 au 0718736874 ili aweze kupata mashauri zaidi yahusuyo mbinu mwafaka zaidi na faida za kuwafuga tombo.

SWALI: Ninaitwa PETER WAMALWA kutoka Kimilili, Naomba kujua machungwa ya rangi ya manjano hupatikana wapi na hunawiri katika maeneo gani ya humu nchini. Je, mkulima anahitaji nini hasa ili akifanikishe kilimo cha matunda haya?

JIBU: Machungwa ya sampuli nyingi hupatikana katika maeneo mbalimbali ya Kaunti ya Makueni. Hata hivyo, ingalifaa zaidi ikiwa utafafanua makala ambayo uliyasoma katika Jarida hili la Akilimali ili tukukutanishe na mkulima wa matunda hayo akupe ushauri wa kutosha ambao pia utakufaidi katika kilimo chako.

SWALI: Mimi ni LUCY WAWERU kutoka Thika. Nifahamisheni jinsi bora ya kupanda mboga aina ya spinachi.

JIBU: Mboga aina ya spinachi ni sawa na mboga za mchicha au sukumawiki na hupandwa kwa mtindo sawa na hizo. Hata hivyo, ni lazima uzingatie aina ya mbegu ambazo utapanda kutegemea hali ya hewa ya eneo ambalo unataka kuendeshea kilimo hicho.

 

Jinsi ya kutengeneza dawa hii:

Teka mkojo wa sungura wako kila siku. Ukitaka kuunda mbolea, changanya kila lita moja ya mkojo wa sungura na lita tano za maji kisha unyunyizie kwa mimea yako. Unafaa kufanya unyunyiziaji wa mbolea hii kila asubuhi ? na jioni. Mimea hii itapokea mbolea hiyo kupitia kwa majani yake moja kwa moja huku mizizi ikifaidika pia.

Iwapo unataka kuunda dawa, changanya mkojo huu na majani ya mimea ya Tithonia na Mexican Mint Marigold kisha uhifadhiwa kwa kibuyu kwa siku saba. Changanya sasa na maji kwa kiwango cha 1:2 ambapo sasa mchanga- nyiko huu unaweza kutumiwa kama dawa dhidi ya wadudu na magonjwa ya mimea kwa kunyunyizia.

Maelezo yamekusanywa na Chris Adungo