Makala

AKILIJIBU: Nini kiini cha kuku kutaga mayai yenye chembe za damu?

September 12th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

SWALI: Ninaitwa JUSTINE Nasenya kutoka Webuye, Bungoma. Ningependa kujua kiini cha kuku wangu kutaga mayai yaliyo na chembembe za damu.

JIBU: Hii ni mojawapo ya athari za ugonjwa wa Coccidiosis. Dalili ya ugonjwa huu ni chembe za damu kwenye mayai au katika kinyesi cha kuku.

Pia kuku hubadilisha ghafla mtindo wa kula na kuanza kunywa maji mengi nyakati za asubuhi hata kabla kupata lishe ya kawaida.

Iwapo rangi ya kinyesi itabadilika kuwa manjano baada ya muda mfupi, basi huenda wamevamiwa na vimelea vya protozoa. Dalili ya uvamizi huu ni kuku kujikunja kama kwamba wana baridi kali na hata kukosa kabisa hamu ya kula. Fika katika maduka ya kuuza dawa za mifugo uelekezwe zaidi.

 

SWALI: Mimi ni ELIAS MAKAU kutoka Kitui. Ng’ombe wangu wanatokwa na uvimbe shingoni, tumboni na miguuni na kufa ghafla. Je, wana tatizo gani?

JIBU: Huu ni ugonjwa wa Kimeta. Ugonjwa wa Kimeta unawashika mifugo na pia mbogo, punda-milia na wanyamapori wengine walao majani. Vimelea vya Kimeta vinaweza kuishi kwenye udongo kwa muda mrefu.

Kuna uwezekano wanyama wakapata ugonjwa wa kimeta mwanzoni mwa majira ya mvua, wakati majani wanayokula yanapokuwa mafupi. Kutokana na mabadiliko ya matumizi ya ardhi, ambayo yanaifanya mifugo na wanyamapori kukaa pamoja kwenye eneo dogo, matukio ya kimeta yanaongezeka. Binadamu wanaweza pia kuupata ugonjwa huu, kwa kushika au kula nyama ya mifugo iliyoambukizwa.

Kama watu au wanyama walao mizoga wataupasua mzoga (na kuufanya utumbo kutoka) wa mnyama aliyekufa kwa kimeta, wanaweza kusababisha kuanza kwa mlipuko wa kimeta kwa kusababisha vimelea kusambaa kwenye hewa na udongo.

Ardhi ambayo itafikiwa na majimaji kutoka kwenye mzoga wa mnyama aliyeugua Kimeta yaweza kuhifadhi vimelea vya ugonjwa huo hata kwa miaka ipatayo 60! Iwapo unahisi mnyama amekufa kutokana na kimeta, linda mzoga au ufunike kwa miiba au mawe kuzuia wanyama walao mizoga wasiupasue.

Uchome mzoga baada ya kuunyunyizia mafuta ya taa au petroli. Au ufukie kwenye shimo la urefu wa mita mbili na kuumwagia majivu au chokaa. Ili kuzuia na kudhibiti, chanja kwa miezi kati ya tisa na kumi na mbili na chanjo hiyo bora iwe imehusisha juhudi ya jamii au serikali ikilenga kuwachanja ng’ombe wote. Dawa dhidi ya bakteria (Antibiotics) zinaweza kuwa dawa sahihi iwapo matibabu yataanza mapema, ingawa ni bora kuzuia ambako pia gharama zake ni nafuu.