Makala

AKILIMALI: Alenga kuingia jumuiya ya mamilionea kupitia teknolojia ya utengenezaji makaa

August 24th, 2019 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

MNAMO Januari 12, 2016, Bi Mercy Wanjiru akiwa na umri wa miaka 21 aliingia katika dukakuu jijini Nairobi kujinunulia chokoleti, lakini akaishia si tu kununua alichotaka bali pia ‘kununua’ wazo la kibiashara ambalo leo hii linamzolea pato la Sh50,000 kwa mwezi na ambapo matumaini yake makuu yaliyo hai ni kuwa, kabla ya mwaka wa 2025, atakuwa akijipa pato la Sh1 milioni.

Maisha ya huyu mwanadada – ambaye kitaaluma amesomea Teknolojia ya Mawasiliano (IT), Uchapishaji na Masuala ya Burudani – yakabadilishwa na shughuli hiyo ya kujinunulia chokoleti.

Anasema kuwa alikuwa amesaka kazi kwa miaka minne mfululizo bila kupata afueni na kwamba ile ajira ya maana sana aliyokuwa amepata na iliyokuwa imempa hela hizo za kuwa mteja ndani ya duka hilo ilikuwa ni ya kuwa mhudumu katika hoteli ya wastani, mshahara ukiwa Sh150 kwa siku.

Kwa mwezi pato lake likiwa ni Sh4,500 na hapo awali akiwa ameondoka kutoka ajira ya Sh8, 000 kwa mwezi kwa kuwa gharama za kutoka nyumbani hadi kazini kwa mwezi zilikuwa Sh6,000 hivyo basi “kunigeuza kuwa mwajiriwa wa Sh2,000 kwa mwezi.”

Bongo lake la kibiashara liligutuka wakati akiwa katika supamaketi hiyo alizuru eneo ambalo lilikuwa limebandikwa notisi ya “makaa”.

Anasema kuwa alichanganyikiwa na akajiuliza: “Makaa pia yanauzwa ndani ya maduka haya?”

Anasema kuwa alisongea eneo hilo ili kujipa ushahidi kuwa makaa pia huuzwa ndani ya maduka hayo na ndipo alikumbana na uhalisia kuwa makaa hayo hayakuwa yale ya kuchomwa bali yalikuwa ya kutengenezwa kiteknolojia zaidi.

“Ndipo nikajipa ufahamu kuwa makaa hayo yalikuwa na jina Briquettes na ambayo siyo ya kuandaliwa kwa njia ya ukataji na uchomaji wa miti, bali ni makaa mbadala yanayotengenezwa kwa kutumia kila aina ya malighafi yaliyo na uwezo wa kuchomeka yakiwa yamekauka,” anasema Wanjiru.

Anasema kuwa vipande 10 vya makaa hayo vilikuwa na bei ya Sh200 na ndipo hesabu ya haraka ilimwingia katika kichwa chake na alipojipa jibu, akagundua “hapa ndipo mwanga wa utajiri wangu ulipo.”

Anasema kuwa aliondoka kutoka duka hilo akiwa ashaamua kuwa muuzaji wa makaa ya kutengenezwa liwe liwalo.

Na ndipo alifanya utafiti wake na akagundua kuwa malighafi aliyokuwa akihitaji yalikuwa kwa wingi mashinani; kwao katika kijiji cha Kihiu Mwiri, Kaunti ya Murang’a.

Malighafi hayo ni pamoja na majani yaliyokauka, ungaunga ambao hutokana na upasuaji mbao, mabaki ya makaa ya kuchomwa na pia vipande vya karatasi.

Anasema kuwa kile alichokuwa hana ufahamu nacho ni teknolojia ya utengenezaji na ndipo alizama tena katika utafiti akisaka ni wapi ajipe ufahamu huo.

Ni katika harakati hizo ambapo alipata dokezi kuhusu kundi moja la kijamii la Kaunti ya Kiambu ambalo lilikuwa katika kazi ya kuyapa makundi uwezo wa kimaisha na ambapo utengenezaji wa makaa hayo ulikuwa mojawapo ya nyenzo.

“Nilienda mpaka eneo la Thogoto katika Kaunti ya Kiambu na nikajiunga na kundi hilo na ambapo nilifahamishwa kuwa kwa siku moja pekee, gharama ya elimu ya utengenezaji makaa hayo ilikuwa Sh5,000,” anasema.

Anasema kuwa siku hiyo ilikuwa inatosha kujipa uwezo kamili wa kutengeneza makaa hayo na “nililipa na nikaingia darasani.”

Bi Mercy Wanjiru katika pahala pake pa kazi ya utengenezaji makaa katika kijiji cha Kambi, Kaunti ya Murang’a. Picha/ Mwangi Muiruri

Anaongeza kwamba alionyeshwa vile malighafi huchomwa kwanza ndio yageuke kuwa jivu na hatimaye unachanganya na maji, unaweka katika vifaa vya kutoa umbo la makaa na hatimaye unayakausha ukitumia ama moto au jua na matokeo yanakuwa ni makaa mbadala sampuli ya Briquettes.

Anasema kuwa kuna mashine spesheli ya kurahisisha kazi hiyo na ambayo bei yake ni Sh145,000 kwa sasa.

“Nilikuwa na bahati kwa kuwa wazazi wangu walinisaidia na nikainunua,” anasema.

Anasema kuwa majirani ndio walikuwa wateja wake wa kwanza na ambapo alijishindia umaarufu na imani huku ikibainika kuwa makaa hayo ya kutengenezwa kiteknolojia zaidi yalikuwa salama kwa mazingira, ya bei nafuu na yaliyokuwa na huduma murwa.

Anasema kuwa mwanzoni mwa 2019 ndipo biashara yake ilijipa faida ya kwanza ya Sh5,000 na ambapo akianza Juni, faida hiyo ilikuwa imetinga Sh50,000 kwa mwezi ndani ya kampuni yake inayofahamika kama Mwashime Enterprises.

Anasema kuwa akizidisha harakati za mauzo na pia matangazo ya kibiashara atajipa mashiko ndani ya soko na ambapo ana imani kuu kuwa biashara hii yake itamuingiza katika jukwaa la ukwasi wa kuorodheshwa miongoni mwa mamilionea.

Leo hii amesahau kuwa kuna wakati katika maisha yake “nilipokuwa nakisaka kazi kwa udi na uvumba.”

Anasema: “Dunia yangu ishajipa taswira ya baraka ya pato na kile tu ninachohitajika ni kuzidisha bidii na umakinifu na matunda niyapate.”

Anajiwekea malengo kuwa kabla mwaka wa 2025 kuisha, atakuwa na kiwanda chake cha utengenezaji makaa haya na ambapo analenga biashara ya Sh1.0 milioni kwa siku na kwa mwezi awe akijipa faida ya Sh10 milioni.

Akiwa kwa sasa ni mama wa watoto wawili wenye umri wa miaka tisa na miwili mtawalia, anasema kile anachowindana nacho kwa kila ncha na taji ni kupata mtaji wa Sh8 milioni ambazo amedadisi kuhitajika kuzindua biashara ya kuafikia lengo hilo lake la 2025.

“Na usiwe na shaka yoyote. Nitapata mtaji huo na niafikie lengo langu,” anajipa tumaini.