AKILIMALI: Aliacha mahindi ili kula ndizi kwa kijiko

AKILIMALI: Aliacha mahindi ili kula ndizi kwa kijiko

Na PETER CHANGTOEK

BAADA ya kukuza mihindi kwa muda mrefu pasi na kuona faida ya zao hilo, alikata kauli kuiacha shughuli hiyo, na kujitosa katika ukuzaji wa mimea ya matundadamu, migomba na pilipili mboga.

Charles Lavaha, 49, mkazi wa eneo la Kiptuiya, katika Kaunti ya Nandi, anasema kuwa, wakati alipokuwa akiikuza mihindi, alikuwa akizitumia fedha nyingi katika uzalishaji wa zao hilo, na hata kupata hasara kwa wakati mwingine, hususan hali ya anga inapobadilika.

Hilo ndilo jambo ambalo lilimsukuma kuwaza na kuwazua, kuhusu mradi ambao angejishughulisha nao, ili apate riziki ya kuridhisha na hata kuilisha familia yake bila kuhangaika wala kufadhaika.

Wazo la kuikuza migomba ndilo lililomjia akilini, baada ya kupiga hesabu za uzalishaji wa mmea wenyewe.

Mkulima huyo hulitumia shamba ekari mbili kuikuza migomba. Katika shamba hilo, ipo migomba 300 iliyokomaa, na mingine 200 ambayo aliipanda mwaka uliopita.

Anapoipanda migomba yake, huhakikisha kuwa anaacha nafasi ya mita tatu kutoka kwa mmea mmoja hadi kwa mwingine.

Ana migomba 100 aina ya Williams (TCB) na 400 aina ya Giant. “Nilinunua miche ya Giant kutoka kwa wakulima wanaofanya kilimo hicho katika eneo hili. Nilikuwa nikinunua kila mmoja kwa Sh50. Nilichimba kila shimo kwa Sh75,” asema, akiongeza kwamba, migomba aina ya Giant hupendwa sana, ndiposa akaikuza kwa wingi.

Luvaha anafichua kuwa, alizinunua mbolea za mbuzi na kondoo matrela matatu kutoka kwa mkulima mmoja wa eneo hilo, na kuzitumia kuikuza mimea hiyo. Anadokeza kuwa alinunua mbolea hizo kwa Sh1,500 kwa kila trela.

Alijitosa katika kilimo hicho mnamo mwaka 2019. “Ile ya kwanza inaendelea kuzaa,” aongeza mkulima huyo, ambaye ni baba wa watoto tisa.

Baada ya kuipanda miche ya migomba, aliipanda mimea ya pilipili mboga na mimea ya maboga katika nafasi iliyoachwa, ili kuhifadhi unyevu mchangani, na kuyazuia maotea kuota shambani.

“Ilimaliza mwaka mmoja nikaanza kula ndizi za kwanza,” adokeza Luvaha, ambaye huuza mkungu mmoja wa ndizi kwa kati ya Sh400 na Sh500.

“Huwa ninapeleka hapa Kapsabet. Nina mteja kutoka eneo la Lessos, ambaye huwa anachukua kwa wingi. Huchukua kama mikungu kumi kwa bei ya wastani ya Sh400, kila mmoja” asema.

Mkulima huyo anasema kuwa aina zote za migomba anayoikuza huchukua muda wa mwaka mmoja ili kuanza kuzaa ndizi.

Awali, alikuwa akiikuza mihindi na miharagwe, lakini hali ya hewa ikamtatiza kwa kubadilikabadilika, na akawa anavuna mavuno kidogo kutoka kwa shamba lake.

“Kwa wakati mwingine nilikuwa nikivuna magunia 10 au 15 ya mahindi kwa ekari moja, na nimesubiri kwa muda mrefu na gharama ni kubwa. Nikakaa chini na kusema niweke kilimo cha mahindi kando, na niipande migomba,” aeleza, akiongeza kuwa, alikuwa akishurutika kusubiri kwa muda wa miezi sita ili ayavune mahindi shambani.

Anaongeza kuwa baada ya kuondoa gharama, alikuwa akipata hasara kwa wakati fulani kwa uzalishaji wa mahindi. Bei ya zao hilo ilikuwa duni pia. “Ukichukua mkopo huwezi kulipa na unaweza kufa maskini (kwa uzalishaji wa mahindi).”

Baada ya kupiga hesabu na rafikiye mmoja, akagundua kuwa mgomba mmoja unaweza kumpa mikungu minne kwa mwaka, na akiuza mmoja kwa Sh500, angepata Sh2,000 kutoka kwa mmoja. Alipopiga hesabu za migomba mia tano kwa Sh2,000, akang’amua kuwa angepata faida zaidi ikilinganishwa na uzalishaji wa mahindi.

Mkulima huyo hutegemea mvua kuendeleza shughuli zake za ukulima. Anaongeza kuwa kwa wakati huu, ana azimio la 2022, analoliita ‘Operesheni Angamiza Umaskini’, ambapo anaazimia kujitosa katika ufugaji wa kundoo, nguruwe na nyuki.

Mkulima huyo anasema migomba yake haijawahi kuathiriwa na magonjwa wala kuvamiwa na wadudu waharibifu.

Luvaha anatoa wito kwa serikali kuwaauni wakulima, ili nchi iwe na utoshelevu wa chaakula. “Zile pesa ambazo serikali inatumia kununua chakula nje, zinaweza kufanya kazi nyingine. Halafu tunahitaji maafisa wa kilimo wawe wakiwatembelea wakulima,” asema mkulima huyo.

“Serikali yetu iwe kama ya Uganda ambayo huwapa wakulima miche ya migomba aina ya TCB bila malipo,” apendekeza mkulima huyo.

Anaongeza kuwa anapania kujitosa katika shughuli ya kuongeza thamani kwa ndizi katika siku za usoni, kwa kuzisaga ili unga upatikane.

Mbali na kushughulika na ukuzaji wa migomba, mkulima huyo pia, ana mimea 2,000 ya pilipili mboga na ya mutundadamu kadha wa kadha.

You can share this post!

TAHARIRI: Fujo hizi za kisiasa hazifai kuvumiliwa

BONGO LA BIASHARA: Jinsi video, picha zilivyomsukuma...