AKILIMALI: Aliacha ubawabu sasa anapepea katika kilimo cha mboga akijikimu

AKILIMALI: Aliacha ubawabu sasa anapepea katika kilimo cha mboga akijikimu

Na PATRICK KILAVUKA

ALIACHA kazi ya ubawabu baada ya kuifanya kwa mwezi mmoja kutokana na malipo duni na kuyoyomea katika ukulima aliokuwa amefunzwa na wazazi wake.

Joseph Afwabi anasema baada ya masomo yake ya Darasa la Nane katika Shule ya Msingi ya Mukomari, Kaunti ya Kakamega, alisafiri hadi jijini Nairobi kusaka njia mbadala ya kujiendeleza kimaisha kutokana na tatizo la ukosefu wa karo.

Hapo ndipo aliajiriwa kazi ya ulinzi na hakuridhika nayo na hivyo basi, akaamua kusaka majani mabichi ya kikazi kusaidia hata ndugu zake kwa sababu yeye ndiye aliyekuwa kifungua mimba.

Anasema akiwa nyumbani, alikuwa anapenda sana kupanda mahindi, mboga za kila aina na miwa. Na, wazo la kuendeleza ukulima lilimgonga akilini na mara moja akatafakari kuhusu mustakabali wa kupata fursa nyingine ya kujiliwaza katika kazi hiyo.

Anasema aliajiriwa kibarua katika shamba la mkulima Samuel Kamau sehemu ya Gathondeki, Dagoretti, kama mchungaji wa mifugo na kufanya ukulima shambani.

Bila kukata tamaa ya kuafikia malengo ya kuwa mkulima, alimfanyia kazi miaka miwili akijiwekea hazina kidogo kutoka kwa mshahara kisha akafunguka kimawazo na kujikodishia kijisehemu kwa Sh15,000. Aliweza kupanda mboga za kila aina kupitia mtaji alioanza nao wa kima cha Sh25,000 na akarudisha pesa kwa mwaka huo huo. Aliweza kujikodishia vijishamba vingine ambavyo anavitumia kupanda maboga mbalimbali. Hajaacha ajira yake kwani anatumia ukulima wake kama njia mbadala ya kujiongezea pato kwa kuufanya katika muda wake wa ziada kwa miaka tisa sasa.

“Huwa namaliza kazi kwa wakati ufaao kisha ninaenda kujikakamua kuangalia mboga zangu,” anadokeza mkulima Afwabi.

Ameunganisha mifereji ya kunyunyuzia maji kwa sababu anajiamini kuwa mpanzi wa kila msimu.

Mboga ambazo hupanda ni; Brokoli, cauliflower, kabeji, sukuma, kunde, Spinachi na lettuce ambazo ni za aina mbili – iliyo ngumu na nyororo. Isitoshe, ni mweledi wa upanzi wa vitunguu.

Anasema anapenda kupanda mboga hizo kwani nyingi yazo huchukua miezi mitatu kuvunwa hali ambayo inamwezesha kupanda msimu mitatu au minne.

“Miezi mitatu tu hivi, huwa nishaweka pesa mfukoni. Hii huwa baada ya kutayarisha nasari, kupanda nikitumia mbolea ya upanzi – DAP na ya unawirishaji – CAN. Zinamea baada ya wiki hivi kisha kukaa kwa nasari kwa mwezi mmoja kabla kuhamishia kwa vijishamba vyangu vya upanzi,” anaeleza mkulima huyo na kuongezea kuwa huipanda, kuipalilia kukomesha kwekwe na kunyunyuzia dawa ya kuangamiza wadudu au ya kudhibiti hali ya ubaridi ambao unazua changamoto pia kwa mimea.

Afwabi ameonja matunda ya jasho lake la ukulima na anakimu familia yao na yeye mwenyewe.

Anasema msimu ukiwa mzuri, mbegu ambazo huzinunua kwa Sh2,500, zinafaa kumpa au kuchangia pato la kati ya Sh15,000-20,000. Japo kuna wakati anasema unaweza kuambulia patupu endapo msimu umekuwa mbaya kutokana na changamoto za maangamizi ya wadudu na baridi au kiangazi kikali kinachoweza kukausha hata chemichemi za maji.

Kwa mfano, alishuhudia tukio kama hilo miaka mitatu; 2014, 2017 na 2020. Hata hivyo, anakariri kwamba yeye kama mkulima aliyejitolea kuwa na ari na mapenzi ya kukuza kilimo, hakuona haja ya kukata tamaa kwa sababu kwake hizo changamoto zinampa njia mbadala ya kujifunza mbinu za kujiendeleza katika taaluma hii.

Mkulima huyu anasema kujenga uhusiano mwema kati ya mwenye shamba alilokodisha na wateja wake, ameona kazi yake ikiendelea. Isitoshe, amejenga mtandao wake wa mauzo kutoka wateja wa maeneo Gathondeki, Uthiru, Kawangware, masoko ya Wangige na jijini.

Mboga zake huuzwa kwa vipimo vya kilo au mafungu. Kwa mfano; huuza brokoli kwa Sh50/60 wakati ziko kwa wingi ama Sh100 wakati wa kiangazi ilhali Cauliflower hunadiwa Sh40 wakati zinapatikana kwa wingi na Sh80 wakati wa kiangazi.

Zingine kama kunde na sukuma wiki huuzwa kwa mafungu kulingana uhitaji wa mteja.

 

Joseph Afwabi akionyesha nasari anayotumia kustawishia kilimo cha mboga. Picha/ Patrick Kilavuka

Afwabi anasema hupenda kujiongezea maarifa akisema hamna anayejishibisha kimaarifa. Yeye hutembelea wakulima wengine sehemu za Karinde na Wangige kubadilishana ufundi wa ukulima na kujionea mboga zingine zinazokuzwa sehemu hizo na kujaribu kuzipanda na amepata mafunzo tele.

Anasema hakuwa anapanda Lettuce lakini baada ya kupata maarifa ya kupanda mboga hizo sehemu alizotaja, amefua dafu kuzipanda na zinanawiri.

Kujaribu kuongeza idadi ya wateja, anasema huwapa nyongeza ya mboga kama njia ya kuimarisha mauzo na kuvutia wateja wengine wa kila siku na matabaka yote.

Kilimo kikiwa uti wa mgongo wa uchumi wetu, anawahimiza vijana kujitosa katika ukulima akisema utafaa kuliko kukaa bila cha kufanya na kujingiza katika visa viovu na kuathiri maisha yao.

Isitoshe, anawataka wafahamu kwamba dhahabu imetulia udongoni na wana uwezo wa kutumia mikono yao kwa kutia bidii ya mchwa kujitafutia kupitia ukulima. Hachelewi kusema kwamba, vijana washike jembe na hawatajuta!

You can share this post!

KAMAU: Kenya ihakikishe amani yake itaendelea kudumu

FAIDA YA UBUNIFU: Anatengeneza mitambo ya kilimo kusaidia...