Makala

AKILIMALI: Alifanya hesabu; ndizi zamlipa kuliko mahindi

September 19th, 2019 3 min read

Na PAULINE ONGAJI

KATIKA jamii nyingi Magharibi mwa Kenya, ndizi ni mojawapo ya mimea muhimu ambapo ni nadra kuingia katika boma la yeyote na kukosa.

Hii ni mojawapo ya sababu zilizomsukuma Mzee Musamula Patrick Deans, 61, mkazi wa kijiji cha Busaina, Mbihi, Kaunti ya Vihiga kujitosa katika aina hii ya kilimo.

Kwa Bw Musamula, udogo wa shamba lake haujamzuia kujihusisha na kilimo hiki ambapo huu ukiwa mwaka wake wa tatu tangu ajishughulishe vilivyo katika kilimo hiki, anazidi kufurahia mazao.

Licha ya kwamba shamba lake ni la ukubwa wa ekari 0.9 pekee, kwa sasa ana mimea 32 ya ndizi mbapo anashughulikia aina tatu ya mmea huu; fhia 17, valery na grand Nain.

“Nina mimea minane ya fhia- 17 na mimea mingine 25 ni mchanganyiko wa ndizi aina za valery na grand nain,” anasema.

Kulingana na Musamula, wazo la kujihusisha na kilimo hiki lilimjia baada ya kufanya utafiti na kugundua kwamba angepata mazao mengi kutokana na mmea huu ikilinganishwa na mahindi ambayo yanapandwa kwa wingi katika sehemu hii.

“Kwa mfano, niligundua kwamba shamba la ukubwa wa mita 7m x12m lingetoa gunia moja la kilo 90 la mahindi lenye thamani ya Sh4,000. Kwa upande mwingine, kwenye nafasi hiyo hiyo ningepanda mimea sita ya ndizi na baada ya mavuno ya kwanza, kila mmoja ungenipa migomba mitano ya ndizi, ikiuzwa kwa Sh800 inaleta Sh24,000,” aongeza.

Mbali na masuala ya kitamaduni, ari yake ya upanzi wa ndizi ilitokana na faida zinazotokana na mmea huu.

“Awali nilikuwa nahusika na kilimo cha mahindi, ambapo mazao hayakuwa na faida sana, tulikuwa tunatumia tu kwa lishe. Baadaye niligundua kwamba ndizi zingeniletea faida kubwa hasa ikizingatiwa kwamba bei yake sio mbaya sokoni,” aeleza.

Tangu aanze kulima amevuna zaidi ya migomba 60 ya ndizi, suala ambalo limempa matumaini mengi. Lakini haijakuwa rahisi kwa Musamula kwani kilimo hiki kina gharama zake.

“Nilikuwa na mashimo 32 ambapo kila moja lilikuwa likijazwa na toroli moja ya mbolea ya kawaida. Sokoni, bidhaa hii inanunuliwa kwa Sh80 kwa kila kilo. Aidha, shimo hilo lazima lijazwe kwa gramu 240 za mbolea ya DAT inayonunuliwa kwa Sh50 kwa kilo. Pia, uchimbaji mashimo haya una gharama kwani kila moja inagharimu Sh150. Mbali na hayo, lazima uwe tayari kuondoa magugu, shughuli inayofanywa mara moja kwa mwaka,” aongeza.

Fedha bado kidogo

Anasema kwamba bado hajaanza kunufaika vilivyo kifedha kutokana na kilimo hiki, lakini ufanisi wake katika matumizi ya kipande kidogo cha ardhi kuzalisha mazao mengi umekuwa kivutio cha wakulima wengine eneo hili.

Sasa penzi lake limeenda hatua zaidi ambapo ameanzisha mradi wa kutoa mafunzo kwa wakulima kuhusiana na kilimo cha ndizi.

“Mafunzo haya yanahusisha kuwafunza kuhusu jinsi ya kupanda mmea huu, vilevile thamani ya ndizi badala ya kujihusisha na upanzi wa mahindi pekee. Kwa wanaoishi katika eneo hili, hawahitaji kusafiri mwendo mrefu ili kujijulia kuhusiana na kilimo cha ndizi,” asema.

Kampeni zake zimempeleka vijijini na hata katika shule eneo hili huku zikiwavutia wakulima katika eneo hili na mbali.

“Kijijini, tayari nimepata watu wanne wanaotaka kujihusisha vilivyo na kilimo cha ndizi. Kwa upande mwingine, nimekuwa nikipokea mialiko ya kutoa mafunzo katika maeneo ya Kakamega na Eldoret,” aongeza na kusisitiza kwamba nia yake ni kueneza ufahamu wake kwa watu wengine na hasa vizazi vijavyo.

Anasema kwamba nia yake pia ni kuelimisha wakulima wa eneo hili na kuwapa ujuzi na mbinu za kujiimarisha kupitia kilimo tofauti, badala ya kujihusisha na upanzi wa mahindi na maharagwe pekee.

Penzi lake katika masuala ya kilimo lilianza mwaka wa 1981, ambapo wakati huo alikuwa akifanya kazi kama mtaalamu wa misitu eneo la Kitui.

“Nilikuwa nimehudhuria chuo cha mafunzo ya juu ambapo nilisomea uchumi wa elimu misitu (forest economics),” asema.

Lakini penzi lake kwa upanzi wa ndizi lilitokana na tatizo la ardhi ambalo kwa miaka limekuwa likiwakumba wakazi wa eneo la Vihiga.

“Hapa, kwa kawaida tuna vipande vidogo vya ardhi, na hivyo niligundua kwamba mahindi ambayo yalipandwa kwa wingi hayakuwa na manufaa mengi kwa jamii yetu,” asema.

Kwa hivyo kama mtaalamu wa misitu anasema kwamba alifanya utafiti kuhusu mmea ambao ungemletea thamani kubwa kwa kipande kidogo cha ardhi.

“Tayari watu katika eneo hili walikuwa wanajihusisha na kilimo cha ndizi, lakini tatizo ni kwamba hawakuwa wanafanya hivyo ili kuwaletea faida,” aeleza.

Na hivyo Februari 2016 alikata shauri ya kujitosa katika ukulima wa ndizi baada ya kupokea ufadhili kutoka kwa mradi wa ustawishaji uchumi (economic stimulus program), kwa ufadhili wa Serikali ya Kaunti ya Vihiga na ushirikiano na Wizara ya Kilimo.

Licha ya kuzama katika kilimo cha ndizi, hajaacha taaluma yake ya awali kama mtaalamu wa misitu. Amekuwa akishughulika katika upanzi wa miche na kuuza katika sehemu zingine humu nchini na mbali.

Lakini kwa sasa anazidi kuimarisha ujuzi wake kama mkulima wa ndizi na anasema kwamba yuko tayari kupeleka mafunzo yake katika sehemu zingine nchini.