Makala

AKILIMALI: Alilazimika kufunza wanunuzi kuijua stroberi, sasa soko limeiva

October 31st, 2019 3 min read

Na RICHARD MAOSI

ZAO la stroberi hufanya vyema katika sehemu yenye joto la kadri na miinuko ya mita 1500 hivi, udongo tifutifu wenye rutuba na ikiwa mkulima analenga kufanya ukulima wa stroberi itamlazimu kuendesha shughuli hii katika eneo lenye maji mengi lau sivyo itamlazimu kunyunyizia maji kila wakati.

Huu ndio ushauri wa Beth Wairimu Kinuthia, mwanzilishi wa mradi wa kukuza stroberi (Kenbet strawberry), katika eneo la Ol Joro Orok, Nyandarua.

Miongoni mwa mafanikio aliyopata Beth na mumewe ni pamoja na kupokea tuzo kama mkulima bora nchini Kenya, 2019 , Rais Uhuru Kenyatta alipotambua mchango wao katika sekta ya ukulima.

Akisaidiana na mumewe, Beth alianzisha mradi wa kukuza stroberi yapata miaka sita iliyopita kwa mtaji wa Sh6,000, lakini kabla ya hapo alikuwa ni mkulima wa kabeji,nyanya na karoti.

Alieleza kuwa walipanda miche ya stroberi kwanza, ambayo hatimaye ilisafirishwa katika kipande cha ardhi cha mita 15 kwa 15 mraba na ilichukua miezi mitatu kwa mazao yao kuwa tayari, ingawa haikuwa rahisi kupata soko la moja kwa moja.

“Watu wengi hawakuwa wakifahamu tunda la stroberi vilivyo, ikilinganishwa na matunda mengine kama vile maembe na machungwa,” aliongezea.

Anasema aina ya stroberi anazopanda zinafahamika kama Kenbet strawberry na zinaendelea kupata umaarufu mkubwa sio tu humu nchini, bali pia katika soko la kimataifa.

Wateja wake wengi wakiwa ni wamiliki wa maduka ya kijumla yanayovutia wanunuzi wengi, kwa sababu ndio hutumika kama daraja la kufikia soko la kimataifa.

Beth alianza kuchuuza matunda ya stroberi katika nyumba za watu akilenga kuwaelimisha wanunuzi kuhusu manufaa ya stroberi kabla ya kuwauzia, kwa Sh20 kila pakiti.

Ilichukua miaka minne kabla ya kushika mizizi, kisha akafanikiwa kulipanua soko la wanunuzi na sasa anaweza kujivunia matunda ya jasho lake kutokana na hatua kubwa aliyopiga chini ya miaka 10.

“Msimu usipokuwa mzuri sisi huuza stroberi kwa gramu 250 kwa Sh150 na wakati mwingine inaweza ikafikia 300,” alisema.

Beth anawahimiza vijana kujianzishia miradi midogo ambayo inaweza kuwaletea mapato madogo, na wasichague kazi hasa wakati huu ambapo gharama ya maisha ni kubwa.

Aidha anawashauri kuiga mifano ya wale waliofanikiwa katika sekta za kujiajiri, wakope mawazo yao na kuhudhuria makongamano ya kitaalamu ili kupanua mawazo yao ilmuradi waweze kujiboresha.

Alieleza kuwa soko lake kubwa ni kutoka kaunti ya Nyandarua,Nyeri, Nakuru, Eldoret na Ruiru ambapo anaamini kuwa matumizi ya tunda hili ni ya manufaa makubwa katika afya ya binadamu, mbali na kufanya biashara.

Anasema upandaji wa stroberi unaendana na ufugaji wa samaki, kwani maji yanayotumika katika vidimbwi vya samaki yanaweza pia kutumika kama mbolea katika shamba.

Lakini kama hauna mabwawa ya kufugia samaki, unaweza kutumia mbolea nyingine kama ile ya ng’ombe, mbuzi, kuku au kondoo.

“Kwa sababu upanzi wa stroberi unahitaji kiwango kikubwa cha maji, lazima mkulima awe na mfumo mzuri wa kumwagilia mimea yake maji mara kwa mara angalau mara nne kwa siku,” alisema.

Kila baada ya masaa manne stroberi zinastahili kumwagiliwa maji kwa robo saa, na endapo mkulima hatafanya hivyo majani ya stroberi hayatachanua na mimea itaishia kunyauka na kuwa hafifu.

“Ili kuzuia mimea yako isije ikashambuliwa na ukungu, virusi au magonjwa unaweza ukachanganya kitunguu saumu na dawa nyingine za kiasili kama vile pareto na matokeo yake huwa ni mazuri,” aliongezea.

Kinyume na awali watu wengi walifikiri kuwa hili ni zao la kichaka, lakini sasa wamepata kuelewa kwa kina umuhimu wa mmea huu endapo mkulima atakumbatia mfumo wa kisasa ndani ya kitalu (greenhouse).

Muda wa kukomaa

Zao la stroberi huchukua muda mfupi sana kukomaa na wakati mwingine huchukua mwezi mmoja kukomaa tangu kupandwa, ikitegemea na spishi yake na miti ya stroberi ikadumu kwa miaka mitatu mtawalia kabla ya kuzeeka na kufa.

Aidha ameongezea tunda hili thamani kwa kutengeneza bidhaa nyinginezo muhimu ambapo zinaweza kuchukua nafasi ya siagi.

Aina hiyo ya bidhaa ameipatia jina la Strawberry Jam ambayo haina aina yoyote ya kemikali zinazotumiwa viwandani kwani ni mchanganyiko wa matunda mengine kama vile machungwa na ndimu.

Anasema kuwa katika hatua ya kwanza matunda hukaushwa vizuri ili kuondoa maji yote kisha kwa mtambo maalum jam hutengenezwa na inaweza kudumu kwa mwaka mmoja bila kuharibika.

Jam inaweza kutumika kupaka katika mkate na ladha yake ni nzuri ukilinganisha na aina nyingine ya siagi inayotumika kupaka mkate.

Hivi sasa Beth anasema kuwa lengo lake kubwa ni kununua mtambo wa kisasa utakaomsaidia kutengeneza jam za hali ya juu.

Hili litamsaidia kuimarisha ushindani mkali katika sekta ya viwanda ambapo bidhaa za jam ni nyingi mojawapo ikiwa ni Zesta na siagi ya Blueband, ambazo zimekuwa zikitawala soko kwa muda mrefu akiamini kuwa hakuna jambo lisilowezekana.