Makala

AKILIMALI: Alitoka jijini akajiimarisha mashambani kupitia kilimo

February 21st, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

BAADA ya kuhitimu Stashahada ya Uhandisi katika masuala ya nguvu za umeme mwaka wa 1998 Bw John Muthee alihamia jijini Nairobi kutafuta ajira.

Alikuwa mwingi wa matumaini kwamba mara tu aingiapo jijini angepata nafasi ya kazi moja kwa moja, mradi tu awe ametuma maombi kwa kampuni na mashirika mbalimbali.

Hata hivyo, matamanio yake hayakujiri alivyotarajia.

Aliishia kufanya vibarua vya hapa na pale, na kulingana na simulizi yake akikokotoa hesabu ya malipo, mshahara aliopata haukuzidi Sh2,000 kwa mwezi wakati huo.

Anaeleza kwamba aliishi kuwa mtumwa wa madeni.

“Kila mwishoni mwa mwezi mapato yangu niliyaelekeza kulipa madeni na mikopo,” anasema Bw Muthee.

Baada ya kuhangaika si haba kukimu mahitaji yaliyozidi kwa kiwango kikuu pato lake, mwaka wa 2005 Muthee aliamua kuchukua hatua nyingine.

“Niliamua liwalo na liwe, sitaendelea kuwa mtumwa wa madeni tena jijini. Nilirejea mashambani,” anasema.

Mapato jijini, mbali na kushindwa kukithi mahitaji yake, hayakumudu kumpa nauli kurudi mashambani. Anafichua kwamba alilazimika kuomba nauli.

Kulingana na maelezo yake, ilikuwa hatua chungu, ila hakuwa na budi kufanya hivyo. Kilichomkereketa maini ni jinsi angeeleza jamaa na marafiki zake mashambani, ikizingatiwa kuwa wengi wanaamini maeneo ya miji ndiyo yana mapato ya kuridhisha.

Hata hivyo, Muthee alirejea, akijipa motisha “watazungumza, leo, kesho na kesho kutwa, mtondo na mtondogoo watakimya, maisha yaendelee”.

Alipowasili, alikuwa na lengo mawazoni “kuingilia kilimo”, uamuzi anaoutaja na kusifia kuwa wa busara zaidi katika maisha yake.

Kwa mtaji wa Sh1,200 aliingioa kilimo cha kabichi katika kipande cha shamba chenye ukubwa wa robo tatu. Anaeleza kwamba Mwenyezi Mungu alimjaalia mazao yakawa ya kuridhisha.

Mkulima John Muthee amegeuza sehemu kame kuwa nzuri kwa ajili ya kilimo. Anakuza maharagwe ya kijani, maarufu kama mishiri. Picha/ Sammy Waweru

Ni katika harakati hizo, Muthee alipevuka na kufunguka macho akaingilia kilimo cha maharagwe ya kijani, maarufu kama ‘Mishiri’, na ambacho amekidumisha kufikia leo.

Zao hilo pia ‘French Beans’ kwa Kiingereza analikuza kwenye ekari tano na nusu. Sawa na wakulima wengine waliozamia kilimo cha zao hilo, wateja wake ni kampuni au mashirika yanayouza nje ya nchi.

“Mkulima hutia saini mkataba nao, ambapo huelekezwa aina ya maharagwe wanayohitaji kulingana na soko,” Muthee afafanua.

Anaendeleza kilimo hicho eneo la Laikipia Kaskazini, Kaunti ya Laikipia. Eneo hilo ni nusu jangwa lakini katika mgunda wa John Muthee, utalakiwa na rangi ya kijani cha mishiri.

Licha ya kutegemea Mto Onterere, analalamikia baadhi ya kampuni za kilimo kubadili mkondo wa mto huo na kuuelekeza katika mashamba yao suala ambalo husababisha maji kupungua.

Ana jenereta ya kupampu maji, na kunyunyizia mimea kiungo hicho muhimu katika shughuli za kilimo.

Ili kuepuka changamoto za upungufu wa maji Emmanuel Olelei, mtaalamu wa kusindika mifereji ya kunyunyizia maji shambani, maarufu kama ‘Irrigation’ anahimiza wakulima haja ya kuwekeza pakubwa katika uvunaji maji. Anataja uchimbaji wa vidimbwi, mabwawa na vilevile mashimo, kama miongoni mwa njia kuvuna maji.

“Pia wakulima wakumbatie ununuzi wa vitekamaji kama vile matenki,” anashauri.

Kwa kufanya hivyo, mdau huyo anasema soko la bidhaa za kilimo halitakosa mazao, jambo ambalo anasema litapiga jeki wakulima pamoja na wafanyabiashara. Anaisihi serikali, za kaunti na ile kuu, kuongoza katika kampeni ya uvunaji maji.