Makala

AKILIMALI: Amegeuza eneo kame ardhi safi kukuza mapapai

August 13th, 2020 3 min read

Na SAMMY WAWERU

KIJIJI cha Rwika, eneobunge la Mbeere Kusini, kilichoko umbali wa kilomita 10 kutoka Mji wa Embu tunakaribishwa katika shamba la Simon Mwangangi na mapapai yanayoendelea kuvunwa.

Tunampata mkulima huyu akiwa katika harakati ya kupanua mradi wake anaouita Vuma Orchard. Ana ekari moja iliyositiri mipapai 960.

Utamu wa kazi ni pesa, na kwa Mwangangi utamu wa jitihada zake ni mapato anayoendelea kupokea kupitia mavuno ya mapapai, mazao ambayo yamemchochea kuongeza ekari nne zaidi.

Isitoshe, ana ekari nyingine moja ya mapapai katika eneo la Mwingi, Kaunti ya Kitui, yenye mipapai 1,000 anayosema yamesalia na mwezi mmoja pekee aanze kuyavuna.

Katika shamba lake la Mbeere Kusini, mapapai ya kudondosha mate yamening’inia mitini. Hukuza mapapai aina ya Solo Sunrise, eneo hilo ambalo ni nusu jangwa.

Kijana Mwangangi ambaye ana umri wa miaka 26 anachuma papai, analichambua na kumega kipande.

“Aina hii ina ladha tamu, ikilinganishwa na yanayokuziwa maeneo ya baridi,” anasema.

Anaendelea kueleza kwamba mengi yana wastani wa uzani wa gramu 650, kila tunda, ndani yakiwa mekundu badala ya manjano.

Mbali na ladha yake ya sukari, yanadumu muda wa wiki mbili baada ya mavuno, maumbile yanayoyafanya kuleta ushindani mkali sokoni.

Akiwa mzaliwa wa Mbeere Kusini, Mwangangi anasema wenyeji wengi hukuza mahindi na maharagwe kupitia maji ya mvua.

“Wanategemea msimu wa mvua. Wachache tuliokumbatia mfumo wa kunyunyizia mimea na mashamba maji kwa mifereji, tunalima mimea kama mapapai, matikitimaji, vitunguu, nyanya na Maharagwe ya Kifaransa,” anaeleza.

Mkulima huyo hata hivyo anasema alikumbatia kilimo cha mapapai, baada ya kugundua kuna uhaba wa zao hilo nchini.

“Niliona na ninaendelea kuona wanunuzi wakizunguka mashambani wakiulizia mapapai. Mahitaji yake ni mengi kuliko kiwango kinachozalishwa nchini,” anadokeza, akisema ana mapenzi ya dhati katika ukuzaji wa matunda hayo ili ‘alishe’ taifa.

“Nilihisi ni jukumu langu kuongeza mchango wa kuwepo kwa matunda haya nchini,” anasema. Mwangangi ni mhitimu wa Shahada ya Stadi za Kompyuta na Sayansi kutoka Chuo Kikuu cha Multimedia 2016.

Anasema aliingilia kilimo cha mapapai Oktoba 2019, na ni baada ya kufanya vibarua vya hapa na pale anavyotaja malipo yake kuwa ya chini mno.

Ili kupiga jeki mapato yake, anafichua kwamba pia alifanya shughuli ya uundaji wa matofali -Interlocking Soil Stabilized Blocks – ISSB.

“Utengenezaji wa matofali uliniwezesha kupata mtaji kuingilia ukulima wa mapapai, hatua iliyonigharimu Sh65,000,” anaeleza, akisema ekari moja anakodi Sh10,000 kwa mwaka.

Ili kuondoa gharama ya kununua miche, Mwangangi anasema kwa sababu alikuwa na muda mwingi wa ziada, alitengeneza kitalu na kujikuzia miche.

Anasema alinunua mbegu 1,000 kila moja akiuziwa Sh6.

Gharama nyingine ilikuwa ununuzi wa mifuko ya kutunza miche, mbolea na pia leba.

Upanzi

Mwangangi anasema ikiwa kuna mimea rahisi kukuza, ni mapapai. Kulingana naye, miche yake inapandwa kwenye mashimo yenye urefu wa futi mbili kuenda chini, na upana wa futi mbili pia.

“Nafasi kati ya mipapai iwe mita mbili, na kati ya laini, mita mbili na nusu,” anaelezea.

Daniel Mwenda, mtaalamu wa kilimo cha matunda, anasema udongo wa juu uchanganywe na mbolea, mchanganyiko huo urudishwe shimoni hadi kimo cha asilimia 95 iwapo shamba ni tambarere na hadi kimo cha asilimia 80 eneo la mwinuko.

“Upanzi wa mipapai ni sawa na ule wa miti mingine. Muhimu kufanikisha kilimo cha mapapai ni kuwepo na maji ya kutosha,” Mwenda anaeleza.

Mwangangi amekumbatia mfumo wa kunyunyizia maji kwa mifereji, ambapo hupampu maji kwa jenereta kutoka Mto Rupingazi, ulio umbali wa mita 800 kutoka shamba lake.

Katika shamba lake la Kitui, mkulima huyo anadokeza kuwa ana kisima cha urefu wa futi 10 na kinachotoa takriban lita 30, 000 za maji, awamu moja ya kupampu.

Wakati wa mahojiano, Mwangangi alisema mipapai huanza kuchana maua miezi mitatu baada ya upanzi.

“Miezi minne baadaye inaanza kutunda. Kimsingi, mipapai huchukua miezi saba kuanza kuzaa matunda, baada ya upanzi,” akasema, akieleza kuwa hunyunyizia maji mara moja au mbili kwa wiki, hasa wakati wa kiangazi.

Huku ekari yake moja inayozalisha matunda ikiwa na mipapai 960 mkulima huyo alisema kwa sasa anavuna wastani wa kilo 180 kila wiki, kilo moja ikinunuliwa Sh50 bei ya jumla.

“Wakati wa kiangazi bei ya mapapai hupanda maradufu, hadi Sh100 kwa kilo. Ninalenga kuvuna zaidi ya kilo 860 kila wiki, kufuatia mikakati niliyoweka kuimarisha na kunawirisha mipapai. Kero linalozingira ni mawakala wanaotupunja,” alisema.

Kwa mujibu wa maelezo ya Mwangangi, kila wiki akiwa anavuna kilo 180, kiwango cha chini, zidisha na Sh50 bei ya chini, ni bayana anaingiza mapato yasiyopungua Sh36,000 kwa mwezi.

Atakapolenga shabaha kuvuna kilo 860 kila wiki, atakuwa akitia kibindoni Sh172, 000 kila mwezi. Hiyo ni hesabu ya ekari moja pekee.

“Lengo langu ni kuwa na jumla ya ekari sita, tayari nina mbili, moja inayozalisha, nyingine imesalia mwezi mmoja pekee mavuno yaanze na nina nne ninazoendelea kufanya upanzi.”