AKILIMALI: Amegeuza taka ya mifupa, mayai kuwa mbolea asili

AKILIMALI: Amegeuza taka ya mifupa, mayai kuwa mbolea asili

WAIKWA KIBOI na CHARLES WASONGA

NYAKATI hizi wakulima wengi wamekumbatia matumizi ya mbolea asili badala ya zile za kisasa, almaarufu fatalaiza.

Hii ni kwa sababu mbolea asili sio ghali na haina kemikali zinazoweza kusababisha madhara kwa afya ya mwanadamu.Tafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa kemikali katika vyakula vilivyozalishwa kwa fatalaiza huchangia magonjwa sugu kama vile kansa.

Kwa mfano, imebainika kuwa mboga nyingi zinazouzwa mijini huwa zimetiwa kemikali hatari kama vile Nitrogen Peroxide, Ammonia na Lead, ambazo hutumika sana katika utengezaji wa fatalaiza na dawa za kuangamiza wadudu waharibifu shambani.

Ni kwa ufahamu huu ambapo Mzee Waweru Gikunju kutoka eneo la Gitero, Kaunti ya Nyeri, aliamua kuwekeza katika utengenezaji wa mbolea asili mnamo 2010.Gikunju, 73, anaendesha kazi hii katika kiwanda chake kilichoko katika eneo la viwanda vidogo mjini Nyeri – maarufu kama Nyeri Light Industries.

Katika mahojiano na Akilimali majuzi, asema malighafi yake huwa ni mabaki ya mboga, matunda, samadi za mifugo, mifupa, maganda ya mayai na aina mbalimbali za taka.

“Chokoraa ndio huniletea malighafi haya kisha natumia kutengeneza mbolea. Huniuzia ili nao wapate senti kidogo za kujikimu,” anasema.

Gikunju hununua mifupa Sh20 kwa kilo, nayo bei ya vitu hivyo vingine hutegemea kiwango chao cha madini katika mbolea itakayoundwa.Anaeleza kuwa mifupa na maganda ya mayai yana madini kama vile Calcium na Phosphorus ambayo ni muhimu sana katika uzalishaji wa nafaka na mboga.

“Katika kiwanda changu mimi husaga mifupa, maganda na vitu vinginevyo.” Anasema kando na utengenezaji wa mbolea kazi hiyo yake imechangia katika utunzi wa mazingira mjini Nyeri na viungani kwani anaondoa taka.

Je, alijifunza wapi kazi hii?Mzee Gikunju alipata mafunzo ya kutengeneza mbolea asili kwenye warsha moja iliyodhaminiwa na Chuo Kikuu Cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) mjini Nyeri mnamo 1993.

“Mafunzo hayo yaliendeshwa katika mkahawa wa Green Hills ambapo baadh ya wakufunzi walikuwa ni Naibu Chansela wa zamani Prof Nick Wanjohi,” aeleza na kuongeza kuwa mafunzo hayo ya wiki mbili yalitolewa bila malipo.

Baada ya mafunzo Gikunju alianza kutengeneza mbolea mnamo 2002 katika kibanda kidogo nyuma ya nyumba yake kijijini Gitero.

“Nilitengeneza mbolea kwa kuozesha nyasi na samadi ya mifugo kama vile ng’ombe, mbuzi, kondoo na hata kuku. Kwanza nilitumia mbolea hii shambani mwangu kabla baadaye kuanza kuwauzia majirani, aambao waliichangamkia sana.”

Muda si muda alihamisha kiwanda chake hadi eneo la Nyeri Light Industries mnamo 2010 baada ya kupata mtaji wa kununua mtambo wa kusaga malighafi mbalimbali kwa ajili ya kutengeneza mbolea.Kwa sasa mjasiriamali huyu huuza mbolea yake kwa bei ya Sh2,500 kwa kila gunia moja la kilo 50.

“Wakulima wengi wanapenda aina hii ya mbolea kwa sababu ya ubora wake. Kwa mfano, kando na kwamba ni bei nafuu huwa haiongezi asidi katika udongo shambani; kama inavyoshuhudiwa na fatalaiza ya Diamonium Phosphate (DAP) inayotumiwa kwa wingi msimu wa upanzi wa mahindi,” alieleza Mzee Gikunju.

Vile vile, wakulima wengi wamekimbilia mbolea hiyo asili kwani zile za kisasa – kama DAP na Calcium Ammonia Nitrate (CAN) – ni bei ghali ambapo gunia la kilo 50 linagharimu Sh3,500.

You can share this post!

AKILIMALI: Mbinu safi ya kuzalisha mbegu za viazi vya...

Kocha Jesse Marsch wa RB Salzburg kujaza nafasi ya...