Makala

AKILIMALI: Amepata tuzo mbalimbali kwa ufugaji bora wa mbuzi

June 20th, 2019 2 min read

Na PETER CHANGTOEK

SHAMBA lijulikanalo kama Mwihoko Dairy Goat Farm ni maarufu mno, kiasi cha kutambulika na kutuzwa kwa tuzo mzomzo, katika maonyesho mbalimbali ya zaraa.

Robert Macharia ni mmiliki wa shamba hilo, lililoko katika eneo la Mwihoko-Githurai.

Shamba lake, japo ni dogo, lina mbuzi wengi. Saizi ya shamba hilo ni futi 20 kwa 20, na lina mbuzi wa maziwa zaidi ya ishirini waliokomaa.

“Nilianza kushughulika na ufugaji wa mbuzi mnamo 2013. Nilianza kwa kumfuga mbuzi mmoja wa kienyeji ambaye nilipewa na babangu kama zawadi. Wakati huo nilikuwa nikikamua maziwa lita moja kutoka kwake,” asema mkulima huyo mwenye umri wa miaka 37.

Mja akiingia nyumbani kwa mkulima huyu, ni nadra mno ang’amue kuwa wapo mbuzi wanaofugwa pale.

Macharia anatuarifu kuwa yeye huhakikisha kwamba usafi unadumishwa katika vibanda ambavyo yeye huvitumia kuwafuga mbuzi wake.

Vibanda hivyo, ambavyo mkulima huyo huvitumia kwa ufugaji wa mbuzi, viliinuliwa juu futi mbili kutoka ardhini, wakati vilipokuwa vikijengwa, kusudi kinyesi cha mbuzi kianguke chini ili kuirahisisha kazi ya kulisafisha eneo hilo.

Macharia huwalisha mbuzi hao mara moja kwa siku, kwa kuitumia lishe aina ya ‘hay’ iliyotengenezwa kwa nyasi aina ya ‘Rhodes’ na ‘Lucerne’. Aidha, yeye huwapa chumvi ya kuramba.

“Kama unataka kuwa na ufugaji wa mbuzi uliofana na wenye tija, basi unahitajika kuwa na usimamizi bora. Pia, unapovijenga vibanda, unafaa kuvijengea mahali pasipokuwa na upepo kwa sababu mbuzi huathiriwa sana na nimonia,” mkulima huyo ashauri.

Kabla hajajitosa katika kilimo hicho, alikuwa akifanya kazi katika kampuni ya SportPesa, kwenye idara ya usafirishaji.

Aliiacha kazi hiyo mnamo 2016 ili kushughulika na zaraa hiyo, ambayo anasisitiza inalipa vyema.

Mbuzi wa Robert Macharia eneo la Mwihoko. Picha/ Peter Changtoek

Mkulima huyo, ambaye hufuga mbuzi aina ya Alpine, amekuwa akipata ujuzi zaidi kuhusu ufugaji wa mbuzi, kutoka mtandaoni, katika maonyesho ya kilimo na kutoka kwa wakulima waliobobea, ambao hutagusana nao.

“Nimekuwa nikipenda ufugaji wa mbuzi tangu utotoni. Hii ni kwa sababu kule nyumbani tulikuwa tukiwafuga mbuzi, japo ni wale wasiokuwa na manufaa makubwa,” afichua Macharia.

Mnamo 2014, aliwanunua mbuzi wawili wa kike aina ya Kenya Alpine, kwa Sh25,000 kila mmoja. Wawili hao walikuwa na mimba na wakazaa baada ya muda wa miezi minne.

Hapo ndipo alipoamua kuwauza mbuzi aliokuwa nao ili ashughulike na ufugaji wa wale walioboreshwa (hybrid).

Akaanza kutafuta soko la kuyauzia maziwa, kwa kuwajuza watu.

Punde si punde, akawa na wateja kadha wa kadha. Miezi michache baadaye, akamnunua mbuzi mwingine.

“Mbuzi mmoja anaweza kukupa lita mbili za maziwa kwa siku, akilishwa vyema. Nilikuwa nikipata lita tatu, na nilikuwa na wateja waliokuwa tayari, jambo lililonisukuma kutia bidii zaidi,” asema mkulima huyo, ambaye ni baba wa mtoto mmoja.

Kufikia 2016, mbuzi wake walikuwa wameongezeka maradufu, na akaamua kuwapeleka kwa maonyesho ya kilimo ya Nairobi, na hapo ndipo alipopata mwangaza, maadamu alitambuliwa kuwa mfugaji bora wa mbuzi na kutambuliwa pia mwaka uliofuatia kwa uzalishaji bora wa mbuzi.

Kwa wakati huu, yeye hukamua maziwa lita 30 kila siku na huwauza mbuzi waliokomaa kwa wakulima wengine.

Uuzaji

Mkulima huyo huyauza maziwa hayo kwa Sh200 kwa lita, na humuuza mbuzi mmoja aliyekomaa kwa Sh40,000-Sh60,000.

“Wateja wangu wengi ni wale walioagizwa na madaktari kuyatumia maziwa ya mbuzi kwa kuwa yana madini ya Calcium kwa wingi, huimarisha kinga na hayana kolestero,” adokeza.

Macharia anapania kuongeza idadi ya mbuzi anaowafuga ili kuchuma zaidi kutokana na zaraa hiyo adhimu.

Aidha, yeye huwapa mafunzo wakulima kuhusu mbinu aula za ufugaji wa mbuzi.

Pia, anaazimia kuuasisi ushirika pamoja na wafugaji wengine wa mbuzi.

“Ipo haja ya kuanzisha ushirika kwa sababu wanaohitaji maziwa ni wengi ila wauzaji si wengi, kwa hivyo tukija pamoja, tutakuwa na maziwa ya kutosha,” asema, akiongeza kwamba endapo hilo litatimia, wataanza kutengeneza bidhaa zitokanazo na maziwa, mathalani jibini na maziwa gururu.