AKILIMALI: Anaelewa kuhangaikia nafsi yake kwa njia halali

AKILIMALI: Anaelewa kuhangaikia nafsi yake kwa njia halali

Na SAMMY WAWERU

RATIBA ya kila siku ya John Muiboro Ngugi ni yenye matukio na shughuli chungu nzima.

Hurauka alfajiri na mapema kujiandaa kusukuma gurudumu la maisha, na itimiapo saa kumi na mbili jua linapoanza kuchomoza, miale huchomoza katika sehemu yake ya kazi.

Ni mpishi hodari wa chapati eneo la Zimmerman, Nairobi.

“Upishi wa chapati, sijauanza leo, jana wala juzi. Nina miaka kadhaa,” Ngugi anadokeza.

Afisi yake ni kibanda cha mbao, paa likiezekwa kwa mabati. Huku mapishi ya kitafunio cha chai na kitoweo anachoandaa kikiwa kimekumbatiwa na wengi.

“Huwa nakanda unga wa chapati kwa kuongezea karoti iliyosagwa ili kuziongeza ladha,” anaelezea.

Licha ya kuwa hajaingia katika taasisi yoyote ile ya mapishi kunoa bongo na maarifa, ni ubunifu ambao umefanya huduma zake kuwa za kipekee na kivutio kwa wengi.

Hata ingawa ana mipango mikuu kuboresha kazi yake, Ngugi anasema aliingilia upishi wa chapati miaka minne iliyopita.

Aidha, alianza kama kibarua katika mojawapo ya mkahawa jijini Nairobi.

“Nimefanya kazi katika hoteli kadha, jukumu langu likiwa kupika chapati pekee,” anasema.

Unapotangamana naye, kinachojitokeza bayana ni kijana mwerevu, mkakamavu na mkwasi wa bidii.

Mtajie baadhi ya kazi ngumungumu na zenye uzito, atakueleza amezifanya ili kujiendeleza kimaisha.

Kwa Ngugi, 30, hamna kazi yenye uzito, mradi tu ni halali na itampa mkate wake wa kila siku, imlipie bili na aweze kuweka akiba kwa sababu ya siku za usoni.

Si mchaguzi wa gange, kauli mchagua jembe si mkulima ikimpa motisha ipo siku atajiunga na ligi ya mamilionea, mabilionea na Mungu akimjaalia awe trilionea.

John Muiboro Ngugi pia ni mtangazaji, akiwa studioni katika kituo cha redio cha Hood FM. Picha/ Sammy Waweru

Kabla aanze mapishi ya chapati, Ngugi anafichua amewahi kufanya kazi ya kuchuuza nguo, ujenzi, kupiga sakafu deki, shamba boi, na pia kufunza.

“Mimi ni hasla anayejua kujitafutia, huwa sibagui ajira,” anaelezea, akihimiza vijana wenza kuzika katika kaburi la sahau dhana “nimesoma, nina cheti cha Stashahada, Digrii, Shahada ya Uzamili, Shahada ya Uzamifu, hivyo basi kazi inayonifaa ni ya afisi pekee yenye mshahara mnono.”

Barobaro huyu ana cheti cha masuala ya kompyuta, na alipoona kazi za ofisi zimempiga chenga, hakuzembea.

Ngugi anaeleza kushuhudia kipindi kigumu mwaka uliopita, 2020, janga la Covid-19 lilipoathiri Kenya na dunia kwa jumla.

Ni janga la kimataifa ambalo lilisababisha yeye pamoja na wafanyakazi wenza katika hoteli aliyokuwa ameajiriwa, kupoteza ajira.

“Ulikuwa mwaka mgumu. Miezi kadhaa nililemewa kulipa kodi ya nyumba, kwa sababu vibarua havikuwa vikipatikana. Hata hivyo, niliibuka mshindi,” anaiambia Akilimali.

Sekta ya hoteli na utalii, ni kati ya zilizoathirika zaidi na virusi vya corona.

Ngugi akiwa kijana aliyepitia mengi maishani, alijituma katika vibarua vilivyopatikana na hatimaye akamudu kufungua kazi ya kupika chapati.

Anafichua ilimgharimu mtaji wa Sh3, 000 kuanza safari. “Kwa siku, huandaa chapati zisizopungua 120,” anadokeza.

Aidha, kila chapati huiuza Sh10 pekee, kwa siku wakati ambapo mauzo ni ya chini akiweka kibindoni faida isiyopungua Sh550.

Vile vile, hukaanga soseji, hivi karibuni akipangia kujumuisha mayai.

Mbali na kipaji cha upishi, mjasiriamali huyu ni mtangazaji wa redio, Hood FM, kituo kinachopeperusha matangazo yake kupitia mitandao ya kijamii.

“Nimekuwa redioni kwa zaidi ya miaka mitatu, hata ingawa ni kazi ya kujitolea, bila malipo,” Ngugi, maarufu kama Mhenga wa Lugha kwa mashabiki wake, anasema.

Isitoshe, yeye pia ni mtunzi wa mashairi.

Huku akiwa produsa na mtangazaji wa makala ya Tusemezane, kutokana na milima na mabonde aliyopitia, Ngugi huhamasisha vijana kuepuka kushiriki uhalifu, matumizi ya dawa za kulevya na mihadarati na pia mimba za mapema.

You can share this post!

AKILIMALI: Sungura ‘mjanja’ ila thamani yake kubwa...

Majaji wakemea Uhuru, wamzuia kujadili kesi, BBI