Makala

AKILIMALI: Anajaribu kurejesha umaarufu wa karakara Nyeri

June 20th, 2019 3 min read

Na DUNCAN MWERE

MIAKA ya tisini vijana wengi walikuza matunda aina ya karakara (Passion Fruits) katika maeneo mengi ya Mlima Kenya.

Ni wakati huo walipong’amua kuwa manufaa yake ni maridhawa na ukuzaji wake haukuwa na shida nyingi kwani ilikuwa mara ya kwanza kukuzwa kwa wingi.

Enzi hizo wengi walifanikiwa zaidi maishani kwani soko lake lilikuwa nafuu. Kadri siku zilivyosonga ndivyo ukuzaji wa tunda hili ulisahaulika.

Katika kitongoji cha Kiriko Gachuiro hatua kadhaa kutoka Mji wa Karatina, eneobunge la Mathira jimboni Nyeri, utakutana na mkulima anayeendeleza zaraa hii na kufanikiwa zaidi.

Peter Nderitu amebakia kuwa kati ya wakulima wachache wanaovuna ghawazi lukuki msimu baada ya mwingine kutokana na matunda haya.

Katika kipande hiki cha urithi, Nderitu amekitumia barabara na kukiuka ada ya kukuza mimea inayokuzwa katika maeneo haya.

Kwa kutunza mimea yake vyema anafichulia Akilimali kuwa amepata mihela si haba kuliko wanaopanda kahawa anaopakana nao.

Anaeleza oda ya matunda haya ni ya hali ya juu na wakulima wachache wameshindwa kuwakidhia wateja wao bidhaa hii.

“Ni wazi kuwa wakulima wa karakara ni wachache mno huku walaji ni wengi sana,” asema. Yeye huuza matunda yake katika soko la Karatina lililo la pili kwa ukubwa barani Afrika.

Aidha soko lake liko katika taasisi kama vile za elimu na afya kwani walimu na matabibu huwarai wanafunzi na wagonjwa kula matunda haya kwa wingi.

Gwiji huyu anawahimiza wakulima na hasaa vijana kukuza matunda haya ikiwa ni njia mojawapo ya kuchuma riziki na kupuzilia mbali kauli ya ‘hakuna ajira’.

Kwa wanunuzi wa jumla yeye huwauzia shilingi 100 kwa kilo.

Japo huchuma matunda yake kila wiki, kwa mwezi anaweza kutia kibindoni takriban shilingi 70, 000.

Mkulima anahitajika kuandaa shamba lake na kuondoa magugu na maotea yote.

Mmea huu aghalabu hufanya vyema hususan maeneo yalio na joto la wastani.

Nderitu anaeleza Akilimali kuwa msimu wa mvua mmea huu hukabiliwa na changamoto kadhaa jambo linalochangia mkulima kuvuna mavuno yasio ya kuridhisha.

Mkulima anahitajika kuchimba shimo lenye urefu wa futi moja.

Kisha baada ya hapo achanganye na mbolea ya mifugo. Ahakikishe mchanga wenyewe ni mwepesi na cha msingi asiweke mbolea nyingi katika shimo pindi anapopanda.

Fatalaiza aina ya DAP ni mwafaka wakati wa kupanda.

Ili kuhakikisha maua ambayo hatimaye huwa tunda yanadumisha ubora wake na kutoa mazao bora, hana budi kuweka fatalaiza aina ya 17.

Muda wa miezi kati ya miwili na mitatu mkulima anashauriwa kuondoa matawi yasiotakikana, prunning.

Kipindi hiki ni mwafaka kwa kupulizia dawa baada ya kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa nyanjani walioidhinishwa na Wizara ya Kilimo Nchini.

Dawa hutofautiana kutegemea na mchanga na hali ya hewa ya eneo.

Kutoka mmea mmoja hadi mwingine aache nafasi ya mita mbili unusu hadi tatu sawa na hiyo upande wa upana kutoka laini moja hadi nyingine.

Hewa

Sababu mbili kuu ni kuwa mmea utapata hewa inayofaa.

Pili mkulima hupata nafasi ya kutunza mmea huu bila usumbufu wowote.

Vifaa vingine muhimu ni nyaya na vikingi.

Kuhusu nyaya mkulima huyu anaeleza baadhi yazo ni hatari kwani hushika kutu na kisha uzito wa matunda unapoongezeka huanguka na mazao kuharibika.

Kuhusu vikingi mkulima anafaa kutumia miti inayofahamika kama ‘Hardwood’ ili kuzuia kushambuliwa mara kwa mara.

Mkulima Nderitu aliye na jitihada za mchwa alisema kuwa ukosefu wa kipande kikubwa cha ardhi ni kizingiti kikuu kinachochangia kutopiga hatua kuu maishani.

Kuhusu maji, anamvulia kofia mbunge wa eneo hili Rigathi Gachagua kwa kuimarisha miundo msingi katika sehemu hii. Mojawapo ni kuhakikisha wenyeji wa hapa wanapata maji na hili limechangia walio na ari ya ukulima wanatimiza ndoto na maazimio yao.

Nderitu amekuwa akitoa mafunzo ya kilimo katika shamba lake na kuuza miche bora ya karakara.

Anafahamika na wengi kutokana na mbinu za kupandikiza (Grafting).

Ujuzi na uelewa huu kuhusu mimea ainati alipata baada ya kuhudhuria makongamano na maonyesho ya kilimo katika kaunti mbalimbali.

Ombi la Nderitu ni moja; akipata mwanya na chuo cha kutoa mafunzo ya kilimo anaweza kufanya makuu mathalani kuelimisha jamii na vijana wanaosubiri kuajiriwa ajira za hadhi.