AKILIMALI: Anajichumia kwa kuunda unga wa mabuyu na mafuta ya nazi jijini Nairobi

AKILIMALI: Anajichumia kwa kuunda unga wa mabuyu na mafuta ya nazi jijini Nairobi

Na WINNIE ONYANDO

MABUYU ni tembe ambazo Wapwani wamezimumunya kwa miaka mingi, baada ya kuongezwa rangi tofauti, maarufu ikiwa nyekundu, na sukari.

Utamu wake umevutia wengi katika maeneo tofauti nchini na kuyapatia umaarufu mkubwa.

Lakini, mmea huo unaofahamika kwa kimombo kama baobab, una matumizi tele ambayo wengi wamepata kuyagundua katika siku za hivi punde, na kuvumisha zaidi umaarufu wake hata ughaibuni.

Katika mtaa wa Mlango Kubwa karibu na shule ya Upili ya Pangani, Akilimali ilikutana na Abdalla Akuku,33, ambaye anaendesha biashara ya kuuza bidhaa asilia kama za mafuta, unga wa mabuyu na pia nyingine zinatokana na mabuyu.

Mwanamume huyo ambaye ana shahada ya Sayansi ya Biokemia kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta anaeleza kuwa anaendelea kufanya shahada za Uzamili na Uzamifu katika somo la Dini ya Kiislamu Chuo Kikuu cha Madina Saudi Arabia.

Abdalla anaeleza kuwa japo wengi waliathiriwa pakubwa na janga la corona, kwake janga hilo lilimfungulia ukurasa mpya maishani.

Anaeleza kuwa janga hilo lilimtuma kuanzisha biashara yake ya Najma Organics Agosti 2020, biashara ambayo imemsaidia kujikimu pamoja na familia yake.

Anakiri kuwa hajawahi kuwa na mawazo ya kuanzisha biashara, lakini baada ya janga kuzuka, fikra hizo zilimuelekeza kwa kile anachokifanya sasa kwa bidii.

Katika karakana yake, Abdalla anauza nazi pamoja na mafuta yake na bidhaa nyingine zinazotokana na mnani, pamoja na bidhaa zinazotoka kwa mbuyu kama mabuyu na unga wa mabuyu.

Anasema kuwa anajaribu kuwahamasisha watu kuhusu umuhimu wa kutumia mabuyu na unga wake kwa kuwa wengi hawafahamu umuhimu wake katika afya ya binadamu.

Umuhimu wa mabuyu

Katika kuunda unga wa mabuyu, Abdalla alinunua mashine spesheli ya kusaga matunda ya baobab ambayo kwa siku anaweza kusaga gunia moja.

Kwanza kabisa, Abdalla anatueleza kuwa matunda ya baobab huwa na kalsiamu, potasiamu na aina ya Vitamini C ambazo husaidia katika kujenga mwili.

Kwa kawaida, mwili wa binadamu huhitaji aina ya Vitamini C ambayo hupatikana kwenye matunda kama vile machungwa. Japo hili linahitajika, si kila mmoja anaweza kununua matunda kila siku.Hapo ndipo mabuyu yanatumika.

Kulingana na tafiti mbalimbali zilizofanywa na mashirika tofauti, ni dhahiri kuwa mabuyu pamoja na unga wake hubeba zaidi ya asilimia 50 za kalsiamu ambayo husaidia katika kulainisha ngozi, kupoteza uzito na hata kuboresha afya ya moyo kwa walio na matatizo kama hayo.

Mafuta ya mmea huo pia hutumika katika kuboresha ukuzaji wa nywele na kufanya nywele kuwa laini na kung’aa. Pia husaidia wenye chunusi mwilini, kupunguza mwasho mwilini na hata kulainisha ngozi,

Kwa siku, anasema Abdalla anaweza kuuza bidhaa za zaidi ya Sh2,000. Hii ni kwa sababu wengi hawajapata kufahamu umuhimu wa mbuyu.

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali iangamize madhara ya sigara

AKILIMALI: Sungura ‘mjanja’ ila thamani yake kubwa...