Makala

AKILIMALI: Anaoka keki kuuza sehemu ya kipato akitumia kusaidia mayatima

July 2nd, 2020 2 min read

Na FARHIYA HUSSEIN

MIAKA minne iliyopita, hakuwa na nia ya kumiliki kiwanda cha kuokea mikate na keki nchini.

Amina Khalid alioka keki yake ya kwanza akiwa na umri wa miaka 17 ambapo ilikuwa ni siku ya kaka yake kufunga shule.

“Nilioka keki kama njia ya kujifurahisha, lakini kaka yangu alinisihi nimwandalie keki ya darasa lao nzima,” anasema Amina ambaye kwa wakati huo anakiri hakutegemea wala kudhani kwamba ni hapo ndipo angetoa wazo la kuanzisha biashara anayotegemea leo hii.

Kilichomchochea, hata zaidi, anasema, ilikuwa ni majibu aliyopokea ikizingatiwa darasa lote lilikuwa likiongelea “ile keki.”

“Wanafunzi katika darasa la kaka yangu walijiramba vidole vyao na hapo ndipo niligundua nilikuwa nimelalia fursa ya biashara,” anasema.

Binti huyo sasa ana umri wa miaka 21 na anakiri hajawahi kuingia katika darasa lolote kupata mafunzo ya jinsi ya kuoka keki maishani mwake.

Yeye anasema anajifunza kutoka kwa makosa anayofanya na majibu anayopata kutoka kwa wateja.

“Jaribio langu la pili katika kutengeneza keki lilifanikiwa, lakini mapambo yalikuwa ya kutisha. Tangu hapo nimejibidiisha na kujitahidi zaidi kuboresha ujuzi wangu wa kuoka na kuandaa keki,” anasema Amina.

Faida yake ya kwanza kama mwokaji ilikuja alipoandaa keki ya chokoleti ya kilo tano ambayo aliuza akapata Sh4,000.

Amina Khalid mwenye umri wa miaka 21 anamiliki kiwanda cha kuokea mikate na keki. Yeye huuza vyakula hivyo huku asilimia fulani ya pesa anazopokea akitumia kuwasaidia mayatima. Picha/ Farhiya Hussein

Kinachomtofautisha na waokaji na wauzaji keki wenzake ni kwamba kwake asilimia fulani ya pato kutoka kwa keki anazouza huenda kwa mashirika ya misaada.

“Nina mpango wa kufanikisha elimu kwa kuwalipia watoto mayatima watano kila mwaka ili baadaye waweze kujitegemea. Tayari, nimefundisha wanafunzi 10 ambao bado wanaendelea na kozi ya masuala ya uokaji, “anasema.

Kupitia ustadi wake wa ajabu, alifungua kiwande chake cha kuokea mikate na keki mwenyewe akakiita Minat Bakery.

“Nilikuwa na onyesho langu la kwanza eneo la City Mall, Mombasa ambapo nilikuwa na umri wa miaka 19. Baada ya maonyesho, niliona haja ya kukipa jina kile kiwanda changu. Mwanzo nilitaka kusajili jina Minny Bakery, lakini kulikuwa na kampuni nyingine yenye jina hilo,” anasema.

Siku chache baadaye, alilazimika kuipa jina Minat Bakery.

Amina Khalid mwenye umri wa miaka 21 anamiliki kiwanda cha kuokea mikate na keki. Yeye huuza vyakula hivyo huku asilimia fulani ya pesa anazopokea akitumia kuwasaidia mayatima. Picha/ Farhiya Hussein

Amepokea tuzo mara kadhaa kwa mafanikio yake. Miongoni mwazo ni tuzo ya mwokaji wa umri wa chini aliyejifundisha mwenyewe, tuzo ya nambari mbili kategoria ya kurembesha keki katika muda wa dakika nne, na tuzo ya nambari ya tatu katika kategoria ya Ushindani wa Keki ya Haruri yaani wedding glamorous cake.

Alipoanza yote alijua ni kucheza tu na mchanganyiko wa viungo, lakini leo hii Amina ana ustadi na anaoka mikate ya harusi, keki na dessert, mkate wa boflo, kuki – cookies – keki zilizoboreshwa miongoni mwa vitamu vingine.

Biashara yake inategemea upatikanaji wa wateja.

“Katika miezi mingine ninaweza kupata oda chache kama kuoka keki mbili au hata tatu, lakini miezi mingine uhitaji huwa juu ambapo ninaweza kupata oda kuoka keki 15 kwa mwezi ambapo bei hutofautiana kulingana na ladha na saizi,” anasema.