Makala

AKILIMALI: Anaona akifika mbali kwenye ukuzaji karakara

April 4th, 2019 2 min read

Na PETER CHANGTOEK

ALIANZA kujishughulisha na ukuzaji wa mikarakara mwaka uliopita, lakini kwa kuwa ukuzaji wa mmea huo unaonekana kuwa wenye tija kwake, ameamua kujizatiti na kutotazama nyuma asilani.

Alloys Mulla ambaye anashughulikia kilimo hicho katika eneo la Butula, Kaunti ya Busia, amekuwa akiikuza mimea mingine kama vile mianzi, mtama, ndizi, miongoni mwa mimea mingineyo.

Hata hivyo, kwa kuwa mimea kama vile mianzi na ndizi huchukua muda mrefu kukomaa, alikata kauli kujitosa katika uzalishaji wa makarakara kwa kuwa uzalishaji wa matunda hayo huwa hauchukui muda mrefu kabla hajapata faida.

Mulla, ambaye hupenda mno kuyasoma makala ya zaraa katika jarida la Seeds of Gold, katika gazeti la Saturday Nation alianza kujitosa katika shughuli hiyo pindi tu alipoyasoma makala kumhusu mkulima mmoja aliyekuwa ameangaziwa katika Kaunti ya Kakamega.

“Nilianza kushughulika na ukuzaji wa mikarakara mwaka uliopita, baada ya kusoma makala kumhusu Nahashon Asava, aliyekuwa akikuza mikarakara kule Kakamega. Nilimpigia simu na akaniambia alikuwa na miche, na nikanunua kutoka kwake,’’ asema mkulima huyu akiongeza kuwa aliinunua miche 100 na akaongezewa mingine 13.

Hata hivyo, kwa wakati huu ana mimea 105, baada ya mingine kukosa kukua.

“Niliinunua kwa Sh10 kila mmoja. Nilikuwa nimeyachimba mashimo ya kupanda kwayo na kuweka mbolea kutoka kwa kuku,’’ aongeza Mulla.

Anasema kuwa ni wakulima wachache mno ambao hushughulika na ukuzaji wa mimea hiyo ya mikarakara.
Ameikuza mimea yake katika shamba robo ekari, na wakati alipokuwa akiipanda, aliiacha nafasi ya mita tatu kwa mita tatu, kutoka kwa mmea mmoja hadi kwa mwingine.

Mkulima huyo ameutengeneza ua kwa kuitumia seng’enge maalumu kusudi awazuie wezi wenye nia ya kuyaiba matunda shambani.

“Watu wanaoingia shambani na kuyaiba matunda huwafanya wakulima wanaoyazalisha matunda kukata tamaa,’’ afichua.

Kwa sababu ya jua kali na kiangazi kilichopo kwa wakati huu katika eneo hilo, mkulima huyu ameyaweka maranda (sawdust) katika eneo lenye mimea ili kusaidia kuyahifadhi maji au unyevu mchangani.

Hali kadhalika, yeye huyaokota majani ya mianzi na kuyatandaza katika eneo lililo na mimea ili kusaidia kuyahifadhi maji.

Majani hayo, vilevile, hugeuka kuwa mbolea wakati yanapooza, na kuongeza rotuba kwenye mchanga, na hivyo kuboresha kiwango cha mazao anayoyazalisha.

Maadamu ana mimea ya mianzi, Mulla amevichomelea vikingi vya mianzi karibu na kila mmea wa mkarakara, ili visaidie mimea kutoanguka wakati inapoyazaa matunda.

Japo hakuyachuma matunda mengi katika msimu wa kwanza, mkulima huyo anatarajia kuyachuma matunda takribani magunia kumi, katika msimu unaonukia.

Tayari matunda hayo yameanza kuiva, na anatarajia kuanza kuyauza kuanzia mwezi huu wa Aprili.

“Msimu uliopita niliyauza magunia mawili makubwa. Gunia moja kubwa la matunda hayo hapa, yanauzwa kwa Sh3,000, lakini nikipeleka niuze katika maeneo mengine kama vile Busia na Kisumu, nitauza kwa Sh6,000,’’ asema, akiongeza kuwa matunda hayo aghalabu hayakosi soko.

Dukakuu mjini Mumias

Pia, anaongeza kuwa kuna dukakuu moja lililopo mjini Mumias, ambalo linanuia kuweka mkataba naye ili awe akiyauza matunda yake huko.

“Sitaki niandikiane mkataba nao halafu nikose kuyapeleka,’’ asema.

Ili mimea ikue kwa njia nzuri, mkulima huyu anasisitiza kwamba ni jambo aula kupogolewa kwa mimea (kukata majani na matawi yasiyofaa).

“Ukipogoa, mimea inaanza kunawiri na kuwa na matunda makubwa,’’ afichua mkulima huyo, akiongeza kuwa ana rafiki yake ambaye ni mwanaagronomia (mtaalamu wa kilimo), ambaye humsaidia.

Japo mkulima huyo ana mimea mingine anayoikuza katika shamba lake, anasisitiza kuwa ana nia ya kushikilia kikiki shughuli ya ukuzaji wa mimea izaayo matunda ya kila nui, maadamu matunda yana faida.