Makala

AKILIMALI: Anatumia kozi ya teknolojia kuboresha ufugaji wa kuku

August 23rd, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

KILOMITA chache kutoka barabara kuu ya Thika-Garissa, Regina Njeri ana kila sababu ya kutabasamu kufuatia kuimarika kwa hitihada zake katika ufugaji wa kuku.

Chicks Sellers Two Rivers, ni mradi unaomilikiwa na mwanadada huyu eneo la Makongeni, Thika, ambapo huangua vifaranga.

Vilevile, Njeri hufuga kuku wanaofanikisha juhudi za kupata mayai kuanguliwa vifaranga, na mengine kuyauza.

“Ninafanya ufugaji wa kuku wa kienyeji wa kisasa, kama vile Kuroiler na Rainbow, ambao miaka miwili baadaye wakikomaa ninawauza kuwa wa nyama,” asema mfugaji huyu. Kienyeji wa kisasa, ni kuku wenye asili ya India na wale wa Bara Afrika.

Njeri, mama wa watoto wawili, alihitimu Stashahada ya Teknolojia na Mawasiliano, IT, 2012.

Kulingana naye kati ya 2012 – 2015, alifanya ufugaji wa nguruwe na ndege aina ya kware.

Aliwekeza zaidi ya kima cha Sh500,000.

“Nilikadiria hasara, hasa kware ambao walikula bila huruma ilhali hawakunipa mapato,” anaeleza.

Mfugaji huyu anaendelea kusimulia kwamba hakuwa budi ila kusitisha shughuli hizo zilizomuacha bila mbele wala nyuma. Kware, aliwapa majirani na wengine kuwafungulia waende zao angaa wamuondolee gharama.

Kuvunjika kwa mwiko siyo mwisho mapishi, Njeri ambaye ni mzaliwa wa Gatundu Kusini, kaunti ya Kiambu, anasema mapenzi na ari yake ilikuwa kujihusisha na ufugaji, hasa ndege wa nyumbani.

Mnamo 2016, aliwekeza katika ufugaji wa kuku. Aidha, alikuwa na makazi (kizimba cha kuku), na ilimgharimu Sh7,000 pekee, ambapo alinunua jimbi wawili – kuku wa kiume mmoja kwa Sh1,500. Pia alinunua kuku wanne wa kike, mtetea, mmoja akiuziwa Sh1, 000.

Kozi aliyosomea mfugaji huyu, IT, aliitumia kufanya utafiti wa jinsi ya kuimarisha ufugaji wa kuku.

“Mitandao imenisaidia kustawisha jitihada zangu katika kufuga kuku,” anasema Njeri.

Zachary Munyambu kutoka Kiambu Poultry Society, chama cha ushirika kinachowaleta pamoja baadhi ya wafugaji wa kuku Kiambu, anasema haja ipo kwa mfugaji chipukizi kupata mafunzo. Mdau huyu anaeleza kwamba kinachofelisha wakulima wengi, hususan katika sekta ya ufugaji ni kukosa maarifa ya kutunza kuku.

“Mkulima asiingilie biashara asiyoelewa. Ni muhimu apate mafunzo ya namna ya kupokea kuku, kujua kuwatunza, lishe bora na kamilifu na matibabu,” Bw Munyambu afafanua.

Mfugaji Njeri anasema utafiti kupitia mitandao na kutembelea wafugaji waliofanikiwa ulimuwezesha kujihami sambamba.

“Safari haijakuwa rahisi kwa sababu changamoto hasa za chakula duni na magonjwa hazikosi. Utafiti umenipiga jeki kimaarifa na kuninoa,” anasema.

Baadhi ya kampuni za kuunda mlo wa mifugo zinalaumiwa kwa kutengeneza chakula cha hadhi ya chini – kisichoafikia vigezo vya madini faafu. Hata hivyo, Zachary Munyambu anapendekeza haja ya mkulima kujiundia chakula chake, chenye uhakika wa uhalisia wa madini.

“Hayo yote yatawezeshwa wafugaji wakiungana kupitia vyama vya ushirika wajitengezee lishe,” anashauri, akiongeza kusema kwamba vyama vya ushirika pia husaidia pakubwa katika kutafuta soko la mazao.

Uamuzi wa kufuga kuku, Regina Njeri anautaja kama wa busara kwani mradi wake umepanuka kiasi cha kusitiri takriban kuku 1, 000, idadi hii ikijumuisha kuku waliokomaa na vifaranga.

Mfugaji huyu anasema hatua ya kuongeza mazao thamani; kuangua mayai kuwa vifaranga imemsaidia kuepuka kero la bei duni ya mayai. Kifaranga wa siku moja huuza Sh100, bei ikipanda kulingana na umri.

Pia, huuza mayai kreti moja ikigharimu zaidi ya Sh500.

“Mayai ya kienyeji ni bei ghali. Ingawa kuwepo kwa mayai kutoka mataifa ya kigeni yamechangia kudorora kwa soko, ndio maana yangu huyaongeza thamani kuangua vifaranga,” anaeleza.

Kuku haswa wa kike wanapofikisha umri wa miaka miwili na nusu, hushusha ari kutaga mayai.

Njeri huwauza kuwa wa nyama, ambapo mmoja hapungui Sh700.

Katika shamrashamra za Krismasi, mwezi Desemba, bei hupanda hadi zaidi ya Sh1,000.