Makala

AKILIMALI: Anatumia teknolojia kuwalisha na pia kuwanywesha ng'ombe wake

November 21st, 2019 3 min read

Na PHYLLIS MUSASIA

KAMA wasemavyo wahenga akili ni nywele, basi Benard Kemei wa eneo la Sotik Kaunti ya Bomet, ana zake.

Kwa muda wa miaka 10 Bw Kemei amekuwa mfugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Tofauti yake na wafugaji wengine ni kwamba ameifanya kazi hiyo akiwa peke yake bila usaidizi wa wafanyakazi ila kwa uwezo wa mashine ya teknolojia mpya.

Wakati wa mazungumzo nyumbani kwake, Bw Kemei alieleza kuwa hali ngumu ya maisha ilichangia yeye kutumia akili zake za kuzaliwa na kuvumbua mashine inayotumia teknolojia ili kusaidia kurahisisha kazi ya kuwalisha ng’ombe wake na kuwapa maji.

“Niliwahi kuajiri wafanyikazi wawili lakini kufuatia hali ngumu ya uchumi, nilipata ugumu wa kuwalipa ipasavyo,” akaeleza Aliongeza kuwa teknolojia imesaidia kupunguzua gharama ya kazi yake kwa asilimia 50.

“Kazi ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa si kazi rahisi haswa ukiwa peke yako. Mara nyingi wakulima hutafuta wafanyikazi wa kuwasaidia shambani, zizini na kwenye shughuli ndogo ndogo wakati wa malisho na kusafisha zizi la ng’ombe,” akasema Bw Kemei.

Mnamo mwaka wa 2010, Bw Kemei alieleza kuwa alianza kwa kufuga ng’ombe mmoja wa kawaida lakini baadaye akabadili nia na kununua ng’ombe ambao wangempa maziwa kwa wingi.

“Jinsi mambo yalibadili ndivyo kazi iliongezeka. Nakumbuka vyema sikuwa na kazi nyingine ambayo ingenisaidia kupata mapato ya kumlipa mfanyikazi,” kasema Kemei.Aliamua kununua mashine ya kusaga chakula cha ng’ombe wake kama vile mabua za mahindi, nyasi aina ya ‘nappier’, mtama, ‘desmodium’ na Kamba za viazi vitamu.

Mashine hiyo ambayo inauwezo wa kusiaga hadi tani tano ya chakula hicho cha mwezi mmoja, inatumia gesi inayotokana kwa kinyesi cha mifugo hao kilichochanganywa na mkojo alimaarufu ‘biogas’, badala ya petrol.

“Bei ya petrol ni ghali mno na ikiwa mkulima anategemea petrol ili kuendesha shughuli kama hii, kuna hasara kubwa sana ambayo yeye hukadiria kila siku,” akaeleza Bw Kemei ambaye ameunganisha mabomba na nyaya za kusambaza gesi hiyo kutoka kwenye tangi moja chini ya ardhi.

“Kinyesi chote na mkojo wa mifugo wangu wakiwemo ng’ombe kondoo na mbuzi hukusanywa kutoka zizini na kisha kuongezwa maji kiasi na kukorogwa vizuri. Gesi inayotokana nayo ndio mimi hutumia kufanyia kazi kwenye mashine ya kusaga chakula cha mifugo hawa,” akaeleza kwa kina.

Aidha, Bw Kemei alisema kando na teknolojia mpya kumrahisishia kazi, imewezesha pia mifugo wake kuongeza lita za maziwa kutoka lita 7 kwa siku hadi 25 kutoka kwa kila ng’ombe.

“Ninapata wakati wa kutosha wa kuwalisha ng’ombe wangu kwani sikumii nguvu nyingi kama vile kusaga vyakula kwa kutumia panga. Nina ufahamu wa masaa hitajika ambayo kila ng’ombe anapaswa kupata iana ya chakula kinachohitajika,” akasema kwa tabasamu.

Ili kusaidia mashine hiyo kudumu kwa muda mrefu, Bw Kemei alisema anahakikisha kuwa anaondoa mabaki yote ya chakula cha ng’ombe baada ya kusaga ili kuwezesha makali yake kubaki kuwa imara.

Mashine hiyo pia inahifadhiwa chini ya chumba kilichofunikwa juu ili kuzuia jua kali na maji ya mvua ambayo inaweza kusababisha kutu.

“Nimehakikisha pia mashine hii haiguzi sakafu na badala yake inaningini’a kutoka upande wa juu huku ikiwa imezuiliwa upande wa nyuma kwa nati nzito,” akaeleza.

Mabomba ya maji

Kwenye sehemu ya juu ya malisho, kunalo tangi moja kubwa la maji ambalo lina mabomba yanayoelekeza maji hadi kwenye sehemu ya mifugo ya kunywa maji hayo.

“Maji haya pia yanasafirishwa kwa nguvu za gesi hii. Mabomba niliwekwa yanauwezo wa kuongeza kiwango cha maji pindi tu yanapopungua kwenye besheni hizi. Hayahitaji mtu kushughulika kufanya kazi hiyo,” akasema Bw Kemei.

Na hata wakati wa kiangazi Bw Kemei alisema huhakikisha kuwa kuna maji ya kutosha kwa mifugo wote.Kwenye shamba lake la mifugo, Kemei amerahisisha kila kazi na kuhakikisha kuwa mifugo wake wanapata chakula cha kutosha, maji, zizi linasafishwa bila ya msaidizi wowote ila kwa uwezo wa mashine na matumizi ya gesi ya ‘biogas’ aliovumbua mwenyewe.Nyumbani kwake kumegeuka kuwa sehemu ya wakulima wengine kupata mafunzo ili kuiga mfamo wake wa kufanya kazi.

“Kila siku sikosi kuwapokea zaidi ya watu wanne hadi sita ambao huitaji mawaidha kutoka kwa kilimo hiki. Natumai maisha yao yatabadilika,” akasema.

Maono yake Kemei ni kuongeza idadi ya ng’ombe wa maziwa utoka tano hadi ishirini kufikia mwishoni mwa mwaka ujao.Kulingana naye, faida anayopata kupitia kwa uuzaji wa maziwa imemwezesha kuwasomesha wanawe watatu hadi vyuo vikuu na pia kununua shamba ekari sita.

“Sina nia ya kuiwacha kazi hii hata siku moja,” akaeleza kwa ujasiri