AKILIMALI: Avuna hela kutokana na ufugaji sungura na njiwa jijini Nairobi

AKILIMALI: Avuna hela kutokana na ufugaji sungura na njiwa jijini Nairobi

Na WINNIE ONYANDO

SUNGURA kando na kutumika kama chakula miongoni mwa baadhi ya watu, mnyama huyo huwa kivutio hasa miongoni mwa watoto.

Andai Ondele, 40, ni mfugaji mashuhuri wa sungura na njiwa katika eneo la Mlango Kubwa jijini Nairobi.

Biashara aliyoianzisha miaka 20 iliyopita imekuwa kitega uchumi kwake na kuwakimu pamoja na familia yake.

Alipotembelewa na Akilimali, Ondele alieleza kuwa alipata uraibu wa kuwafuga sungura na njiwa tangu akiwa mdogo.

“Baba yangu alikuwa mfugaji hodari na nilikuwa nikimsaidia kuwalisha sungura wake. Hapo nikaanza kupata uraibu wa kuwafuga wanyama hao,” alieleza Ondele.

Japo alikosa kupata ajira baada ya kusomea kozi inayoshughulika na nguvu za umeme katika Chuo Kikuu cha Nairobi, anaeleza kuwa ufugaji wa sungura umempa mwelekeo mpya maishani.

Tangu aanzishe biashara yake, baba wa watoto watano anasema kuwa hajawahi kujuta.

Katika eneo hilo, wateja wake sio tu watoto pekee bali pia wanaofahamu utamu wa nyama wa mnyama huyo.

Kwa siku, anaweza kuwauza sungura zaidi ya kumi huku kila mmoja akimpa faida ya Sh1,000.

Pesa hizo anazitumia kuwalipia karo watoto wake wawili ambao wako katika shule za upili humu jijini.

Sungura huhitaji mazingira safi. Anaeleza kuwa kila mara, yeye husafisha nyumba yao mara tatu kwa siku ili kuhakikisha kuwa wanakaa katika mazingira safi.

Sungura huchukua muda wa miezi sita kukomaa.

Ondele ana sungura zaidi ya 30. Hivyo yeye huwauza hata wale wadogo ambao hawajakomaa.

“Kuna wazazi ambao huwanunulia watoto wao sungura ambao hawajakomaa. Mdogo kama huyo mimi huuza Sh1,500,” Ondele aliambia Akilimali.

Yeye huwalisha sungura wake kwa kutumia lishe kutoka madukani, lakini pia majani ya mimea fulani na nyasi, na huwalisha mara mbili kwa siku. Pia, huhakikisha kuwa wao hupewa maji safi ya kunywa.

Mkulima huyo, anayefuga sungura kama vile: Californian White, Chinchilla, Dutch, Havana, na Flemish Giant, anadokeza kuwa, ni watu wachache ambao hushughulika na ufugaji wa sungura katika eneo hilo.

Ili kuzuia uzalishanaji kati ya sungura wa uzao mmoja, mkulima huyo huwachukua sungura wa kiume kutoka sehemu tofauti, ili kuwatumia kuwatungisha mimba wale wa kike.

Changamoto

Mojawapo ya changamoto ambazo amewahi kuzipitia ni kufa ghafla kwa baadhi ya sungura wake.

“Baadhi ya sungura hawaonyeshi dalili za kuugua, utawapata tu wakiwa wamekufa,” asema Ondele.

Vyakula vya sungura huwa ghali. Hii humgharimu sana. Anaeleza kuwa anaweza kutumia zaidi ya Sh5,000 kuwanunulia chakula sungura wake.

Andai Ondele akionyesha baadhi ya sungura ambao anawauza eneo la Mlango Kubwa, Nairobi. Picha/ Winnie Onyando

Anaeleza kuwa si kila mmoja anajua utamu wa nyama ya sungura. Wengi wananunua kama pambo ya nyumba au kuwafurahisha watoto wao. Hii inamfanya kuwauza sungura wachache.

“Wanaofahamu utamu wa mnyama huyu ni wachache. Wengine hutumia nyama yake kama tiba kulingana na Imani yake,” alieleza Ondele.

Anasema kuwa, sungura wana magonjwa kadha wa kadha, japo mengi huweza kuzuia kwa urahisi, kwa kujenga vibanda vilivyo bora.

“Ugonjwa unaowaathiri sungura mara kwa mara ni ule unaowafanya kuhara,” asema, akiongeza kuwa, yeye huuzuia ugonjwa huo kwa kuwapa lishe isiyokuwa na unyevu.

Ondele anawahimiza vijana kujitosa katika biashara ili kujiinua kiuchumi.

You can share this post!

Mfumo wa kuinua uchumi bottom-up umetajwa kwenye Biblia –...

Haji aamuru polisi sita washtakiwe kwa mauaji ya ndugu...