Makala

AKILIMALI: Baada ya mwezi mmoja, mmea huu utakuletea faida

November 1st, 2018 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

SIMON Njenga ni mkulima wa saladi katika kijiji cha Chura, eneo la Kabete, Kaunti ya Kiambu. Yeye amekuwa akihusika na kilimo hiki kwa miaka minne sasa na anasimulia ya kwamba ni kilimo chenye faida kubwa kwa mkulima mwenye bidii.

Njenga mwenye umri wa miaka 38 na baba ya watoto wawili anasema kilimo hiki ndicho kitega uchumi kwake na huwa anakuza saladi hizi katika sehemu ya shamba lake lenye ukubwa wa nusu ekari.

Sehemu hii ya shamba ina uwezo wa kubeba kati ya saladi 3,000 na 3,500 kwa wakati mmoja wa msimu wa upanzi.

Kwa kawaida Bw Njenga huwa anapanda mmea huu katika sehemu moja ya shamba na kisha kupanda miche hiyo katika sehemu nyingine za shamba baada ya kipindi cha mwezi mmoja.

Baada ya hayo saladi almaarufu ‘Lettuce’ hukua kwa mwezi mmoja na nusu na kuwa tayari kuanza kuvunwa.

Katika muda huu wote, saladi huwa zinanyunyiziwa maji kila siku ili kuhakikisha kwamba zinakua haraka na zinastawishwa kwa afya bora.

Pia wakati huu, huwa anatumia dawa za kuua wadudu hatari ambao huwa wanakula majani ya saladi. Kwa muda huu, pia huwa anashughulika na upalizi wa mimea hii mara tatu huku akiyatoa majani yasiyohitajika kwenye shamba.

Kulingana naye, saladi huwa inafanya vizuri zaidi anapotumia mbolea ya kiasili badala ya zile za kununuliwa madukani.

Bw Njenga anapoanza kuvuna, huwa inachukua muda wa hadi wiki mbili ama tatu kufanya shughuli hii. Wakati huu, yeye huwa amewajulisha wateja wake kuyajia mavuno ya saladi shambani na baadaye kuuza katika soko za City Park, Nairobi na Wangige, Kaunti ya Kiambu.

“Huwa ninauza saladi moja kwa Sh50 na kwa msimu mzuri wa miezi mitatu, nina uwezo wa kuuza kati ya saladi 3,200 na 3,700,” anaelezea Bw Njenga.

Ombi lake kwa serikali ya kitaifa na ya Kaunti ya Kiambu ni kuwatafutia wakulima wa saladi masoko mengi ya humu nchini na hata ya nje.

Hili, anasema litasaidia kuwatia motisha zaidi na wakulima waweze kukuza saladi kwa wingi.

“La mno ni wakulima waelimishwe kuhusu masuala ya teknolojia mpya za kukuza na kutunza saladi,” Njenga anasema.

Anasema ya kuwa wakulima wengi hawajaweza kuwekeza katika kilimo hiki kwa wingi kwa hivyo mazao ambayo yanapatikana hayatoshelezi mahitaji ya masoko.

Sababu ya kutowekeza, Bw Njenga anaeleza kuwa, ni ukosefu wa ufahamu miongoni mwa wakazi wengi kuhusiana na kilimo hiki.

Baadhi ya changamoto ambazo huwa anakabiliana nazo ni pamoja na uhaba wa maji wakati wa kiangazi. Wakati huu anasema ni haswa mwezi wa Februari na Machi. Changamoto nyingine ni wingi wa wadudu ambao huwa wanaathiri mmea huu.

Pia katika msimu wa baridi, hasa mwezi wa saba, mmea huu huathiriwa pakubwa na mabadiliko ya hali ya hewa.