Makala

AKILIMALI: Badala ya kuajiriwa alikuja mjini kukuza mimea na kufuga samaki

August 15th, 2019 3 min read

Na PETER CHANGTOEK

BAADA ya kukamilisha masomo yake ya stashahada ya Utalii, alikataa katakata kuajiriwa na badala yake, akaufuata mkondo alioelekezwa na moyo wake.

Alianza kufanya shughuli za ufugaji wa samaki na kuku pamoja na ukuzaji wa mimea kwa kutumia kivungulio (greenhouse).

Sarah Wambui, 31 pia aliwahi kuwafuga sungura, lakini gharama ya ufugaji wa sungura ilipopanda na kuushinda uwezo wake, aliamua liwe liwalo, akaasi shughuli hiyo, licha ya kuwa kwa wakati mmoja aliwahi kuwa na sungura takriban 300.

Katika ploti yenye kipimo cha futi 22 kwa 75, Wambui amedhihirisha dhahiri shahiri kuwa ili mja awe mkulima, si lazima awe na shamba kubwa, bali hata kipande kidogo ni muhimu kwa uendeshaji wa zaraa.

Ushupavu wake katika kilimo anachokiendeleza ulimwezesha kudhaminiwa na mashirika kadhaa kuenda kuwawakilisha vijana wa Kenya nchini Canada.

Wambui, ambaye ni kitindamimba katika aila ya watoto sita, anauendeleza ukulima huo katika mtaa wa Donholm, viungani mwa jiji la Nairobi.

Mtu aingiapo katika ploti yao, kinachokutana na macho yake ni dude aina ya aquaponics, ambalo hutumiwa katika ufugaji wa samaki aina ya kambare.

“Maji huzunguka kutoka hapa na kuingia katika matangi haya yenye samaki, na kutoka hapo, huingia katika tangi la kuyasafisha. Kutoka hapo, huingia katika sehemu hii ambako mimea hukuzwa. Maji huchujwa katika sehemu iliyo na mimea, na kurejeshwa katika matangi haya yenye samaki yakiwa safi,’’ afafanua kinagaubaga kuhusu mchakato mzima wa kuzungushwa kwa maji katika dude hilo lenye samaki.

Lakini alianzia wapi na lini? Mnamo mwaka 2008, Wambui, pamoja na mamaye, Evelyn Wamuyu, walikopa mikopo kutoka kwa mashirika mawili ya kutoa mikopo ya fedha.

Mama yake alipewa mkopo wa Sh150,000 kutoka kwa Hazina ya Biashara kwa Wanawake, Kenya (Kenya Women Enterprise Fund), naye Wambui akapewa mkopo wa Sh100,000 kutoka kwa Hazina ya Vijana (Youth Enterprise Development Fund).

Walizitumia fedha hizo kuiasisi zaraa ya ufugaji samaki na kuku.

“Mara ya mwisho tukiwahesabu samaki hao walikuwa 150 na 130 katika matangi hayo mawili,’’ afichua Wambui, akiongeza kwamba humwuza samaki mwenye uzani wa kilo moja kwa Sh500.

Hata hivyo, samaki mwenye uzito uo huo, huuzwa kwa bei ya juu zaidi, endapo atauzwa akiwa amekaangwa.

“Wateja wangu ni majirani, marafiki, na watu katika mitandao ya kijamii,’’ afichua, akiongeza kuwa yeye huwalisha samaki wake akitumia lishe zenye protini nyingi.

Kwa mujibu wa mkulima na mfugaji huyo, samaki awafugao hawajawahi kuathiriwa na maradhi yoyote.

Mkulima huyo, ambaye ni mzazi wa mtoto mmoja, anasema kuwa yeye hudumisha usafi katika mazingira anayotumia kwa ufagaji.

Ili kuvikabili visa ambapo samaki wakubwa huweza kuwahangaisha na kuwala wadogo, yeye huwatenganisha kwa kuzingatia ukubwa. Yaani, wale wakubwa hufugwa pamoja katika sehemu yao, na wadogo hufugwa katika sehemu tofauti.

Mbali na ufugaji wa samaki, yeye pia hushughulikia ufugaji wa kuku.

“Kwa sasa, nina kuku takriban mia moja (100),’’ asema mkulima huyo, ambaye ana stashahada ya Utalii kutoka kwa taasisi ya Railways Training Institute (RTI).

Kutoka kwa kuku hao, yeye huyapata mayai zaidi ya thelathini kwa siku, ambapo huyauza mengine, huku mengine yakianguliwa kuwa vifaranga.

Mbali na kuwa mfugaji wa samaki na kuku, yeye hutoa mafunzo kwa wakulima kwa ada ya Sh1,500. Kwa wale ambao hutalii kule anakofanyia shughuli za kilimo, hutozwa ada ya Sh1,000.

Anafichua kuwa wageni wake hutoka mumu humu nchini, ilhali wengine hutoka ughaibuni; Amerika, Canada, India, Dubai, Sierra Leone na Tanzania; na kitabu ambacho hutiwa saini na wageni hao kinathibitisha hayo.

Kongamano

Mnamo mwaka wa 2013, mkulima huyu alikuwa mwenye bahati ya mtende alipoupata ufadhili kuzuru nchini Canada kwa madhumuni ya kulihudhuria kongamano la zaraa.

“Nilienda kule kuwawakilisha vijana wa Kenya. Nilifadhiliwa na mashirika ya Rooftops Canada na OCIC Global Citizens Forum. Nilijifunza mengi,’’ asema Wambui, ambaye ana cheti cha masomo ya utunzaji mimea kutoka kwa Chuo Kikuu cha Nairobi, Bewa la Upper Kabete.

Mmojawapo wa mikakati aitumiayo kuuza ni utumiaji wa Facebook (Smart Urban Farm Technologies).

Kwa sasa, hana wafanyakazi, maadamu husaidiwa na mamaye, ambaye ni mhasibu ambaye amestaafu.

Kwa mwezi mmoja, anafichua, huweza kutia kibindoni Sh100,000, pesa taslimu kutoka kwa shughuli zake zote za zaraa