Makala

AKILIMALI: Bayogesi inavyopunguzia wakulima gharama

July 25th, 2020 3 min read

NA RICHARD MAOSI

Wakulima wengi mashinani wameanzisha mikakati ya kupunguza gharama ya kulipia kawi ya umeme na mafuta, wakati huu ambapo taifa linaendelea kukabiliana na janga la Covid-19.

Aidha wengine wamegeukia mbinu mbadala za kulisha mifugo wao kama vile ng’ombe, mbuzi na kondoo badala ya kutegemea vyakula vinavyoundwa viwandani.

Huu ukiwa ni mfumo wa kupunguza gharama ya maisha na kuendeleza nyenzo za kujikimu, bila kupoteza nafasi za ajira wala kuyaharibu mazingira.

“Janga la Covid-19 limekuja na hasara nyingi kuliko faida, lakini hali hii imetengeneza fursa kwa wajasiria mali kujiongezea kipato na hatimaye kupigana na umaskini,” anasema Moses Gathua.

Yeye ni mkaazi wa eneo la Lanet viungani mwa mji wa Nakuru ambapo anafanya kazi ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na ukuzaji wa mimea ya aina mbalimbali kama vile sukumawiki na nyanya.

Anasema bayogesi imekuwa ikimsaidia kupunguza matumizi ya hela zinazotumika kulipia umeme kila mwisho wa mwezi. RICHARD MAOSI

Mradi wa kuzalisha Bayogesi

Alianzisha mradi wa kuzalisha bayogesi na kutengeneza silage , ili kuzalisha nguvu kazi(kawi) na kuimarisha upatikanaji wa malisho kwa mifugo.

Hata hivyo Moses amejianzishia mradi wa kuzalisha bayogesi kutokana na samadi ili kupunguza gharama ya kulipa umeme wakati huu wa Covid-19.Pia amefanikiwa kuondokana na gharama kubwa ya kununua makaa, kuni na gesi ya mitungi inayotumika kupikia.

Anatumia kawi ya bayogesi , hali ambayo anaona imempunguzia matumizi ya hela nyumbani, ikizingatiwa kuwa , katika hali ya kawaida anaweza kuhifadhi zaidi ya 3000 kila mwezi kulipia stima.

Kulingana na Moses bayogesi hutengenezwa na aina mbalimbali ya vimelea pasipokuwa na uwepo wa oksijeni.

Moses anasema kuwa kawi ya bayogesi ni nafuu, ikilinganishwa na aina nyingine ya umeme kama vile kutumia mafuta taa.

Isitoshe bayogesi hutoa nishati safi ambayo haiwezi kusababisha mchafuko wa mazingira kwani haitoi aina yoyote ya mvuke wala moshi.

Anasema kuwa nyasi za aina yoyote zinaweza kukatwa kwa mtambo wa chaffcuter na kuchanganywa na molasses, kisha zikahifadhiwa katika shimo zikisubiri kutumiwa msimu ambao malisho ni haba. Picha/Richard Maosi

Alieleza Akilimali kuwa bayogesi inaweza kutumika mashinani ambapo wakazi wengi ni wafugaji wa ng’ombe na stima hazijafika, hii ni kwa sababu jamii nyingi za wafugaji zina uhakika wa upatikanaji wa samadi.

Anasema samadi ya ng’ombe hatimaye humenywa na bakteria na kupunguza viungo vya samadi kuwa vipande vidogo vidogo ambavyo hatimaye huweza kutoa gesi ya methane ambayo ndiyo hasa huwaka.

Akitumia mtindo wa kisasa ameunganisha paipu zinazoelekea chumbani kutoka kwenye mfumo wa kuzalisha nishati ambao ni mchanganyiko wa samadi na maji.

Kwa kuchimbia shimo lenye kina cha futi tatu hivi, Moses amejaza samadi kutoka kwa mifugo wake watatu na kufunika kwa tandarua .

“Mtu anapotumia gesi inayotokana na bayogesi itamlazimu kujaza samadi na maji na haitahitajika kulipa pesa za umeme kila mwezi,” akasema.

Kulingana na Moses sehemu ya kwanza huwa ni ile na kuchanganya samadi na maji ili kutoa nafasi kwa bakteria kuchakachua mchanganyiko huo.

Pili atafute mkondo maalum wa kusafirisha gesi hadi chumbani mara tu baada ya kuzalishwa hadi mekoni ambapo inaweza kutumika.

Sehemu yake ya kuzalisha gesi huwa imefunikiwa ardhini na kuwekewa misingi kwa matofali ya kutosha yalichanganywa na saruji ili maji ya mvua yasije yakasomba mchanganyiko huo wa samadi.

Kutengeneza lishe

Silage ni aina ya lishe inayotengenezwa na aina yeyote ya malisho yanayofaa kutumika na mifugo hususan majani au mabaki ya mahindi.

Kulingana na Moses Ili mkulima kutengeneza kiwango sahihi cha silage ni sharti atafute aina ya majani anayolenga kutumia kama vile matawi ya mahindi au nyasi.

Mchanganyiko huu uhifadhiwe katika shimo ili kutoa nafasi ya kukauka vyema, wakati mwingine mkulima anaweza kuhifadhi ndani ya silo na kuhifadhi akitumia aina maalum ya kemikali.

“Hatimaye mkulima anaweza akachanganya na Molasses ili kulisha mifugo wake hasa msimu wa kiangazi wakati ambapo malisho ni ghali,” alieleza.

Silage ni lishe muhimu kwa sababu ina virutubishi vyote kama vile protini, vitamin na madini yanayoweza kuongeza kiwango cha maziwa yanayozalishwa.

Anasema Silage inastahili kuwa na unyevu wa kiwango cha asilimia 70, aidha ni lazima iwe na kiwango kikubwa cha sukari.

Ili kuhifadhi silage ni vyema kuchimba shimo la kina cha mita mbili, na kupondaponda mchanganyiko wa majani hadi yawe laini.

Baada ya siku tatu mchanganyiko inaweza kuwa tayari kwa ajili ya matumizi ya mifugo shambani.