Makala

AKILIMALI: Bei duni yawasukuma wakulima wa kahawa Machakos kukumbatia mimea mingine

January 3rd, 2019 3 min read

Na CHARLES WASONGA

MWAKA uliopita wa 2018, wakulima wa zao la kahawa janibu za Ukambani walikabiliwa na changamoto na masaibu chungu nzima, nusra wakate tamaa na kutundika chini zana zao za ukulima kwa kukosa matumaini.

Hali ilikuwa mbaya kiasi kwamba baadhi yao waliamua kung’oa mikahawa yao na  kukumbatia kilimo mbadala cha mboga na matunda ili waweze angalau kukidhi mahitaji yao ya kimsingi, kando na kugharamia karo za watoto wao.

Kwa mfano, kati ya mwaka wa 2015 na 2016 bei ya kilo moja ya kahawa ilikuwa Sh75 kwa kilo. Lakini kuanzia mwanzoni mwa jana (2017) bei hiyo ilishuka hadi Sh28 kwa kilo moja ya kahawa ghafi. Hii ina maana kuwa mkulima ambaye aliwasilisha kilo 10,000 ya kahawa kiwandani kwa mwaka angetia kibindoni takriban Sh750,000, kabla ya kuondoa gharama za uzalishaji.

Lakini sasa kiasi hicho cha mapato kimepungua hadi kufikia Sh280,000 ambapo baada ya kutoa gharama za pembejeo za kilimo na ujira wa vibarua, mapato hayo yatasalia finyu mno.

Mkulima David Kathya akiwa katika shamba lake la parachichi katika kijiji cha Kisooni, Kathiani, kaunti ya Machakos. Sasa anachuma mapato ya juu baada ya kuipa kisogo kiliimo cha Kahawa. Picha/ Charles Wasonga

Hii ni maana wakulima wengi wa zao hilo waliamua kupanua mawanda yao kwa kuanza kukuza mimea mbadala kama vile mboga, matunda, makadamia na mengineyo yenye mapato mazuri na ya haraka.

Mmoja wakulima hao, Mama Hellena Muteti, ambaye aling’oa mikahawa katika sehemu ya shamba lake na kupanda mimea ya makadamia. Na hajutii hatua hiyo kwani mapato yake yameimarika mara dufu.

“Kilimo cha kahawa kilipoanza kudorora kutokana na bei yake katika masoko ya kimataifa kuanza kuyumbayumba na kukosa msimamo thabiti, niliingilia kilimo cha makadamia na nimeanza kuchuma mapato mazuri’’, asema mkulima huyu ambaye ni mkazi wa kitongoji cha Muuini, kata ya Iveti, kaunti ndogo ya Kathiani, kaunti ya Machakos.

Mama huyu azidi kuarifu ya kwamba, kilimo cha kahawa kilimpatia hasara mwaka jana wa 2018, licha ya kuwekeza maelfu ya pesa katika kilimo hicho. Hata hivyo, kilimo cha makadamia kimemletea afueni maishani mwake.

Mkulima Julius Ndugu ambaye ni mkazi wa kata ya Iveti, Machakos akiwa na mkewe wakionyesha hawana waliovuna kutoka sehemu ndogo ya shamba lao  Picha/ Charles Wasonga

“Sasa tunauza makadamia kwa bei ya Sh150 kwa kilo ilhali kahawa ilikuwa ikinipa Sh28 pekee kwa kilo. Shamba langu la ekari mbili limeweza kunipa zaidi ya Sh900,000 kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita,” akasema Muteti.

Mkulima mwingine, Musyoki David asema kwamba, alipoanza kilimo cha mboga na matunda baada ya kuipa kisogo kilimo cha kahawa, watu wengi wakimpuuza wakidai eti alikuwa amepoteza dira ya kimaisha mwaka huo, na kumbe sivyo!

“Kinyume na matarajio ya wengi, miaka michache iliyopita nilikumbatia fani ya kilimo cha mboga na matunda aina ya maparachichi na nikafanikiwa zaidi ya nyakati ambapo nilitegemea zao la kahawa pekee. Sasa mimi hutia kibindoni angalau Sh50,000 kwa mwezi, pesa ambazo singeweza kupata kutoka na mauzo ya kahawa,” akasema.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kiwanda cha kusaga kahawa cha Mukuyuni Farmer Cooperative Society, Stephen Muia Wambua asema kwamba, alipoona bei ya kahawa ikielekea kudorora alikata kauli kuanzisha miradi kadha kiwandani humo ili kuwainua wanachama wake kimapato huku wakitaraji kuwa bei ya zao hilo ingeimarika siku za usoni.

Wakulima waonyesha zao la makadamia. picha/ Charles Wasonga

“Tulianzisha miradi ya ufugaji nyuki na kuku wa kienyeji huku tukiambatanisha na kilimo cha mboga ili kujichumia mapato ya ziada kiwandani hapa, ’’ asema mwenyekiti huyo.

Si hayo tu, mwenyekiti huyu asema kwamba, amejaribu juu na chini ili kuhakikisha ya kwamba wakulima walio wanachama wa kiwanda hicho wanazidi kuboresha zao la kahawa kwa matumaini makubwa kuwa bei yake itanyooka na kuimarika maradufu katika soko la kimataifa.

“Nawashauri wakulima wa kahawa watunze mmea huu kwa kunyunyizia madawa na kutia rotuba na samadi itakikanavyo maana bei yake inaelekea kuimarika mno msimu huu’’, akashauri mwenyekiti huyu.

Lakini kulingana na mwenyekiti wa kiwanda cha kahawa kinachomilikiwa na Chama cha Ushirika cha Kaliluni Farmer’s Cooperative Society, Bw Edwin Mulomba, kilimo cha kahawa kilisambaratika katika maeneo ya Ukambani kutokana na ufisadi mwingi uliokolea katika kamati husika na kuwafanya wakulima wapoteza mamilioni ya pesa.

Bw Edwin Mulomba, ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Wakulima wa Kahawa wa Kaliluni (Kaliluni Farmers Cooperative Society). Anasema kilimo cha kahawa kimevurugwa na visa vya upunjaji wa wakulima wa zao hilo. Picha/ Charles Wasonga

“Wanakamati wengi wa viwanda vya kahawa janibu za Ukambani walikuwa wamekolewa na hulka mbaya ya ufisadi ambayo iliporomosha kilimo hiki na kuwafanya wakulima wengi wakose matumaini katika zaraa hii ashirafu.’’ asema Bw Mulomba.

Bw Mulomba asema ya kwamba, laiti wanakamati wangekuwa waaminifu na kuheshimu kabisa jasho la wakulima, bila shaka kilimo cha kahawa kingekuwa kinazidi kuwavutia watu wengi, na hasa pia wasomi wa kila tabaka.

Hata hivyo, Bw Mulomba anaamini kwa dhati ya moyo wake kuwa bei ya kahawa itaimarika maradufu mwaka huu wa 2019. Kwa minajili hii, Mulomba anawasihi wakulima wasife moyo asilani, bali wazidi kupalilia mashamba yao na kufuata kikamilifu mbinu bora za kilimo cha kahawa na kwa hakika, wataona faida yake siku za halafu.

Bw Mulomba ambaye pia ni mkulima mashuhuri wa kahawa vile vile anawashauri wakulima wenza kukumbatia kilimo mseto, lakini wasigure kabisa zaraa hiyo.

“Japo, ni jambo la busara kwa wakulima kukumbatia kilimo cha mimea mingine, nawashauri wasing’oe mikahawa yao kwani bei itaimarika siku zijazo. Lakini wasimamizi wa viwanda vya kahawa pia wanafaa kuwa waaminifu na wakome kuwahadaa wakulima,” akasema.