Makala

AKILIMALI: Biashara ya manati yampa pato nono licha ya kutumia mtaji mdogo

June 11th, 2020 3 min read

Na LUDOVICK MBOGHOLI

JOHN Mati Maithya (42) (almaarufu Kalembe) alitoka Mwingi Kaskazini (Kitui) mwezi Novemba 2019 akaja kukita kambi mtaani Kisimani, Bombolulu (V.O.K) jijini Mombasa kutafuta riziki.

Hata hivyo Kalembe hakutatizika kwani alipokosa ajira alianza ubunifu wa kiufundi ili kumwezesha kukidhi mahitaji yake.

“Nilifikiria sana maana kila ofisi niliyofika kuomba kazi sikuajiriwa” Kalembe adokezea Akilimali kwenye mahojiano.

“Nilijiwa na wazo la kuunda manati (au panda) ambazo huko kwetu hutumiwa kwa kufukuzia tumbiri na nyani mashambani” aarifu Kalembe huku akionekana mwingi wa tabasamu.

Kwa ufafanuzi wake anasema aliwaza wingi wa kunguru waliotapakaa kila mahali jijini Mombasa, ambao wamekuwa chukizo kwa wenyeji.

“Niliona jinsi watu wanavyotaabika kufukuzana na ndege hawa wanaodaiwa kuwa waharibifu, kwa kuwa wenyeji hawapendi kuwaona ndege hawa, ndio nikajiwa na wazo la kuunda manati ili wazitumie kwa kuwatimua mitaani” Kalembe apasha zaidi Akilimali.

Kalembe ni baba wa familia ya watu saba. Ana mke na watoto sita aliowaacha huko kwao Mwingi Kaskazini kaunti ya Kitui, ambao wanamtegemea pakubwa. Miongoni mwa wanawe, wa nne ni wavulana na wawili ni wasichana.

“Wanangu wote wako shuleni isipokuwa msichana mkubwa (kifungua mimba) aliyemaliza darasa la nane, niliyempeleka kwenye chuo kimoja cha Saluni alikojifunzia kazi ya ususi, na sasa anajitegemea” anapasha Akilimali.

Kalembe anaarifu kuwa, mmoja wa wanawe yuko katika darasa la saba mwaka huu, wengine wako katika madarasa ya sita, tano, nne, tatu na Chekechea.

Hata hivyo kabla ya kuanza uundaji wa manati, Kalembe alifikiria atakapopata vijiti vya kuanzia shughuli hiyo.

“Ilibidi nizunguke kila mahali hapa Mombasa nikitafuta miti yenye vijiti vyenye panda, sikufanikiwa ndipo nilipofikiria kuwapigia simu watu wa kwetu huko Mwingi Kaskazini” Maithya asimulia Akilimali.

Anadai miti yenye sampuli hiyo ya vijiti iko mingi huko kwao Mwingi na hivyo alikuwa na uhakika wa kuvipata.

Anasema jamaa zake walimtafutia na kumtumia kwa magunia wakihitaji malipo ambayo alitafuta na kuwatumia.

“Niliwalipa kwa kazi ya kunitafutia panda za kutosha” anadokeza bwana Maithya huku akiarifu alipoletewa alianza moja kwa moja kununua mipira ya chubu za matairi ya baiskeli na magari.

“Nilinunua mipira ya rangi nyekundu maana ina uzito wa kawaida na inapendwa sana huko kwetu Mwingi” anasema Maithya.

Anadai kila mpira (unaotambuliwa kama blada) wenye urefu wa mita moja alinunua kwa Sh100.

“Nilinunua mita moja ya mpira kwa Sh100, ambapo ilibidi nikate kwa vipande viwili kwa ajili ya kuundia manati hizi,” anaarifu Akilimali.

Anadai kila kipande cha mpira anachotengenezea manati hizo humwingizia Sh150 na kunufaika kwa faida ya Sh200.

“Kipande kimoja kinarejesha mtaji ninaotumia na kipande kingine kinanipa faida. Sh100 nnayotumia kwa ununuzi wa mpira mmoja (blada) inaniingizia Sh250 na kunipa pato la Sh150” anasisitiza kwenye mahojiano na Akilimali.

Kwa siku John Mati Maithya anaunda manati 20 ambazo huzichuuzia wateja wanaosinywa na Kunguru kwa Sh200.

“Huwa nachuuza manati hizo na zote huisha, napata pato la Sh4,000 kwa siku” anadokeza Maithya huku akisisitiza kuwa kila mteja anayenunua bidhaa hii ni lazima asafishe mikono kwa kutumia kieuzi alichonacho ili kuepuka maambukizi ya virusi vya corona.

Hata hivyo anaambia Akilimali kuwa lengo lake ni kufikia kuunda manati kati ya 50 na 100 kwa siku.

“Nafikiria ntakavyounda kati ya 50 na 100 kwa siku, lakini kufanikiwa itabidi niajiri kijana wa kunisaidia kazi” Maithya ajuza zaidi Akilimali kwenye mahojiano haya.

Maithya anatumia mtaji wa takriban Sh1,200 kila siku kwa ajili ya ununuzi wa mipira na ngozi za kuundia manati hizo licha ya kutafuta mifuko ya kudumisha shughuli ya uundaji huo, kumaanisha kwa mwezi anatumia mtaji wa takriban Sh36,000

na kwa mwaka anatumia jumla ya Sh432,000

Kwa muktadha huo, Akilimali inabainisha kuwa John Mati Maithya anajiingizia kibindoni jumla ya Sh120,000 kwa mwezi na Sh1,440,000 kwa mwaka licha ya mtaji anaotumia wa Sh432,000

Hata hivyo akiondoa mtaji anaotumia kwa kazi yake, John Mati Maithya anapata faida ya jumla ya Sh1,008,000 kwa mwaka.