Makala

AKILIMALI: Biashara ya vyungu na miche ina hela kama changarawe

June 20th, 2019 3 min read

NA RICHARD MAOSI

Ufinyanzi sawa na uchongaji vinyago kwa kutumia udongo ni sanaa ya kale miongoni mwa jamii nyingi za Afrika. Katika karne ya 21, utawapata watu wachache mno wenye ujuzi huu huku wito ukitolewa kwa vijana wajifundishe kufinyanga.

Kutokana na tajriba ya kufanya ufinyanzi,binadamu anaweza kuhifadhi kumbukumbu za historia yake ,kwa lengo la kuwavutia watalii wanaotembelea mataifa yao.

Wataalamu wanaamini kuwa ufinyanzi sio tu kwa kuhifadhi kumbukumbu za historia bali pia ni nyenzo muhimu wanayotumia wasomi na watafiti kuyaelewa mazingira yao.

Akilimali ilipata fursa ya kuzuru barabara ya Nakuru – Nairobi, kuzungumza na Johnson Kirago, 40, mjasiriamali anayetumia udongo katika shughuli za kila siku kujikimu kimaisha.

ohson akiwa katika biashara yake ya kutengeneza vyungu vya maumbo mbalimbali eneo la Section 58 Nakuru. Picha/ Richard Maosi

Johnson anasema udongo ni kama dhahabu sio tu kwa mkulima, bali pia kwa kizazi cha sasa kinachotegemea teknolojia na ufundi kutengeneza vyombo kwa matumizi ya binadamu.

Kupitia malighafi haya ya asilia anaweza kutengeneza vinyago vya aina na maumbo mbalimbali,kwa kutegemea mahitaji ya wateja wake, wanaomiminika kutoka ndani na nje ya kaunti ya Nakuru.

Anasema miaka ya mbeleni mbao zilikuwa ni tele,ndiposa watu wengi wangeweza kupata bidhaa za kuchonga kwa urahisi.Kinyume na siku hizi ambapo kampeni dhidi ya ukataji miti zimeshamiri.

“Haja ya kuhifadhi mazingira ilinifanya kugeukia mchanga usiovunjika kwa urahisi(clay) kutengeneza bidhaa zangu.Aidha ilinipasa kuwa mbunifu kila ninapokaa ndani ya karakana kuibua na kuunda miundo tofauti,”akasema.

Johnson Kiragu akionyesha baadhi ya bidhaa anazotengeneza kupitia ujuzi wa ufinyanzi. Picha/ Richard Maosi

Kulingana naye ijana wanaohangaika kutafuta ajira wanaweza kuyatumia malighafi yanayopatikana kwenye mazingira yao kujiendeleza kimaisha,kama vile upepo,mvua,mawe na hata jua.

Ili wafanikiwe zaidi watahitajika kukaa karibu na wazee ambao wamekonga ili kujipatia ujuzi huu ambao umebakia mikononi mwa watu wachache tu.

Johnson anaeleza kuwa mbali na kuwa na stadi ya kuchonga vinyago yeyote anayezamia kazi hii lazima awe fundi stadi inapokuja kwenye swala la kupaka rangi.

Rangi ziendane na hali halisia ya maisha, akiamini watu wanapendelea rangi zenye mvuto.Kila umbo linatakiwa kukaushwa ,kupambwa na kuchomwa kwa moto.

Na kwa njia hii ndipo anaweza kupata vyombo vilivyozoeleka kutumika nyumbani kama vile vyungu,mabakuli,vikombe na sahani au wakati mwingine mabirika.

Kando na kutumia udongo kutengeneza bidhaa kama vyungu,Johson Kiragu pia anakuza miche. Picha/ Richard Maosi

Johnson anasema udongo wa mfinyanzi una chembechembe ndogo sana.Uwe ule unaoweza kuyashikilia maji kwa muda mrefu, uwe laini na wa kushikamana vyema,lakini unapokauka uwe mgumu kiasi.

Nyingi ya bidhaa zake hapa ni zile za kupanda maua kwenye bustani au mitungi ya kuhifadhi maji.Ingawa anasema leo hii vyombo vingi vya mfinyanzi hutengenezwa viwandani kwa sababu ya ukosefu wa nguvu kazi.

Mchanga unapatikana kwa wingi katika kaunti ya Nakuru,lakini Johnson alituelezea kuwa sio mchanga wa aina yeyote unaweza kutumika,isipokuwa ule unaokuwa mgumu kila baadaya kuchomwa.

Yeye hupata mchanga kutoka eneo la Menengai crater kwa shilingi 700 kila tani, kisha akausafirisha hadi kwenye karakana lake lililo mkabala na njia kuu ya kuelekea Nairobi eneo linalofahamika kama Section 58.

Akishirikiana na vibarua wake huacha mchanga ukauke kabla ya kutumika,kwani anasema endapo mchanga hautakauka vyema unaweza kufanya umbo kuwa hafifu kwa kutengeneza nyufa.

Kiragu hutumia mbinu hii kuhuchuja mchanga kabla ya kutumia akitumia tairi kuhakikisha ni safi. Picha/ Richard Maosi

Johnson anaona kuwa wanafunzi kati ya umri 8-12 wanaweza kufundishwa stadi ya ufinyanzi na wakaiboresha tajriba yao wanapofikia umri wa miaka 15 hivi wakaboresha ujuzi na kufanya ufinyanzi kama taaluma.

Kulingana naye endapo mjasiria mali atazingatia hatua zote za ufinyanzi,anaweza kujiajiri na kuwaajiri watu wengine,anasema sanaa hii inawza kuinua mtu kimaisha awe mtu wa kujitegemea.

Anapendekeza kozi maalum zinazoshirikisha ujuzi wa mikono, zianzishwe kwenye taasisi za mafunzo ya kiufundi kote nchini ili kukabiliana na ukosefu wa nafasi za ajira kote nchini.

“Jambo la kwanza ambalo mwanafunzi anaweza kufundishwa ni kuchonga umbo linalohitajika, pili asaidiwe kupiga msasa na hatimaye kulainisha kazi yake,” Johnson alisema.

Kulingana naye sio kila mtu anaweza kuwa mchongaji wala mfinyanzi kwa sababu binadamu anatakiwa kufanya juhudi za kutumia ubunifu kwa kuhusisha fikra zake na kukopa ujuzi kutoka kwa watu wengine.

Wanafunzi wa shule za msingi wanaotembelea eneo hili kujifunza umuhimu wa kutunza mazingira. Picha/ Richard Maosi

Anasema inahitaji subira nyingi kabla ya mwanafunzi kuboresha stadi hii ingawa kujifunza hakuna mwisho.Kila siku mawazo tofauti yanakuja kutokana na shindano kali katika soko la uagizaji na uuzaji bidhaa kama hizi.

Anasema kero kubwa ya shughuli hii ni usumbufu wa mchwa endapo mchaongaji hatahifadhi miundo yake kwenye sehemu bora,bila shaka ataambulia hasara kubwa au wakati mwingine akalazimika kuirudia kazi yake.

Wanunuzi wake wengi ni wasafiri wanaotumia barabara ya Nakuru-Nairobi na biashara hii imemwezesha kuanzisha biashara nyingine ya kukuza na kuuza miche,iliyomsaidia kuongeza wanunuzi mara dufu.

Aida watalii wanaozuru mbuga ya wanyama ya Lake Nakuru hufika kwenye karakana yake sio tu kujipatia bidhaa kutokana na ufinyanzi bali pia kujifundisha namna ya kuchonga miundo ya sampuli mbalimbali.