Makala

AKILIMALI: Dereva asifia ufugaji nguruwe akisema unamlipa malaki

December 13th, 2018 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

UFUGAJI wa nguruwe nchini unaendelea kukita mizizi na kufanywa na wakulima kama njia ya kujitafutia riziki. Bi Martha Waithira, mwanadada mwenye umri wa miaka 23 na nduguye Stephen Ng’ang’a wa miaka 34 kutoka eneo la Limuru wamepiga hatua kubwa katika ufugaji wa nguruwe.

Bw Ng’ang’a ambaye pia ni dereva wa malori anasema japo alikuwa anakusudia kufanya kilimo, wazo la kuwafuga nguruwe lilimjia miaka miwili iliyopita. Kulingana naye, alianza kutafuta hela za kununua nguruwe wachanga ili aanze ufugaji rasmi. Kuwepo kwa rafiki yake ambaye anajishughulisha na ufugaji huo katika eneo tofauti mjini Limuru kulimfanya aombe ushauri kabla ya kujitosa katika ufugaji wenyewe.

Maelezo aliyopata kutoka kwa rafikiye huyo yalimchochea aanze ufugaji wenyewe mara moja. Ng’ang’a ambaye alisomea kuwa fundi wa stima katika shule ya kiufundi ya Kabete, aliliwazia zaidi suala la ufugaji huo kisha akazungumza na dada yake mdogo Martha na hapo wakaamua kujituma ili washughulikie ufugaji wa nguruwe.

Walipoanza mwanzoni mwa mwaka huu, walianza na nguruwe watano wachanga. Waliwanunua kati ya Sh2,500 na Sh3,000 kutoka kwa wafugaji wengine tofauti viungani mwa jiji la Nairobi. Baadaye, waliamua kuongezea wengine japo wakubwa ambao kulingana na Waithira, wameshazaana na kuongeza idadi ya nguruwe waliokuwa nao.

“Kwa sasa tuna jumla ya nguruwe 58 maanake nguruwe wakubwa tuliowanunua hawakuchukua muda mrefu kabla ya kuanza kuzaa,” anasema.

Waithira ambaye pia ni mwanamitindo maarufu jijini Nairobi kwa wakati mwingine anasema kwamba nguruwe hujifungua kati ya watoto wanane hadi 12 na kwa sasa nguruwe wakubwa walionao ni 20 na wengine ni wachanga (wengi wakiwa na umri wa miezi miwili na mitatu).

Wawili hawa wameajiri kijakazi ambaye huwa wanasaidiana naye katika kuwatunza nguruwe. Anasema, “kila siku nguruwe hupatiwa chakula katika majira ya asubuhi kati ya saa moja na saa moja unusu hivi na kwa kawaida, hulishwa kwa kati ya kipindi cha saa moja na saa mbili.”

Huwa wanawapa nguruwe chakula na maji kwa kuwawekea kwenye vijisehemu maalum ndani ya kibanda.

Waithira anasema kwamba nguruwe wadogo ambao hawajafikisha umri wa miezi mitatu huchanganyishiwa chakula cha dukani na maji ili waweze kukila kwa urahisi. Kulingana naye, huwa wanauza nguruwe anapofikisha kati ya kilo 60 hadi 80 ambapo wanauza vichinjioni na hatimaye kuuzwa katika maduka ya kuuza nyama ya nguruwe.

Nguruwe mmoja wa uzani huo huuzwa kwa kati ya Sh18,000 na Sh20,000 na kwa kawaida, wao huwa wanauza nguruwe 10 kwa wakati mmoja. Ina maana kwamba pato lao hufikia hadi Sh200,000 kila wanapoamua kuwauza nguruwe wao.

Wamewajengea nguruwe vibanda vizuri vilivyo na mapaa ili kuzuia mvua inaponyesha kwani inaweza kuwa hatari kwa nguruwe kwa sababu ya baridi. Vyumba hivi hunadhifishwa kila siku ili kuzingatia usafi wa hali ya juu ili kuwapa mazingira bora ya kuishi.

Vyumba vinaoshwa mara mbili kwa siku. Mbolea inayotokana na kinyesi cha nguruwe hutumika katika shamba lao la mboga za aina mbalimbali. Anasema kwamba hata kama nguruwe wako katika hatari ya kupata maradhi kama vile kikohozi na numonia, huwa wanaalika madaktari wa mifugo ili kuwakagua na kuwapa chanjo ya kupigana na maradhi hayo ambayo husababishwa na baridi kali.

Nguruwe wanapouzwa pia, daktari huwakagua kabla ya kuchinjwa. Hii ni katika juhudi za kuhakikisha ubora wa afya kwa nguruwe na kwa walaji wa nyama yake.

Waithira anasema faida moja katika ufugaji wao wa nguruwe ni kwamba hawahitaji usimamizi mkubwa maanake wanapopewa chakula na maji ya kutosha, hawahitaji jambo jingine la kufanya kwa dharura. Matarajio yao ni kufuga zaidi ya nguruwe 300 kufikia mwisho wa mwaka ujao; na idadi hiyo inapozidi, wanauza wale ambao wameshakomaa kwa watu binafsi au kampuni kwa ajili ya nyama na bidhaa nyinginezo zitokanazo na nyama ya nguruwe.

Anakiri kwamba ufugaji wa nguruwe una mafao mengi hasa ikizingatiwa kwamba walaji wa nyama ya nguruwe ni wengi katika maeneo mbalimbali ya Limuru, Kijabe na Nairobi.

Mifugo hawa hula chakula kidogo kwa wakati maalum na kuhifadhi kingi katika miili, jambo linalowasaidia kuongeza uzani mkubwa katika kipindi kifupi cha muda.

Ili kumudu lishe ya nguruwe wao, Waithira hutegemea sana mazao ya nafaka, nyasi na mabaki ya chakula cha nyumbani na hotelini.

Mbali na kuchukua muda mfupi sana kuanza kuzaana, nguruwe pia huhitaji kati ya miezi 6-8 pekee ili kukomaa.

Wanapofikia umri wa miezi miwili, nguruwe huwa wamejaza uzani wa hadi kilo 12, na kwa mwaka mzima wanaweza kuzaa hadi watoto 20 idadi hiyo ikipungua sana.

Japo si rahisi wao kukabiliwa na maradhi, inahofiwa kwamba endapo wataugua African Swine Fever (ASF), basi wanaweza kufa wote kwa mkupuo.