Makala

AKILIMALI: Dereva wa kike aioneaye fahari kazi yake

January 31st, 2020 4 min read

Na MARY WANGARI

HOFU, wasiwasi, shaka na kebehi ndizo hisia za mwanzo zinazoashiria nyusoni mwa abiria, wanapogundua dereva wao siku hiyo si mwingine ila ni Esther Wanjiru mwenye umri wa miaka 26.

Sura yake changa inayomfanya kuonekana kama kijana chipukizi haisaidii hali huku ikionekana kuchochea wasiwasi wa abiria.

Hali huvurugika hata zaidi kutokana na mtindo wake wa mavazi ambao ni tofauti kabisa na mabinti wa hirimu yake.

Kinyume na wenzake wenye hulka ya kutumia vipodozi na kutengeneza nywele za kila aina hali ni tofauti kabisa kwa binti huyu ambaye ni vigumu kupuuza urembo wake asilia.

Nywele zake fupi huku akiwa amevalia sare rasmi ya dereva wa matatu: kaptura ndefu, koti ya mikono mifupi na shati yenye rangi ya samawati, binti huyu ni taswira halisi ya mwanamke anayejiamini na kujivunia anachofanya.

Ni bayana kwamba hisia chanya anazokumbana nazo binti huyu hazimpigi mshipa kamwe na ni kama macho ya chura ambayo hayamzuii kamwe ng’ombe kunywa maji.

Kuanzia tabasamu lake linavyoangaza usoni mwake anapoingia matatu, utulivu, uhakika na ukakamavu wake anaposhika usukani wa gari, ni ithbati tosha kwamba alizaliwa kuwa dereva.

Haichukui muda mrefu kwa nyoyo za abiria kutulia punde baada ya safari kung’oa nanga wakiwa na imani kwamba wako mikononi salama.

Baada ya masafa kadha katika safari yetu, afisa wa trafiki anasimamisha matatu kwa shughuli ya kawaida ya ukaguzi.

Binti huyu anachomoa stakabadhi zote zinazohitajika huku wakiwasiliana bila tashwishwi yoyote na punde si punde tunaruhusiwa kuendelea na safari yetu.

Ni vigumu kukosa kuvutiwa na jinsi anavyomakinika barabarani na kutaniana na madereva wenzake kupitia ishara ambazo ni madereva tu wa matau wanazozifahamu.

Si jambo geni kuwa na manamba wanawake ambao idadi yao imezidi kuongezeka katika siku za hivi majuzi.

Lakini ni nadra sana kuona dereva mwanamke katika ulingo wa matatu ambao aghalabu hunasibishwa na wanaume na wahuni wasio watanashati na wenye hulka ya kuzua fujo na kutumia lugha ya matusi inayokwaruza masikio na hisia.

Ndiposa Wanjiru, dereva wa matatu anayefanya kazi na shirika la matatu la 4NTE, ni kivutio kwa wengi ambao wamekuwa na bahati ya kutagusana na kuwa abiria wake kwenye mkondo wa Nyahururu-Nakuru na Nakuru Nairobi.

Hata hivyo, haijakuwa safari rahisi hadi kufika alipo sasa jinsi anavyotufahamisha Wanjiru, aliyezaliwa na kulelewa mjini Ndaragwa eneo linalofahamika kama Subego.

 

Bi Esther Wanjiru huvalia sare kamili ya dereva wa matatu. Picha/ Mary Wangari

Kama anavyotusimulia binti huyu, hakufikiri kwamba wakati mmoja angekuwa dereva wa matatu alipokuwa akilelewa na wazazi wake Lucy na James pamoja na ndugu zake watatu: Peter, Jane na Mary.

Kulingana naye, ndoto yake alipokuwa msichana mdogo, alitaka kuwa daktari wa mifugo.

Lakini mawazo yake yalibadilika na kuchukua mkondo mpya alipokamilisha masomo ya shule ya upili na hapo ndipo wazo la kujiunga na tasnia ya matatu lilipomjia.

“Nilisomea Shule ya Msingi ya Suguroi na kisha nikajiunga na Shule ya Upili ya Uruku ambapo nilisoma hadi Kidato cha Nne.

“Baada ya kukamilisha elimu ya sekondari niliona kwamba watu wengi wana mazoea ya kuchagua kazi na hapo nikakumbuka kwamba nilijua kuendesha gari nikiwa na umri wa miaka 17 na sikuwa nikiona wasichana wengi wakiendesha matatu,” anatupasha,

Binti huyu anayetujuza kwamba alifahamu kuendesha gari akiwa kijana chipukizi baada ya kufundishwa na mjomba wake, hakukomea hapo.

Alikata kauli ya kutia makali ujuzi wake na kujiboresha hata zaidi huku akifahamu fika kwamba mtaka cha mvunguni sharti ainame.

“Nilijiunga na Shule ya Mafunzo kuhusu uendeshaji gari ili niweze kupata leseni,”

Badala ya kurejea nyumbani kwao baada ya kukamilisha masomo ya uendeshaji gari na kupata stakabadhi zilizohitajika, Wanjiru mwenye moyo shupavu alijitosa nyanjani mzima mzima.

“Baada ya kumaliza masomo na kupata leseni sikurudi nyumbani. Nilienda katika kituo cha matatu cha Maili Nne mjini Nyahururu ambapo nilifanya kazi kama utingo kwa miaka minne,”anatueleza.

Ukiwa mtu mwenye moyo wa kudiriki na kupania makuu, binti huyu baadaye alijiunga na kampuni ya Kiwanja Line Sacco na kufanya kazi kama dereva.

Baada ya kufanya kazi kwa miaka miwili katika shirika hilo alijiunga na kampuni 4NTE kama dereva.

Jinsi anavyotueleza Wanjiru, familia yake imekuwa nguzo yake kuu huku wakimpongeza na kumtia moyo kuzidi kubobea katika tasnia hii.

Hali hii imemwezesha kukabiliana kirahisi na changamoto mbalimbali alizokumbana nazo mwanzoni alipojitosa kwenye ulingo wa matatu ikiwemo unyanyapaa, kudunishwa, bezo, na hata matusi.

“Kwa familia yetu hakuna dereva mwanamke. Ni mimi tu. Huwa wananifurahia sana na wananiunga mkono kwa sababu sikuchagua kazi,” anatueleza.

Kwa sasa Wanjiru anaweza tu kutazama umbali aliotoka akiwa na moyo uliojaa shukrani huku marafiki zake waliomdhihaki hapo mbeleni wakimtafuta kumwomba ushauri.

“Marafiki zangu walinisema wakidhani singetoboa. Lakini kadri miaka inavyosonga, wameanza kunijia wakiniomba ushauri kuhusu wanavyoweza kujiunga na sekta ya matatu,” anasema.

Sawa na jinsi kila safari haikosi panda shuka zake, Wanjiru hajakosa kijisehemu cha masaibu ambayo amekumbana nayo katika ulingo wa matatu.

Ikizingatiwa hali ya sekta ya matatu inayofahamika kwa yote yasiyo mazuri bila shaka imekuwa kibarua kigumu.

“Matatizo ni mengi sana. Kuna baadhi ya watu wanaokuonea wivu wakishangaa ni jinsi gani msichana mchanga unapata hadhi hiyo ya kuwa dereva au hata ulipata vipi ujuzi huo.

“Wakati mwingine inakuwa vigumu kupata mtu anayeweza kukuamini na gari lake kutokana na kasumba potovu kuhusu wanawake, wanaona tu huwezi. Pia huna budi kukabiliana na matusi, madharau na kudunishwa miongoni mwa matatizo mengine,” anatueleza.

Lakini anaweza vipi kukabiliana na changamoto hizi hasa matusi na utani, ni swali tunalomuuliza ambalo hachelei kutupa jibu linatuvutia hata zaidi.

“Kuhusu matusi, mtu huhitajika kuvumilia tu ili uwazoee wadau katika sekta ya matatu. Ni baada ya kuwazoea ambapo unagundua kwamba si matusi na lugha hiyo haikukwazi tena kwa kuwa ni sajili tu ya kituoni mwa matatu,”anatueleza.

Wanjiru anatofautiana na dhana kwamba hakuna ajira nchini huku kama anavyoeleza, kazi ni tele nchini lakini tatizo kuu ni watu wanaochagua kazi akiafikiana na wenye busara waliofahamu fika mchagua jembe si mkulima.

“Ushauri wangu hasa kwa vijana ni kwamba kazi ni nyingi nchini, wafanyakazi ndio wanakosa. Kazi iko, mradi usichague kazi huwezi ukakosa jambo la kufanya litakalokuwezesha kujikimu maishani na kutimiza ndoto yako,” anashauri.

Bila shaka, hata mbungu si upeo kwa binti huyu ambaye ni bayana ni kielelezo cha kuigwa na vijana na kina dada wenzake huku akiwa na maono makuu ya kutamba na kutia fora katika ulingo wa matatu.

“Maulana akinijalia, katika siku za usoni ningependa nimiliki matatu kadhaa, niajili madereva watakaonikusanyia hela huku nikipumzika nyumbani na familia yangu,” anatupasha Wanjiru, nasi tukimtakia kila ka kheri katika maazimio yake.