Makala

AKILIMALI: Hela anazorina kuuza dania, mbegu zake zilifanya auze gari la teksi ya Uber

December 24th, 2020 3 min read

Na GRACE KARANJA

Michael Ngacha ni mzaliwa wa eneo la Mukurweini, kaunti ya Nyeri. Kama wengine wengi alitua kaunti ya Nairobi ili kutafuta kazi ambayo baada ya kufanikiwa aliweza kuweka akiba na kununua gari ambalo aliligeuza na kuwa teksi.

Alijisajili chini ya kampuni maarufu ya ubber kwa zaidi ya miaka mitano. Hata hivyo, ushindani mkubwa katika sekta hiyo ya uchukuzi wa kibinafsi ulimpelekea kuasi biashara hiyo kutokana na upungufu wa mapato.

‘Biashara ilianza kuenda mrama na kukosa faida kwa sababu watu wengi walinunua magari na kuyafanya teksi jambo ambalo lilinilazimu kuliuza gari langu mwaka wa 2018 na kutafuta njia mbadala ya kukimu mahitaji ya familia,’ anaeleza.

Kulingana naye alihitaji kilimo biashara cha mimea ambayo huchukua muda mfupi kukomaa na ambayo mauzo yake ina faida. Baada ya kufanya utafiti wake aligundua kwamba mmea wa dania hukomaa kwa muda mfupi na matumizi yake ni ya kila siku katika mapishi mijini.

Anasema kuwa baada ya muda aligundua alikuwa na tatizo la uhaba wa mbegu anazohitaji na pia gharama ya juu ya mbegu ya mbegu hizo zilizopelekea kuchelewa kusia zingine kwa muda ufaao.

‘Katika kilimo biashara cha dania inatakikana mkulima kuwa na mbegu zake kila mara ikizingatiwa kuwa mmea huu hukomaa baada ya siku 40. Hii ina maana kwamba mmea huu ukiwa na majuma matatu, mkulima anashauriwa kusia mbegu zingine ili asiwe na mwanya wa kuwapoteza wateja. ‘ anaeleza.

Kama anavyoeleza wengi wa watumiaji wa mmea huu hawana ufahamu kwamba mbegu zake zina faida mwilini sawia na matawi yake nia yake sasa ikiwa ni kukuza mbegu hizi na kuwaelimisha walaji kuhusu faida zake.

Utafiti

Kulingana na utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Ayurveda, California, mbegu za dania zina uwezo mkubwa wa kutibu baadhi ya maradhi ya ngozi kama vile ukurutu, mwasho wa ngozi, vipele na uvimbe kwenye ngozi kwani zinaaminika kuwa na viini ambavyo vinavyosaidia kupambana na matatizo hayo.

Pia utafiti huo ulionyesha kuwa mbegu hizi za dania zinasaidia kuponya vidonda vya kinywa. Asidi inayopatikana katika mbegu hizi ina viini vinavyosaidia kupunguza uchungu wa viongo mwilini.

Huku mataifa mengi yakiendelea kutafuta njia za kutibu ugonjwa wa kisukari unaoendelea kuwahangaisha wanadamu inasemekana kuwa nchini India, wengi wamegeukia matumizi ya mbegu za dania kama mojawapo ya njia ya kudhibiti sukari kwenye damu.

Utafiti mwingine uliochapishwa na jarida la Uingereza kuhusu lishe, iligunduliwa kuwa mbegu hizi zina misombo (componds) ambayo ikiongezwa kwenye damu hudhibiti kiwango cha insulini cha mwanadamu.

Kulingana na wataalamu, ukosefu wa usawa wa homoni, kukosa kula lishe isiyofaa ni baadhi ya mambo yanayopelekea mtu kupoteza nywele. Mbegu za dania zinafahamika kwa kuzuia nywele kuanguka kwani huimarisha ukuaji wa mizizi ya nywele na kuifanya kumea upya.

Wanawake ambao huwa na matatizo ya hedhi kuwa nzito wanashauriwa na wataalamu wa lishe kuongeza mbegu za dania katika lishe.Mkulima Michael anaeleza kuwa dania ni mmea ambao unaweza kulimwa pamoja na mimea mingine kwa mfano mboga na mahindi.

Unahitaji maeneo yaliyo na jua cha muhimu ikiwa ni maji ya kutosha. Anasema mmea huu huhitaji jua kali kwa minajili ya mbegu ingawa kuna aina mbili za dania ile ambayo ni fupi na nyingine refu.

Tofauti yake ni kuwa iliyo refu ina ladha ya kupendeza na huwa na harufu inayovutia kwa umbali ikilinganishwa na hii fupi. Kama anavyoeleza, yeye huwa anasia mbegu katika vitalu tofauti ili kutofautisha zile za kuuzwa mapema na zile anazohitaji kukausha na kuzirejesha shambani msimu unaofuata.

Dania za mbegu husubiriwa hadi zianze kutoa maua ya rangi nyeupe ambayo hatimaye huwa na mbegu. Baada ya kukomaa mbegu hizi huvunwa na kukaushwa kwenye jua.

Soko

Baada ya kukomaa huwauzia wafanyabiashara wa jumla katika soko kuu la Marikiti ili kuepuka madalali ambao huwahangaisha wakulima.

‘Mimi niliamua kujitafutia soko mwenyewe, wateja wangu ni wale wanaouza dania kwa jumla ambao nawapelekea moja kwa moja kutoka shambani. Huwa ninafunga tuta la Sh30.

Safari moja ya sokoni huwa napelekea wateja wangu kati ya matuta 1,300 au 1,500. Hivyo baada ya miezi mitatu napata faida ya Sh39,000 hadi Sh45,000, ambayo kila wakati ninapoenda sokoni baada ya siku 40,” akaelezea Bw Ngacha.