AKILIMALI: Huzifikirii sana chupa za plastiki ila kwake ni pesa

AKILIMALI: Huzifikirii sana chupa za plastiki ila kwake ni pesa

Na CHARLES ONGADI

KWA kipindi kirefu wakazi wa Pwani walitegemea sana sekta ya utalii kama kitega uchumi ila mambo yaliwaendea tenge baada ya sekta hiyo kuanza kuyumba.

Wengi walijipata wakipoteza ajira na kuamua kusaka njia mbadala ya kujipatia mkate wao wa kila leo ilmradi maisha yandelee.

Mwalimu Rashid, 49, ni kati ya maelfu ya wakazi wa Pwani waliojipata bila ajira baada ya kufungwa ghafla kwa hoteli ambayo ilikuwa imemwajiri kwa takribani miaka ishirini.

Hata hivyo, kuvunjika kwa mwiko sio mwisho wa kupika, Rashid, mkazi wa Shanzu iliyoko eneoubunge la Kisauni aliamua kutafuta njia mbadala ya kujipatia riziki.

“Mchagua jembe si mkulima, niliamua kununua mkokoteni na kiasi kidogo nilichosalia nacho na kuanza kazi ya kuzoa takataka majumbani kwa malipo,” asema Rashid katika mazungumzo na Akilimali hivi majuzi.

Aidha, Rashid hakuwa na ufahamu kwamba kati ya takataka alizokuwa akizoa nakutupa jaani baadhi yazo zilikuwa na faida kubwa.

Ni hadi pale alipoangukia oda kutoka kwa kampuni ya kutengeneza vyombo vya plastiki, Petco iliyoko kaunti ndogo ya Changamwe, Mombasa kukusanya vyombo vya plastiki vilivyotupwa na kuwauzia.

Kulingana na Rashid ilikuwa ni kazi rahisi kwake kwani alipata kwa wingi vyombo vya plastiki katika taka alizokuwa akikusanya majumbani na hata katika jaa alilokuwa akitupa taka zake.

“Nilikuwa nikikusanya plastiki kwa wingi na kila nilipofikisha kilo 100 kampuni ya Petco ilifika na kuchukua huku wakiniwacha na donge langu,” asilimulia.

Lakini baada ya kipindi kifupi cha mafanikio, Rashid alikubaliana na kampuni hiyo kukusanya plastiki hizo hadi zifikie tani moja ndipo waje kuchukua.

Kulingana naye, haikuwa kazi rahisi kufikisha tani moja kwa kipindi kifupi alichopewa na Petco na wakati huo huo kuwahudumia wateja wake wa taka mtaani.

Kwa hivyo, aliamua kuwaajiri wasaidizi kumsaidia kukusanya vyombo hivi vya plastiki na wakati huo huo kununua vyengine kutoka kwa vijana wanaookota kutoka mahotelini.

Rashid anafichulia Akilimali kwamba anaiuzia kampuni ya Petco tani moja ya vyombo hivyo vya plastiki kwa kiasi kizuri ambacho kimemwezesha kuwalipa wasidizi wake wanne.

Aidha, Rashid amedinda kufichua kiasi anachopata kwa tani moja akisema ni hatari kwa usalama wa biashara yake na hata yeye pia.

“Kwa mwezi mmoja nauza tani mbili na wakati mwingine hata tani tatu kulingana na msimu ulivyo,” asema Rashid.

Kazi yake imeweza kuweka mazingira ya kupendeza bila vyombo vya plastiki vilivyotumika.

Aidha, Rashid amekuwa akirudisha mkono kwa jamii kwa kuidhamini timu ya mchezo wa soka ya vijana kutoka mtaa anakoishi wa Keroport kwa kuwanunulia mipira na sare za kuchezea.

Kulingana na Safari Kadenge, mmoja kati ya wafanyakazi wa Rashid ni kwamba katika kuhakikisha wanakusanya kwa haraka plastiki hizi, wanajigawa kwa makundi mawili.

Kundi la kwanza ninaelekea ufuoni ziliko hoteli za kitalii ambako mara nyingi vyombo vya plastiki hutumika hasa kwa maji ya kunywa.

“Mara nyingi wakati wa mikutano ama semina, tunapata vyombo kibao vya plastiki kutoka hoteli za karibu,” aongeza kusema Safari.

Kundi la pili huelekea sehemu za karibu zinazotupwa takata na kuchakura vyombo hivi vya plastiki na kuleta.

Kisha kuna vijana ambao humuuzia Rashid vyombo vya plastiki kwa Sh1 kwa kila moja na kuongezea kiwango cha tani zinazohitajika.

Aidha, Kashanga Nyaga anaiambia Akilimali kwamba licha ya kufanya kazi ya bodaboda lakini amekuwa akijiongezea pato lake kwa kukusanya plastiki hizi wakati wake wa mapumziko na kumuuzia Rashidi.

“Nashukuru kila siku siwezi kukosa Sh200 kutokana na plastiki ninazokusanya na kumuuzia Rashidi mbali na shughuli yangu ya kila siku ya bodaboda,” asema Kashanga.

Rashid anakiri mbeleni alikuwa na changamoto ya kupata kwa wingi plastiki hizi lakini mara baada ya kuajiri wasaidizi wanne kazi imekuwa rahisi kwake.

Anaongeza kwamba mbali na kujipatia riziki na pamoja na wasidizi wake, pia kazi yake imeweza kuweka mazingira ya kupendeza bila vyombo vya plastiki vilivyotumika.

Kulingana na Rashidi amekuwa akirudisha mkono kwa jamii kwa kuidhamini timu ya mchezo wa soka ya vijana kutoka mtaa anakoishi wa Keroport kwa kuwanunulia mipira na sare za kuchezea.

Rashid anasema ndoto yake ni kupanua zaidi kazi yake kwa kuunzisha kampuni yake ya kutengeza vyombo vya plastiki katika siku zijazo.

Anawashauri vijana kuchangamka na kuwa wabunifu katika kusaka njia ya kujipatia riziki na wala sio kusubiri hadi wapate kazi za ofisini ambazo mtu hajui ni lini atafanikiwa kuajiriwa.

You can share this post!

AKILIMALI: Punda ni ofisi yake; anawauza kwa wanaosaka...

Ubelgiji yazamisha Belarus na kufungua mwanya wa alama tisa...