Makala

AKILIMALI: Jifunze biashara ya kurembesha viatu

April 2nd, 2020 2 min read

NA MARGARET MAINA

[email protected]

Mwanafunzi mmoja katika Chuo Kikuu cha Unicaf ambaye ni mkazi wa Thika,  alijiuliza swali ambalo limemletea manufaa maishani. “Ikiwa watu 500 wana viatu vingi vinavyofanana, ninaweza kufanya nini kubadili mwonekano wao?”

Hili lilikuwa swali ambalo lilikuwa katika akili ya Westbury Ngigi, 21 ambaye alianzisha suluhisho kwa kurekebisha viatu ili iwe sawa na matakwa ya mteja wake kwa kuongeza muundo na rangi.

Alianzisha biashara yake ya kubuni mnamo Septemba 2019 kwa kutumia talanta yake ya sanaa ili kupata pesa za kugharamia mahitaji zake za kila siku. Alianzisha biashara hii kwa Sh3600 aliyopewa na baba yake.

“Nilianza sanaa nilipokuwa mchanga na nilipata shida na waalimu wangu kwani nilikuwa nikichora picha za vibonzo hata kwenye vitabu vya shule yangu, wazazi wangu waligundua nilikuwa na talanta,” anasema

Bw Ngigi alijifunza biashara hii kutoka kwa Maxine Wabosha ambaye aliwahi kufanya video kuhusu jinsi ya kubadilisha viatu kupitia YouTube.

Mbali na kubadili mwonekano wa viatu Bw Ngigi pia anachakata chupa za glasi na kuzibadilisha kuwa vipande ya mapambo kwa kutumia vitambaa vya Ankara.

“Ninatumia rangi na brashi kupamba viatu. Kununua rangi kunanigharimu Sh 800 kwa seti ya rangi kumi,” viatu Sh300 na brashi Sh100.’’

Bw Ngigi basi huuza viatu kati ya Sh550 hadi Sh700 kulingana na ugumu wa muundo. Wengi wa wateja wake ni wanawake lakini yeye vile vile hutengeneza viatu vya kiume na vya watoto.

Bw Ngigi ameyauza zaidi ya jozi 150 tangu Septemba, Ngigi aatarajia kuitumia faida yake kutoka kwa mauzo kuanzisha studio ya Sanaa

Ufikiaji mkubwa wa uuzaji kwenye mtandao ya kijamii na hamu inayokua miongoni mwa wateja wake imesababisha kufanikiwa kwa Bw Ngigi kibiashara kote nchini.

Alipoulizwa kwanini alianza kuchakata chupa za glasi, Bw Ngigi alisema kuwa hitaji la utunzaji wa mazingira lilimchochea.

“Niliona haja ya kuhifadhi mazingira na nilidhani nitumie vizuri chupa zilizokuwa zimewekwa kila mahali kwa kuzisindika tena. Kwa hivyo nilianza kuchakata kwa kuzibadilisha kuwa vipande vya sanaa,” anasema.

Bwana Ngigi anatarajia kupanua biashara yake na kutoa mafunzo kwa vijana wengine kwenye ustadi huo.

Anashauri vijana wasilalamike juu ya ukosefu wa kazi bali watumie talanta zao na kuwa wenye akili.