AKILIMALI: Jinsi bidhaa za sodo zinazoweza kudumu hadi miaka 10 zilivyobadilisha maisha yake

AKILIMALI: Jinsi bidhaa za sodo zinazoweza kudumu hadi miaka 10 zilivyobadilisha maisha yake

Na MARY WANGARI

HEBU fikiria kuhusu sodo inayoweza kutumika mara zaidi ya moja na inayoweza kudumu hadi kwa miaka 10!

Ebby Weyime 33, anaendesha biashara ya uundaji na uuzaji wa sodo hizo za kipekee (reusable pads) na vikombe vya hedhi (menstrual cups) kupitia kampuni yake, Grace Cup aliyoanzisha 2017. Amepania kuboresha afya ya uzazi kwa wanawake kwa njia inayowapa thamani kwa pesa zao na wakati uo huo kuhifadhi mazingira.

AkiliMali ilipomzuru afisini mwake, mahafala huyu aliyefuzu kwa Shahada ya Biashara na Mauzo kutoka Chuo Kikuu cha Day Star, 2011, alikuwa mwingi wa bashasha tayari kutujuza zaidi kuhusu bidhaa hizo za aina yake, ambazo kwa hakika ndio mwanzo zinaingia katika soko la Kenya.

Kilichoanza tu kama juhudi za kupata suluhisho la kudumu kutokana na kero la kila mara wakati na baada ya hedhi, kiligeuka uvumbuzi muhimu.

“Nilipata motisha kutokana na mahitaji yangu mwenyewe. Nilikuwa natafuta bidhaa ambazo ni tofauti na sodo za kawaida tulizozowea. Sodo za kawaida zilikuwa zinanichoma, ningali na makovu. Nilikuwa nikitumia sodo na tampons kwa pamoja,” anaeleza.

Reusable pads huhitaji tu kusafishwa vizuri kukaushwa kabla ya kutumiwa tena, zinaweza kudumu hadi kwa miaka mitatu…Picha/MARYWANGARI

Utafiti

Akiwa amekata tamaa kabisa kutokana na masaibu yake kila mwezi, mwigizaji huyu ambaye vilevile ni mwanamitindo ya urembo, alianza kufanya utafiti kwenye mtandao wa Google, akitumai kupata bidhaa mbadala, ambazo zingemnusuru.

Wakati wote huo alikuwa akiishi Afrika Kusini alipokuwa akifuata ndoto yake ya uigizaji na miondoko ya urembo. “Nilikumbana na reusable pads kwa mara ya kwanza nilipokuwa nikiishi Capetown. Niliona watu wakizitumia, nikafanya utafiti na nikaamua kuzijaribu. Niliridhishwa mno na matokeo,”

“Nilianza kujiuliza ni bidhaa ipi nyingine ninaweza kutumia kando na sodo za kawaida? Nilitafiti kupitia Google na hivyo ndivyo nilifahamu kuhusu vikombe vya hedhi. Nilipata kikombe changu kwa mwanamke aliyekuwa akijiundia vifaa vyake binafsi na maisha yangu yakabadilika kabisa,” anaeleza.

Akiwa amejihami kwa maarifa na mshawasha wa kuwasaidia wanawake na wasichana wengine wanaopitia hali kama yake, alirejea Kenya mnamo 2017 na kufungua biashara yake miezi mitatu baadaye. Mtaji wake wa kwanza ulikuwa Sh200,000, alizokuwa amehifadhi kama akiba, huku familia yake ikimpiga jeki kwa mkopo.

“Ilichukua muda lakini baadaye nililipa deni lote lakini pesa huwa hazitoshi hasa unapoanzisha biashara. Chochote ulicho nacho anza tu nacho. Kwa sasa Grace Cup inachangia asilimia 90 ya mapato yangu,” anafichua.

“Bidhaa zetu zinajumuisha kikombe cha hedhi (reusable cups) kinachoweza kutumika mara kadhaa hadi kwa miaka 10. Kifaa hicho huwa hakivuji iwapo kitaingizwa ipasavyo. Unaweza ukakaa nacho kwa hadi saa 12. Hakina harufu, unaweza ukafanya chochote upendacho iwe ni kulala, kutembea, kukimbia kuogelea au hata kupanda farasi,”

“Sodo zetu zinahitaji kuoshwa tu kabla ya kutumiwa tena. Hazichomi, ni laini kwenye ngozi. Zinaweza kutumika kwa hadi miaka mitatu. Kinyume na sodo za kawaida ambazo hutupwa tu kila baada ya matumizi, bidhaa zetu mbili zinasaidia kuhifadhi mazingira kwa sababu hakuna kinachotupwa. Tunahifadhi mazingira huku tukipata hedhi kwa fahari!” anaeleza akichanua tabasamu la kuvutia.

VIKOMBE VYA HEDHI (MENSTRUAL CUPS)

Kuna aina mbili: vile vya kawaida (regular cups) na anti-bacterial cups, jinsi anavyofafanua.  Grace Cup ni maarufu kwa anti-bacterial cups ambavyo ni vya pekee duniani kote huku ikijivunia haki miliki ya bidhaa hiyo.

Tofauti kuu kati ya bidhaa hizi ni kwamba, vikombe vya kawaida huhitajii kuchemshwa kwa maji yaliyotokota ili kuvishafisha na kuua viini na huuzwa kwa Sh2000. Antibacterial cups, ambavyo anavitaja kama mwafaka zaidi kwa soko la Afrika, havihitaji kuchemshwa ila kukamuliwa tu kwa maji safi kabla ya kutumiwa na hugharimu Sh3,200.

Antibacterial cups vinatofautiana na vikombe vya hedhi vilivyo sokoni kutokana na ute unaovizingira ambao hutoa kinga dhidi ya bakteria (protective gel). Ute huo hauangamizi bakteria bali huzifukuza na kuzizuia kukwamilia kwenye kikombe. Aidha, una hiari ya kununua sodo moja kwa Sh330 au paketi moja inayosheheni sodo nne kwa Sh1250.

“Wateja tunaolenga ni wanawake wa mijini wanaotilia maanani thamani ikizingatiwa bei ya Sh3200 ni ghali kwa baadhi ya watu. Tunalenga pia serikali za kaunti na mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo hununua bidhaa zetu kwa wingi na kuwasambazia kina dada kwa bei nafuu,”

Hutumia mitandao ya kijamii kama vile Instagram na Facebook kutangaza bidhaa zake.Ili kuhakikisha ubora wa kiwango cha juu, mwekezaji huyu chipukizi ameshirikiana na mashirika kutoka Canada na China, sababu kuu ikiwa kupunguza gharama ya uundaji bidhaa na malighafi inayotumika.

“Tunaagizia bidhaa zetu kutoka China kwa sababu hatutumii pamba. Sodo zetu hutengezwa kwa kutumia malighafi inayofahamika kama bamboo charcoal fiber inayopatikana barani Asia pekee. Ni nafuu zaidi kwa sodo hizo kutengezewa huko na kisha tuziuze huku,”

Huku akisherehekea miaka minne tangu alipoanzishwa kampuni yake, safari haijakosa pandashuka zake. “Changamoto kuu ilitokana na kwamba watu hawakuwa wakielewa wala kufahamu chochote kuhusu vikombe vya hedhi. Nililazimika kufanya uhamasishaji mwingi. Nilihangaika kupata mauzo kwa miaka miwili,”

“Tatizo lingine lilikuwa kubadilisha mtindo. Utaanzaje kuwashawishi wanawake waliozoea sodo za kawaida zinazotumiwa mara moja tu na kutupwa kwamba sasa kuna kifaa kingine unachoweza kutumia mara kadhaa?”

Hakufa moyo ila aligeuza changamoto hizo kumfaidi. Alihudhuria mafunzo ili kutia makali ujuzi wake. Juhudi zake zilizaa matunda alipopata cheti za ukufunzi kutoka Wizara ya Afya ambapo sasa huwaelimisha wanafunzi katika shule mbalimbali nchini kuhusu afya ya uzazi kwa jumla.

Miongoni mwa maazimio yake ni kuanzisha mfumo wa kidijitali hasa wakati huu wa janga la Covid-19, ambalo limesababisha shule nyingi nchini kusitisha shughuli za ziada. “Katika siku za usoni, ninatumai kupanua huduma zangu ili kujumuisha mafunzo na kufanya Grace Cup kuwa kituo ambapo wanawake wanaweza kujihisi salama wanapozungumza kuhusu masuala yanayochukuliwa kama mwiko katika jamii ya Kiafrika,”

“Wanawake wanapaswa kukubali bidhaa za kisasa ambazo si bora tu kwa matumizi bali pia zinalinda mifuko yao na kuhifadhi mazingira,” anasema.

Mwnyambura@ke.nationmedia.com

You can share this post!

Wabunge kusafiri Denmark kunoa bongo kupitisha mswada wa...

Waziri wa zamani Henry Rotich alilipa kampuni ya Italy SH8BN

T L