AKILIMALI: Jinsi mfugaji anavyoweza kukabili kero ya gharama ya juu ya lishe

AKILIMALI: Jinsi mfugaji anavyoweza kukabili kero ya gharama ya juu ya lishe

Na SAMMY WAWERU

GHARAMA ya chakula cha mifugo inaendelea kupanda kila uchao hasa kwa sababu ya bei ya mafuta ya petroli.

Mwaka huu, 2021, bei ya petroli, dizeli na mafuta ya taa imeandikisha kupanda mara kadha, licha ya athari za janga la Covid-19 kukalia taifa.

Bei ya mafuta ya petroli inapopanda, ni ishara ya gharama ya maisha kuwa ghali.

Mafuta ya petroli, ni miongoni mwa bidhaa ambazo ni nguzo za ukuaji wa uchumi. Yanategemewa katika sekta ya usafiri na uchukuzi.

Isitoshe, kuna baadhi ya viwanda vinavyotumia mafuta ya petroli kuendesha shughuli zake.

Bei ya petroli ilipoanza kupanda, mfumko wa bei ya bidhaa nao ulishuhudiwa.

Chakula cha mifugo hakijasazwa, na kimekuwa kikiendelea kuwa ghali.

“Mfuko wa kilo 50 tuliokuwa tukinunua chini ya Sh2, 500 sasa umepanda na kuwa zaidi ya Sh3, 000,” anasema Joseph Mathenge, mfugaji wa mbuzi wa maziwa Kiambu.

Ni ongezeko ambalo huenda likachangia wafugaji wengi kulemewa kuendeleza jitihada zao.

Hata hivyo, badala ya mahangaiko hayo, wafugaji wanahimizwa kukumbatia mkondo wa kujikuzia nyasi na mimea inayolishwa mifugo.

Aidha, kuna nyasi za aina mbalimbali kama vile Mabingobingo (napier grass), Lucerne, Brachiaria, miongoni mwa nyinginezo.

Mifugo pia hulishwa punje za mahindi, majani ya mahindi, ngano, maharagwe, migomba ya ndizi, kati ya malisho mengine.

Huku wengi wakiwa na mazoea ya kuwapa mifugo malisho mabichi, wafugaji wanahimizwa kuwapa yaliyokauka.

Nyasi zilizokauka, huwapa mifugo motisha kunywa maji kwa wingi, jambo ambalo huongeza kiwango cha mazao, kama vile maziwa.

Malisho mabichi huwa na wadudu, ambao ni hatari kwa mifugo.

Ili kurahisishia mifugo kibarua, mfugaji anashauriwa kuwakatakatia nyasi, na ikiwezekana kuzisaga.

Kuna mashine mbalimbali za shughuli hiyo kama vile; Chuff cutter, Choppers, Feed mixers, Maize hullers, kati ya nyinginezo.

Nyasi zilizokauka zimegawanywa kwa makundi mawili; silage na hay.

Silage, ni nyasi zilizovunwa, na kuhifadhiwa kwa kutumia madini yenye uchachu, ili kuongeza na kudumisha kiwango cha Wanga na Protini, huku Hay ikiwa nyasi zilizovunwa na kukaushwa.

Kimsingi, hatua ya kujikuzia nyasi au mimea na kuziongeza thamani kwa kukausha na kuongeza madini faafu, ni mfumo wa kujitengenezea chakula.

“Wafugaji walioukumbatia, wamepunguza gharama kwa kiwango cha juu,” anasema mtaalamu Francis Nduati kutoka Simba Farm Machinery, kampuni inayouza mashine za kusaga.

Francis Nduati kutoka Simba Farm Machinery, akifunga mashine ya mfugaji eneo la Mariira, Murang’a. Picha/ Sammy Waweru

Mdau huyu anasema, mkulima au mfugaji atakuwa na uhakika wa chakula anachowapa kuku, ng’ombe, mbuzi na kondoo wake.

“Chakula kingi cha madukani huwa hakijaafikia ubora wa bidhaa, jambo ambalo linaendelea kukandamiza wafugaji,” Nduati asema, akihimiza wafugaji kukumbatia matumizi ya mashine kujiundia lishe.

Kuna mashine zinazotumia nguvu za umeme, na stima zinapopotea zinawekwa mafuta ya petroli, dizeli au kuunganishwa na sola.

You can share this post!

Lukaku asema haondoki kambini mwa Inter Milan

Ufaransa wapepeta Wales 3-0 kirafiki