Makala

AKILIMALI: Jinsi mitego maalumu inavyotumika kuwakabili wadudu waharibifu wa mimea na mazao

December 9th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

KUENDELEA kuenea kwa ugonjwa hatari wa Saratani na athari zake kunahusishwa na mlo, kando na baadhi ya waathiriwa familia yao kutajwa kuwa na historia ya gonjwa hilo.

Wakati wa mazishi ya aliyekuwa Gavana wa Bomet, Joyce Laboso, ambaye aliangamizwa na Saratani, Rais Uhuru Kenyatta alisisitizia haja ya kutathmini chakula tunachobugia.

Kiongozi wa nchi, alisema “Haya mazoea ya kula bidhaa zilizosindikwa (processed food) kwa kiasi kikubwa yamechangia kukithiri kwa janga la Kansa, na hatuna buda kurejelea chakula asilia na mazao ya kilimo ambayo hayajazalishwa kwa kutumia pembejeo zenye kemikali.”

Pembejeo zinajumuisha mbegu, mbolea hususan fatalaiza na dawa za kukabili wadudu na magonjwa yanayoathiri mimea na mazao.

Matumizi ya fatalaiza na dawa zenye kemikali yanachangia mazao ya kilimo kuwa hatari kwa walaji, yakitajwa kusababisha maradhi sugu kama vile Saratani.

Huku viongozi na wataalamu wa masuala ya afya, kilimo na pia WanaSayansi, wakijaribu kuhimiza haja ya kutathmini ubora wa chakula na kilicho salama kisiha, mchakato huu hautaafikiwa bila kuhusisha wazalishaji, ndio waundaji wa fatalaiza na dawa, na wakulima.

Shambulio la wadudu kwa mimea na mazao, ndilo linachangia matumizi ya dawa zenye kemikali kuwakabili. Waliokumbatia kilimo kwa minajili ya biashara, lengo lao ni namna ya kupunguza gharama na athari za wadudu na magonjwa.

Hata hivyo, wataalamu wa kilimo wanahoji kuna mifumo kadha wa kadha, itakayowezesha wanazaraa kupata mazao bila kutumia dawa zenye kemikali, hususan katika kukabiliana na wadudu.

Wanasema inasaidia kurejesha sekta ya kilimo katika mifumoasilia, na kupata mazao salama.

Mtaalamu Caroline Murage, anadokeza kuvumbuliwa kwa mitego ya rangi tofauti kunasa wadudu.

Kulingana na mdau huyo, wadudu wengi huvutiwa na rangi ya kijani na pia ya maua, hivyo basi mitego yenyewe inapaswa kuwiana na mimea na mazao.

“Inatengenezwa kwa karatasi za nailoni na kuwekwa gamu kuwanasa. Huning’inizwa kwenye matawi ya mimea,” Caroline anaelezea.

Aidha, huwa imetiwa dawa ya kuua wadudu.

“Muhimu zaidi ni kuepusha mimea na mazao kupuliziwa dawa ambazo huenda zikawa hatari na kuzuia kupatikana kwa mazao salama,” anasisitiza.

Isitoshe, kuna wadudu wanaovutiwa na harufu ya maua (nectar), na hao ndio lengo kuu, kwani maua yanapochana ni dalili ya mazao kubisha hodi.

“Mitego pia huwekwa dawa zinazonukia ili kuwavutia,” Caroline anasema, akieleza kwamba wadudu wanaoshambulia mimea ya familia tofauti na mazao ni wale wamoja.

Matumizi ya mitego hiyo ya kipekee, yamesaidia Gad Kibiwott, mkulima Kaunti ya Laikipia kupata mazao salama.

Kulingana na mkulima huyo, ambaye hukuza mimea inayochukua muda mfupi kuvunwa, mazao yake ya nyanya, brokoli na spinachi ni yenye ushindani mkuu sokoni kwa kile anataja kama kuepuka kupulizia dawa zenye kemikali kukabili wadudu.

Hulima katika eneo tambarare na pia kwenye kivungulio (greenhouse).

“Nina mitego inayokabili wadudu hatari kwa nyanya, hasa Tuta absoluta na ya manjano kukabiliana na nzi weupe na vipepeo waharibifu,” Gad anadokeza.

Mtego wa Tuta absoluta unafahamika kama Tuta trap.

Erastus Muriithi, mkulima wa nyanya Kirinyaga anasema ikiwa kuna wadudu waharibifu kwa matunda ya nyanya waite Tuta absoluta. “Wakiingia shambani, usitarajie kupata mavuno. Hutoboa nyanya na kuzaana mle ndani, kuwaondoa ni kibarua,” Muriithi anaelezea, akisema wamekuwa kero kuu katika jitihada zake kwa kilimo.

Gad anasema Tuta trap ndicho kiboko cha wadudu hao. “Mtego huu umewekwa dawa (pheromones) inayovutia spishi ya wadudu hao wasumbufu kwa nyanya na kuwaangamiza,” anafafanua.

Katika mdahalo wa kukabili wadudu, pia kuna matumizi ya mikebe kama mitego, hususan katika kilimo cha matunda kama vile maembe.

Aidha, mitego hiyo imegawanywa kwa makundi mawili: Bactrolure – kukabili nzi wa kiume wanaoshambulia matunda na Torula – ya kukabili wale wa kike.