AKILIMALI: Jinsi ufinyanzi inavyomfaidi

AKILIMALI: Jinsi ufinyanzi inavyomfaidi

NA WACHIRA ELISHAPAN

Mara tu jogoo wa kwanza anapowika ndipo Stephen Kariuki anafunganya virago vyake kutoka nyumbani kwake kiria, kaunti ya Murang’a kwenda katika biashara yake ya ufinyanzi ambayo anadhamini sana.

Kazi hii ya ufinyanzi anaifanya kwa kujitolea vikubwa ili kumsaidia kukidhia mahitaji yake ya kimsingi. Kati ya bidhaa anazofinyanga ni jiko la mkaa na lile la kuni.

Kariuki aliianza biashara hii baada ya kugundua pengo kubwa katika ufinyanzi na hivyo akaamua kuzamia pengo hilo kwa nia ya kujipatia kipato kidogo chake na familia yake.

“ Napenda sana kazi hii yangu ya ufinyanzi kwa sababu ya pato lake: si la juu ila si la chini. Niligundua kuna pengo kubwa sana katika ufinyanzi,na ndipo nikaamua kujishughulisha nao,japo haikuwa rahisi,” anasema Stephen.

Anasema kwamba alivutiwa na jinsi ambavyo wafinyanzi wengi katika eneo lao na hasa wa vyungu walivyofanya kazi zao kwa umoja na kwa kujitolea hadi wakaweza kujimudu kimaisha. Wengi wa wafinyanzi ambao Stephen anawatumia kama kielelezo tayari wana mashamba makubwa ambayo kulingana naye waliyanunua walipokuwa wakianza kazi hiyo.

“ Wengi wa watu ninaowaenzi tayari wamefanikiwa. Wamenunua mashamba na magari na tayari wamejenga mijengo mikubwa na ya thamani kubwa,” anasema.

Alipokuwa akianza ,Stephen anasema kwamba alianza kwa mtaji wa shillingi 10,000 pekee,pesa ambazo alizitumia kununua udongo wa kufinyanga ,pamoja na mchanga maalum wa ufinyanzi.

Kazi zote hizi alizifanya peke yake katika shamba lake huko nyumbani Kamaguta katika eneo bunge la Kiharu kaunti ya Murang’a. kulingana naye,kufanyia kazi nyumbani hakukuwa na raha yoyote kwani alihitajika kubaki nyumbani mchana kutwa.

Ni sababu hiyo ambayo ilimfanya kuhamia nyumba moja ya kukodisha ambayo aliikodi kwa shillingi 2,000,na hapo alikuwa akifanyia ufinyanzi wake nyumbani kisha anayaleta majiko aliyooka mwenyewe ili kuyauzia chumbani humo.

“ Nilianza kwa mtaji mdogo wa shillingi elfu kumi pekee na nilikuwa nikifanyia kazi hiyo nyumbani,kwa hiyo sikuwa nikilipa kodi. Lakini nisingehimili kukaa nyumbani kwa muda wote huo,na ndiposa nikakodi chumba pale Kiria. Hapo nilikuwa naokea majiko yangu nyumbani,kisha nayaleta hapa kwa shughuli za kuuza,” anasema.

Kadri siku zilivyoendelea kusonga, Kariuki anadokezea Akilimali kwamba,upendo wake kwa kazi hii ndivyo ulivyoendelea kuzidi.

Kariuki anasema kwamba tangu hapo shirika moja lisilo la kiserikali lilojiita GIZ liliwapa yeye kati ya wengine mafunzo anuwai kuhusu shughuli nzima ya ufinyanzi.

Ni mafunzo hayo ambayo yalimsaidia na tangu hapo hakukawia kupanua biashara yake zaidi . Aliamua kukodi nyumba nyingine itakayotumika kama karakana ya kuhifadhi bidhaa zake mara tu zinapowasili kutoka nyumbani kwa bei nyingine ya shillingi 1500 pekee.

“ Siku moja lilikuja shirika lisilo la kiserikali kwa jina ( GIZ) kutoa mafunzo kuhusu ufinyanzi. Mimi nilikuwa kati ya waliopokea mafunzo hayo. Mara ndipo niligundua kwamba sehemu niliyokodisha imekuwa finyu sana,na nikaamua kukodi nyumba nyingine ili nipate nafasi ya kuhifadhi majiko yangu mara ninapoyaleta sokoni ,” anadokeza Stephen.

Kupitia kwa kazi hii pekee,Stephen amefanikiwa kununua shamba nusu ekari,kwa mtaji anaojipatia kwa shughuli nzima. Ni katika shamba hili ambapo amehifadhi udongo mweusi wa kukandia majiko yake ambayo yanaundwa kwa kupachika udongo katika mashine,kisha kuuzungushwa hadi yatwae umbo la mviringo. Majiko hayo hatimaye yanapashwa moto ili yahimili vishindo.

“ Tangu nianze kazi hii,nimeweza kununua shamba hili unaona hapa kwa pesa ninazopata hapa. Ni rahisi sana kuunda majiko ya mkaa na yale ya kutilia kuni. Tunachukua udongo maalum tuliochanganya kwa utaalamu wetu,kisha tunauweka kwenye mashine ya mviringo na kuzungusha. Matokeo yanakuwa ni umbo la mviringo,tena tunaanika juani au kupitisha motoni,” anasema.

“ Udongo wa kufinyanga tunaununua huko Maragua,nao mchanga maalum unaochanganywa ili kupata udongo utakaoshika vizuri,tunanunua Kabuta,” anadokeza

Kariuki anasema majiko yake yanaundwa vizuri na yanaweza kusafirishwa mbali bila kupata hasara kupitia kuvunjika au kuharibika. Aidha anasema anajivunia kuwaajiri vijana 6 ambao kufikia jioni huwalipa shillingi 1200 na zaidi. Kwa siku moja, anasema kwamba wao huunda majiko yapatao 200 au zaidi kulingana na wateja.

“ Majiko yetu ni imara, hayavunjiki ovyo. Tunayasafirisha hadi umbali wa huko Mombasa bila hata moja kuvunjika. Hata nimewaajiri vijana 6 ili wanisaidie kazi,ninawalipa shillingI 1200 kwa siku kulingana na kazi ya mtu,” anadokeza.

Kariuki anasimulia jinsi msimu wa mvua huwa mzuri kwa kazi kwani ndipo yeye hufanikiwa kupata faida zaidi katika kazi yake. Anasema kwamba msimu mmoja wa mvua humpa yeye kipato cha zaidi ya laki mbili. Soko la bidhaa zake ni majirani,mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na wafanyibiashara kutoka masoko mbalimbali.

“ Msimu wa mvua huwa mzuri kwa sababu huwa wananunuzi wanakuwa wengi. Kwa wakati mmoja huwa nauza majiko takribani 1200 kwa zaidi ya Sh200,000. Huwa napata wateja kutoka mbali na karibu,” anasema.

Kwa kuwa yeye hufanyia biashara yake mahali palipo na barabara,amefanikiwa kununua gari moja ndogo ambalo kulingana naye hubeba takribani majiko 75 pekee ila ndoto yake ni kununua lori kubwa kubebea bidhaa zake. Jiko moja la makaa linauzwa kwa shillingi 600 huku lile la kuni likiuzwa shillingi 180.

Kariuki anasema kwamba changamoto kubwa katika kazi yake ni jinsi ya kununua mashine za kufinyanga kwani anasema ni za bei ghali mno. Isitoshe,anasema kwamba namna ya kusafirisha mali zake sokoni wakati mwingine humlemea kwani anahitaji gari kubwa kusafirisha majiko yote aliyounda sokoni.

Mbunge wa eneo hilo Ndindi Nyoro amekuwa mstari wa mbele kuwausia vijana kujihusisha katika kazi za aina hiyo na hata kuanzisha miradi ya vyuo vya mafunzo anuwai kama kile cha Kiharu technical institute.

“ Ningewaomba vijana na wazazi kuwapeleka Watoto wao kwenye vyuo vya ufundi,ili wasaidike katika kujiinua kimaisha,” alisema Nyoro wakati mmoja.

Hata hivyo, anawaomba vijana kujitokeza kufanya kazi za kujiajiri ili kuepuka kuwa na msongo wa moyo,mara tu kazi zinapokwisha.

You can share this post!

Shirika linavyohangaishwa na wanyakuzi wa ardhi

Beckham pabaya kikosi chake kukiuka kanuni za MLS...