AKILIMALI: Jinsi vijana watatu Mathare Kaskazini wanavyonufaika kwa kuyapaka magari rangi

AKILIMALI: Jinsi vijana watatu Mathare Kaskazini wanavyonufaika kwa kuyapaka magari rangi

Na WINNIE ONYANDO

WAKIWA katika mavazi yao maalum ya kazi na mikononi wameshika mashine za kutumia wanapopaka rangi magari, vijana watatu wenye umri wa miaka 25 kila mmoja wanaonekana wakiwa katika harakati ya kulipaka rangi gari aina ya Toyota Corolla katika karakana yao ya kazi.

Karakana hiyo ya Komenjwe imekuwa kama ‘Taasisi ya Kiufundi’ wa juakali miongoni mwa vijana barobaro ambao hawakupata nafasi ya kuendeleza masomo yao wanaotoka katika mtaa wa Mathare Kaskazini jijini Nairobi.

Kupitia mwalimu wao maarufu mwenye uweledi mwingi katika taaluma ya umekanika Bw Victor Ochieng’ almaarufu Ombeyi, vijana wengi wamejifunza kazi za juakali ambazo zimekuwa namna ya kitega uchumi kwao na hivyo kuwakimu.

Japo gari lako linaonekana mzee kutokana na rangi kuchipuka, vijana hao wana umaarufu kwa kulifanya gari lako kupata mwonekano nzuri na kuvutia.

Kulingana na data ya Soko la Magari nchini, gari aina ya Toyota limepata soko sana nchini huku mauzo yake ikipanda kwa asilimia 23 mwaka huu wa 2021.

Hii ni ishara tosha kuwa asilimia 25 wana magari ya kibinafsi nchini Kenya. Ukilinunua gari, basi jiandaye kuligharamia kwa kila hali.

Vijana hao, Joel Ochieng almaarufu Jajawa, Francis Bita, na Isaack Ouma almaarufu Obwogo wanaeleza kuwa walipatana Nairobi na kuamua kukiunda kikundi ambacho kingetoa mafunzo kwa vijana barobaro kama wao katika kazi ya juakali hasa katika sekta ya umekanika.

Kikundi walichokianzisha mwaka wa 2015 kimewatunza na familia yao. Wamepitia changamoto nyingi ila bado wamesimama kidete kuhakikisha kuwa ndoto zao zitakuja kutimia.

Walipohojiwa na Akilimali, vijana hao walieleza kuwa waliamua kuanzisha biashara hiyo kama njia moja ya kuwapa vijana mafunzo katika umekanika wa magari na kuwapa mbinu za kujitegemea badala ya kuingia katika mihadarati.

“Sisi kama vijana tunapitia changamoto nyingi, hasa katika mitaa kama haya tunayoishi. Badala ya kukaa na kuingia katika vikundi visivyofaa, tuliamua kujiunga pamoja na kuunda ‘shule ya mafunzo’ hapa,” akasema Obwogo.

Hadi sasa, vijana zaidi ya 10 wamepata mafunzo yanayohusiana na umekanika katika geraji hiyo.

Kila mmoja akiwa na kitengo chake cha uweledi, wanatumia tajriba yao kuwafunza vijana kutoka sehemu mbalimbali nchini kujiendeleza kitaaluma hasa wale ambao hawakupata nafasi za kuendelea na masomo yao baada ya kumaliza shule za msingi kutokana na karo.

Wengi wamenufaika kutokana na bidii ya hao vijana watatu. Kando na kutafuta pesa, wanasema kuwa wanafurahia zaidi ikiwa aghalau kijana mmoja amejifunza mambo mawili matatu katika umekanika.

Kama wanavyotueleza vijana hao, biashara haijakuwa rahisi hasa baada ya janga la corona kuilivamia na kuzorota uchumi wa nchi ya Kenya.

Kulipaka rangi gari huchukua muda na unahitaji umakini na uangalifu. Magari hutofautiana kirangi. Kuna wengine wanaopenda magari ya rangi nyeupe, samawati, nyekundu, hudhurungi, bluu, kijivu na kadhalika.

Katika karakana yao, vijana hao wana rangi ya kila aina kulingana na upendeleo wa mteja. Wana vifaa mbalimbali wanavyotumia katika kukamilisha kazi yao ya upakaji rangi.

Wanavitumia vifaa kama vile mashine ya kujazia rangi (compressor machine), bunduki ya kupaka rangi (paint spraying gun), na msasa (sandpaper).

Hii hutumika katika kuhakikisha kuwa sehemu zilizochipuka zimelainishwa na kuwa nyororo kabla ya kupaka rangi.

Kabla ya kulipaka rangi gari, vijana hao wanatumia gazeti kufunika sehemu ambazo hawataki rangi iendee. Wanatumia tepu kuyashikilia magazeti katika sehemu ambazo hawataki ziendewe na rangi.

Rangi ya kwanza ni primer ambayo hutumika kuupa mwili wa gari matunzo. Rangi hiyo ya kwanza pia hulinda gari dhidi ya kutu, mabadiliko ya joto, matuta, vidonge vya mawe na miale hatari ya jua.

Kulipaka gari rangi ya kwanza pia huboresha uwezo wa rangi kudumu kwa gari lenyewe kwa muda mrefu.

Rangi ya kwanza huweza kupakwa mara nne na kuachwa kukauka kwa muda wa dakika 10 hivi ili kuleta unyororo katika sehemu zilizoathirika.

“Rangi huchaguliwa kulingana na mteja, ikiwa gari lake lina rangi ya bluu, hivyo tutatumia rangi iyo hiyo. Ikiwa anahitaji rangi ya gari kubadilishwa, basi tutafanya kazi kwa haraka sana na kutia pesa mfukoni,” Obwogo akaelezea Akilimali.

Baada ya hapo, gari hilo hupakwa rangi ya kufunika ile ya kwanza (base coat) ambayo hung’aa. Aina hii ya rangi huweza kupakwa mara tatu na kuachwa ikauke kwa muda wa dakika 10 kila mmoja.

Baada ya gari kuwa laini, mwisho kabisa gari hilo hupakwa rangi laini na nyembamba ambayo hufunika kila kitu (clear coat). Mara nyingi huwa wanatumia rangi aina ya 1K ama 2K kulingana na aina ya gari.

Kwa kawaida, aina hii ya rangi ni wa kudumu, na kukinga bodi ya gari dhidi ya jua kali pamoja na kutu.

“Mteja anapolileta gari lake katika karakana yetu, sisi humpa huduma nzuri. Tutalipaka rangi naye afurahie kama mteja,” walisema vijana hao watatu.

Changamoto

Changamoto inayowakumba vijana hao ni ukosefu wa mashine za kutosha za kufanya kazi. Hawajapata hela za kutosha ya kununua kila mashine wanazohitaji katika karakana yao.

“Mahitaji yamekuwa mengi. Huwa tunaweka hakiba kila mwezi ya kujiendeleza kimaisha. Japo hatuja fika katika lengo letu, tunauhakika kuwa mambo yatakuwa shwari Majaliwa,” alisema ‘Obwogo’ ambaye ni mmoja wa vijana hao.

Changamoto nyingine ni kuwa rangi hizo huwaadhuru kiafya. Rangi hujaza kifua hasa unapozitumia bila kuvaa barakoa ama kidude kitakachofunika mdomo na mapua.

Japo kuna changamoto kama hayo, faida wanayopata kutokana na kazi yao ni kubwa.

Wanaeleza kuwa kwa kila gari wanalolipaka rangi, wao hupata faida sio chini ya Sh5,000 kila mmoja. Hivyo biashara yao kuwafaidi kwa kila jambo.

“Tumefanya mengi kupitia kazi hii yetu. Wengine wetu wameoa, kujenga nyumba na kujikimu kupitia kazi hii ya jua kali. Tunafurahia pia kuwa tunawakuza wengi na kuwajengea kiwanda cha ajira,” Joel, mmoja wa vijana hao aliambia Akilimali.

Gari linapoletwa, wao huchukua muda wa siku moja au mbili kabla ya mwenyewe kulikujia likiwa kamilifu.

Kwa siku, wanawezatoa huduma zao kwa watu si chini ya watano.

Wanawahimiza vijana kama wao wanaoishi katika mitaa mbalimbali kujiundia ajira badala ya kujiunga na vikundi visivyofaa.

Wanawahimiza vijana pia kutozingatia kiwango chao cha elimu ila waungane na kujijenga kwa pamoja.

You can share this post!

AKILIMALI: Ndege wa mapambo wanavyompa tonge nono mwalimu...

AKILIMALI: Mfumaji vikapu hodari, mtunzaji mazingira...