Makala

AKILIMALI: Kijana aungama anautambua utamu wa mapapai

December 20th, 2018 2 min read

NA CHARLES ONGADI

PAPAI ni mojawapo ya matunda yanayopendwa sana na watu wa tabaka zote eneo la Pwani na taifa kwa ujumla kutokana na utamu wake.?Kuna aina mbili ya mipapai, Hawai na Mexican ambayo hukuzwa nchini na maeneo mbalimbali duniani ambako kilimo hufanywa.?

Aghalabu wengi hupenda kuteremsha papai au juisi yake muda mfupi baada ya kupata mlo wa kawaida wakati wa mchana au usiku.?Hata hivyo, ni wachache sana hupata nafasi ya kushughulikia kilimo cha papai, wakulima wengi wakikosa mbinu aula ya kupata faida.

Lakini kwa kijana Kadenge Kenga, 25, ambaye ni mkazi wa kijiji cha Magahawani, Bamburi eneoubunge la Kisauni, kilimo cha mipapai ndio tegemeo lake kiuchumi kwa kipindi cha miaka mitatu sasa.

“Nilianza kilimo nikiwa na miaka 18 mara baada ya kukamilisha masomo yangu ya upili na nimeona faida yake,” asema Bw Kenga alipokuwa akizungumza na AkiliMali eneo la Magahawani, Bamburi majuzi.?Kulingana na Bw Kenga, punde baada ya kukamilisha masomo yake ya upili aliamua kuajiriwa katika shamba la Fahim lililoko eneo la Mtwapa kaunti ya Kilifi.

Ni hapa ndipo kijana huyu mkakamavu alijifunza mbinu mbali mbali za kilimo ikiwemo kilimo cha mipapai ambacho hufanywa na wachache sana eneo la Pwani.?Akiwa katika shamba la Fahim, Kenga alijifunza mbinu mbali mbali za kilimo cha aina tofauti ya mboga za kisasa kama Wild Rucula, Parsley, Basil Genovess miongoni mwa nyengine.

Aidha, Kenga anaifichulia AkiliMali kwamba kilimo cha mipapai kinalipa ila kama mkulima ataweza kuzingatia na kufuata masharti yake.?Kipindi cha mavuno Bw Kenga huweza kuvuna kati ya kreti 20 hadi 30 kwa siku ambapo kreti moja hubeba mapapai makubwa 20 wakati papai moja huwauzia wateja wake kwa Sh18.

Wateja wake huwa ni wakazi wa maeneo ya karibu kama Majaoni, Shanzu, Bamburi, Kiembeni na hata Mtwapa ambao humiminika kila asubuhi kununua bidhaa hii.?Pia kuna wafanyabiashara wanaochuuza na wale wa kuuza kwenye vibanda ambao nao hufika kupata bidhaa hii inayopendwa na wengi Pwani.

“Kama mkulima ataweza kufuata barabara masharti ya kilimo cha papai kwa kuitunza vyema basi faida yake ipo,” asema.

Mkulima huyu chipukizi anapanda mipapai aina ya Hawaii na ile ya kienyeji maarufu kama Moyo wa Simba ambayo hupendwa sana na wenyeji hapa.

Kwa mujibu wa Bw Kenga, cha kuzingatia katika kilimo cha mipapai ni jinsi mkulima anavyotayarisha shamba lake kabla ya kupanda mimea yake.?Ili kuvuna mapapai mengi, matamu na yenye afya, ni muhimu kwa mkulima kununua mbegu zake katika duka rasmi lililosajiliwa la kilimo.

Na mara baada ya kuandaa shamba mkulima anahitajika kuchanganya barabara mbolea ya samadi (kinyesi cha kuku, ng’ombe au mbuzi) shambani huku akisubiri miche katika nasari kuwa katika hali nzuri.?Kulingana na Bw Kenga baada ya kipindi cha kati ya wiki mbili na tatu, anahamisha miche yake ya mipapai kutoka kwa nasari hadi shambani.

“Ni muhimu kuzuia mimea kuchomwa na jua kipindi hiki cha upanzi hivyo kila shimo linahitajika kufunikwa kwa mtindo maalum kwa kutumia makuti na wala siyo nyasi ambayo mara nyingi huwa na wadudu hatari,” asimulia Bw Kenga.

Anaongeza kwamba kila baada ya siku mbili anahakikisha amenyunyizia maji mashimo yote yaliyo na mipapai ili kuzuia kunyauka.?Kati ya changamoto zinazomkabili Bw Kenga katika kilimo cha mipapai ni uvamizi wa kila mara wa wadudu waharibifu kama whiteflies.?Hata hivyo, Bw Kenga anahakikisha amejihami kila mara na dawa aina ya Eugio 80ml kuwaangamiza wadudu hao waharibifu.

Anashauri kwamba ni vyema kunyunyizia dawa aina ya CAN ili kuvuna mapapai makubwa, yenye afya na ya kupendeza. Ili mapapai yawe tayari kuvunwa na kupelekwa sokoni, huchukua takribani miezi mitano.?Anawashauri vijana wenzake kukumbatia kilimo badala ya kupoteza muda mwingi wakisaka ajira ambayo pia ni nadra kupatikana.