AKILIMALI: Kijana hodari wa uchoraji aliyejigundua kwenye makao ya watoto alikokulia

AKILIMALI: Kijana hodari wa uchoraji aliyejigundua kwenye makao ya watoto alikokulia

Na CHARLES WASONGA

WASIMAMIZI wa makao ya watoto mayatima na wengine wenye mahitaji maalum, aghalabu, hupenda kuyarembesha kwa aina mbalimbali ya michoro na picha mbalimbali.

Mojawapo ya sababu za kufanya hivyo huwa ni kuwafurahisha watoto hao kusudi wasahau madhila mbalimbali yanayowazonga.

Lakini kwake Gad Wesonga, michoro na picha katika majengo ya Makao ya Watoto ya Virginia Children Home, Nakuru alikolelewa kwa miaka saba baada ya wazazi wake kutalikiana, iliotesha talanta yake ya uchoraji ambayo sasa inamsaidia kuchuma pato.

“Nilivutiwa na michoro ya watu, wanyama na hata ndege, iliyokuwa kwenye kuta za majengo kadha katika makao hayo yaliyonipa hifadhi kwa miaka saba baaada ya wazazi wangu kutengena. Nilitamani kuwa siku moja ningekuwa mchoraji,” anasema.

“Siku moja nilianza kuchora maumbo mbalimbali ya wanyama, kwa kutumia penseli ya kawaida, nikiiga michoro ambayo yalikuwa imechorwa katika kuta za bweni letu. Baada ya muda nilianza kuchora nyuso za watoto wenzangu pale katika Virginia Children Home, na hiyo ikageuka kuwa uraibu wangu,” anaongeza Wesonga mwenye umri wa miaka 25.

Lakini kwa bahati mbaya, anaeleza, hakupata nafasi ya kujifunza rasmi sanaa ya uchoraji kwani hata Shule ya Upili ya Nakuru Day haikuwa inafundisha sanaa ya usanifu (Fine Art) kama somo mahsusi.

Ndoto yake ya kupata mafunzo hayo ilizimwa hata zaidi baada ya Wesonga kukamilisha masomo yake ya shule ya upili kwani mhisani wake, Likwalo Ndeta, alikatiza ufadhili kwake.

“Singeweza kuendelea na masomo katika chuo chochote baada ya mwaka wa 2015 kwa kukosa mfadhili. Hii ni licha ya kwamba nilipata gredi ya wastani ya C+ katika Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE), gredi ambayo ingeniwezesha kujiunga na chuo kizuri kwa elimu ya juu,” Wesonga anaeleza.

Hapo ndipo aliamua kuyoyomea jijini Nairobi kusaka vibarua kujikimu kimaisha. Alitua katika Kawangware na akaanza kusaka kazi za sulubu katika maeneo ya mjengo angalau kujikimu kimaisha baada ya kupoteza matumaini ya kuendelea na masomo kwa kukosa mfadhili.

“Nilifanya kazi katika mitaa ya Lavington, Kileleshwa, Kangemi na hadi mtaa wa Umoja,” Wesonga akasema.

Lakini siasa zilipoanza kunoga mapema 2017, kijana huyo anasema aliamua kurejelea uchoraji, haswa nyakati za jioni.

“Nilikuwa nikichora nyuso za wanasiasa kama vile aliyekuwa Gavana wa Nairobi Evans Kidero, Mbunge wa Dagoretti Kaskazini Simba Arati na Mbunge Mwakilishi wa Nairobi Esther Passaris na wengine. Lakini nilipojitokeza na michoro hiyo kwenye mikutano yao ya kampeni, ili angalau niwauzie, baadhi ya wasaidizi wao walidhani ilikuwa zawadi. Hawakunilipa chochote. Lakini wengine wangenionea huruma na kuniachia hela chache,” Wesonga anaeleza.

Lakini msanii huyo milango ya baraka ilianza kumfungukia mnamo 2018 alipoanza kuweka kazi zake katika mitandao ya kijamii ya Facebook na Twitter.

“Oda ya kwanza niliyopata mitandaoni ilitoka kwa mwanafunzi wa kike wa Chuo Kikuu cha Kenyatta. Alinitumia picha yake na nikaichora kwa makini zaidi na akavutiwa na kazi. Nilimpelekea kazi yake pale katika bewa kuu na akanilipa Sh2,000. Nilifurahi ajabu!” Wesonga akaeleza.

Mapema 2019 kijana huyo alipata nafasi ya kujifunza kazi ya kinyozi katika kituo cha Fresh Cut Foundation kilichoko mtaa wa Kilimani, Nairobi. Alihitimu baada ya miezi sita.

“Baadaye, niliajiriwa katika mojawapo ya vinyozi vinavyomilikiwa na wakfu huo katika mtaa hapa Kilimani. Kwa hivyo, tangu mapema mwaka jana, nimekuwa nifanya kazi ya kinyozi mchana kisha kufanya kazi yangu ya uchoraji baada ya kazi au hata usiku,” anasema Bw Wesonga.

Anasema wengi wa wateja wake ni watu binafsi wa matabaka mbalimbali ambao hukumbana na kazi zake mitandaoni. Bei ya michoro yake hutegemea mahitaji ya wateja wake.

Changamoto anayokumbana nayo katika kazi hii ni kwamba kuna baadhi ya watu ambao hawathamini kazi ya sanaa, kiasi kwamba hutaka kulipishwa pesa kidogo kwa “mchoro wenye gharama kubwa”

“Hatimaye ndoto yangu ni kuanzisha studio ya sanaa ili niweze kuwafundisha vijana kazi hii,” Wesonga anasema.

You can share this post!

Spurs watinga hatua ya 16-bora ya Europa League baada ya...

AKILIMALI: Natija itokanayo na kujua mahitaji ya ufugaji...