Makala

AKILIMALI: Kilimo cha kabichi nyekundu na tija zake kiafya na kimapato

April 12th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

MAONYESHO ya kilimo yaliyofanyika katika shamba la kilimo la Mariira, maarufu kama Mariira Farm kaunti ndogo ya Kigumo, Murang’a, Machi 8 na Machi 9, 2019, yalikuwa yenye manufaa tele kwa wakulima.

Yalileta pamoja wakulima mbalimbali kutoka dira tofauti za nchi, ambapo walipata fursa kutangamana na wataalamu wa masuala ya kilimo pamoja na wakulima waliobobea.

Katika jukwaa la kampuni ya Safari Seeds, mafunzo ya mboga yalivutia wengi. Ingawa rangi yake ni ya zambarau, kila mkulima alikuwa na kiu cha kutaka kujua kuhusu ukuzaji wa kabichi nyekundu, Super Red F1.

Ni aina ya kabichi iliyosheheni Vitamini C na K. Wataalamu wa masuala ya afya wanahoji Super Red F1 ina zaidi ya madini 36, yanayoaminika kukabiliana na ugonjwa hatari wa Saratani.

Japo si wakulima wengi wanaolima aina hii ya kabichi, Caroline Njeri afisa na mtaalamu wa kilimo Safari Seeds anasema ni mojawapo ya mboga rahisi mno kukuza. Sawa na kabichi za kijani, Super Red F1 zinastawi maeneo yenye baridi. Ni muhimu kutaja kwamba hazina kikwazo cha kuchagua udongo, kwani kilimo chake kinafanikishwa katika udongo tifutifu, wa kufinyanga na hata changarawe.

Hata hivyo, Bi Njeri anahimiza umuhimu wa kujua kiwango cha asidi cha udongo. Kwa kawaida, mboga zinastawi katika udongo wenye asidi, pH kati ya 6.0-7.0

“Shamba lako linahitaji kukaguliwa ili kujua aina ya udongo kabla kuanza kulima mara ya kwanza. Endapo haujaafikia vigezo vipasavyo, utashauriwa namna ya kuutibu,” aeleza mtaalamu huyu.

Anaongeza kusema kuwa kinachoangusha wengi katika sekta ya kilimo ni kutozingatia masuala muhimu kama kujua asidi na alkalini ya udongo.

Upanzi

Kulingana na mdau huyu ni kwamba taratibu za kukuza kabichi nyekundu ni sawa na za kijani. Ekari moja inahitaji gramu 100 za mbegu, ambapo inasitiri karibu kabichi 20,000. Safari Seeds inauza gramu moja Sh120, gramu 5 Sh500 na gramu 10 Sh900.

Miche ya Super Red F1 huchukua muda wa mwezi mmoja kitaluni kuwa tayari kwa upanzi.

Shamba linapolimwa, Njeri anasema nafasi ya shimo hadi lingine iwe sentimita 45. Mstari wa mashimo hadi mwingine, uwe kati ya sentimita 60-75.

Caroline Njeri, afisa na mtaalamu wa kilimo Safari Seeds akieleza kuhusu kilimo cha kabichi nyekundu, Super Red F1. Picha/ Sammy Waweru

Kabichi huhitaji madini mengi ya Nitrojini na Potassium, hivyo basi mkulima anahimizwa kuzingatia hili katika upanzi na utunzaji wake.

Aidha, wakati wa kuhamishia miche shambani, kitalu kinapaswa kumwagiliwa maji saa tatu au nne kabla ya shughuli hiyo kuanza. Ing’olewe kwa umakinifu wa juu, kwa kuwa miche ni mimea midogo ambayo haijakomaa.

Udongo wa juu, uliotolewa shimoni uchanganywe sawasawa na mbolea, hai au fatalaiza. Mchanganyiko huo urejeshwe shimoni, kisha miche ipandwe na kunyunyiziwa maji.

“Tunza mikabichi kwa maji, na fatalaiza zenye madini ya Nitrojini na Potassium,” anashauri Njeri.

Lucy Wambui Gathungu, mmoja wa wakulima wa mboga Nyeri, anasema palizi katika kabichi dhidi ya makwekwe ni jambo muhimu kutilia maanani.

“Kabichi inahitaji chakula cha kutosha ili kuunda mboga. Makwekwe yanapomea, yatailetea ushindani mkali wa mbolea na maji,” anaeleza.

Ili kudhibiti makwekwe, mkulima anaweza kuweka nyasi za boji katika nafasi zilizoko kati ya kabichi. Boji huzuia uvukizi wa maji, hasa msimu wa juakali au kiangazi.

Wakati wa mahojiano, Bi Caroline Njeri wa Safari Seeds alisema Super Red F1 ni nadra kuathiriwa na ugonjwa aina ya Black Rot unaoshuhudiwa kwa mboga. Ni changamoto inayofanya majani kukauka na hatimaye kukauka.

“Aina hii ya kabichi inastahimili magonjwa mengi ya mboga, ikilinganishwa zile za kijani. Pia, wadudu huiepuka kwa sababu ya maumbile yake, hawapendi rangi,” adokeza Njeri.

Hata hivyo, wiki kadhaa kabla ya mavuno mkulima anashauriwa kupulizia dawa dhidi ya vidukari na viwavi. Diamond Back Moth, ni aina nyingine ya mdudu anayeshambulia mboga.

Kabichi huwa tayari kwa mavuno miezi mitatu baada ya upanzi. Aghalabu, kabichi hii nyekundu huwa na wastani wa kilo 2, japo kuna zingine kubwa zenye uzani wa hadi kilo 4.

Super Red F1, moja haipungui Sh40.

“Hugharimu hadi Sh100,” aeleza Njeri.