Makala

AKILIMALI: 'Kijishamba cha ghorofa' kinamfaa mkulima wa mjini

December 3rd, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

UHABA wa vipande vya ardhi vilivyotengwa kwa ajili ya kilimo mijini ni suala ambalo ni bayana katika maeneo mengi nchini.

Upungufu huo unachangiwa na ongezeko la watu, hasa kufuatia uhamiaji wa mijini kutoka mashambani.

Wengi wanahamia mijini ili kutafuta ajira ili kujiendeleza kimaisha.

Vilevile, kuna walioko mijini kwa minajili ya kuzima kiu cha kupata masomo, hususan vijana waliopata mwaliko wa kujiunga na taasisi za elimu ya juu.

Mengi ya mashamba, wamiliki wanayageuza kuwa ploti za majengo ya kukodi.

Huku idadi ya watu maeneo ya mijini ikiendelea kuongezeka, ndivyo upungufu wa mashamba unaizi kushuhudiwa.

Sharti wanaoishi humo wabugie cha kutuliza matumbo. Maeneo ya mashambani ndio tegemeo katika uzalishaji wa chakula, hasa mazao mbichi ya kilimo.

Nyakati zingine, kufuatia mfumuko wa bei ya bidhaa za kula, wenye mapato ya chini hupitia wakati mgumu kulisha familia au jamaa zao.

Wakati akilea wanawe, ambao sasa ni watu wazima, Elizabeth Karungari alikumbana na changamoto za aina hiyo.

Hata hivyo, mama huyo anasema alikuwa akitumia kipande chake cha ardhi chenye ukubwa wa robo ekari, kiungani mwa jiji la Nairobi, kupunguza gharama.

Sehemu moja ya ploti yake ikiwa imejengwa nyumba, iliyosalia ameigeuza uga wa kilimo na ufugaji wa kuku.

“Gharama ya mboga, vitunguu na pia ndizi nimeipunguza kwa kiasi kikubwa,” Elizabeth anaelezea.

Ploti yake pia ina miti miwili ya maembe, matunda ambayo msimu wa mavuno humpa mapato ya ziada.

Isitoshe, mbolea anayotoa kwenye kizimba chake cha kuku ndiyo anaitumia kunawirisha mazao ya kilimo.

“Kwangu mayai na nyama ya kuku, hayakosi,” mama huyo anasema.

Kulingana na Salome Muthoni, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kilimo, licha ya uhaba wa mashamba mijini, wakazi wanaweza kutumia nafasi ndogo waliyo nayo kulima mimea inayochukua muda mfupi kuzalisha.

“Mazao mbichi kama vile mboga aina ya sukuma wiki, spinachi, mboga tofauti za kienyeji, nyanya na pia vitunguu, yanaweza kukuzwa kwenye ploti,” Salome anaeleza.

Mdau huyo anasema hayahitaji nafasi kubwa ya ardhi “ila ile finyu iliyopo”.

Mfano, anasema mpangaji kwa idhini ya landilodi anaweza kutengeneza ‘shamba’ lenye umbo la duara (conical-shape), na lenye ngazi kuenda juu, kwa kutumia karatasi ngumu za plastiki zinazotumika katika kilimo.

“Umbo hilo likitiwa udongo na pia mbolea, litakukuzia mboga aina nyingi,” Salome anasema.

Mbali na mboga, umbo hilo pia limekumbatiwa kuzalisha matunda kama vile stroberi, katika eneo tambarare na pia kwenye kivungulio (green house).

Manufaa ya mfumo huo wa kisasa katika kuendeleza shughuli za kilimo, ni kwamba matumizi ya maji huwa yamepunguzwa kwa kiwango kikubwa.

“Kwenye mashina ya mimea, weka na utandaze nyasi zilizokauka (nyasi za boji) ili kuzuia uvukizi wa maji,” mtaalamu Salome anashauri.

Mkulima anayejitambua kama Paul, kutoka Kiambu, amekumbatia mfumo huo na anasema hivi karibuni anapania kuugeuza kuwa kilimo-biashara.

“Nimegundua nafasi inayotumika ni haba, na ni bora kwa wanaoishi maeneo ya mijini,” anasema.

Ni mfumo ambao ukikumbatiwa na wenyeji wa mijini, gharama ya ununuzi wa chakula hasa mazao mbichi ya kilimo yanayochukua muda mfupi kuzalisha, itapunguza kwa asilimia kubwa.