Makala

AKILIMALI: Kilimo cha mananasi kimemjenga hadi sasa ana trekta ya kukodisha

November 19th, 2020 3 min read

Na PETER CHANGTOEK

WILSON Baya, 35, anashika nanasi lililoiva shambani kwake, katika eneo la Viriko, Magarini, Kaunti ya Kilifi, huku akiendelea kuikagua mimea yake ya minanasi.

Amekuwa akiikuza minanasi katika eneo hilo tangu mwaka 2012. Alianza kwa kulitumia shamba ekari tano, lakini kwa sasa, hulitumia shamba ekari 48, na anaazimia kulituma shamba lake lote, ambalo ni ekari 86, kwa shughuli hiyo.

Hapo awali, alikuwa akifanya biashara ya kuuza ardhi, lakini alipokuwa katika harakati hiyo, akaona shughuli ya ukuzaji wa minanasi ikiendelezwa katika mashamba kadhaa, na akafurahishwa nayo.

Hapo mbeleni alikuwa akifanya shughuli ya ukuzaji wa mimea kama vile minyanya, sukumawiki, mahindi, migomba, miongoni mwa mimea mingineyo. Hata hivyo, alipogundua kuwa minanasi ina faida tele, akaamua kujitosa kwenye zaraa hiyo.

“Nilinunua shamba ekari 86 kwa Sh5,000 kwa kila ekari. Wakati huo, nilikuwa nikifikiria ninaibiwa, baadaye nikaona halina maneno. Wakati huo, nilianza kwa ekari tano. Nilifyeka msitu, nikachoma, nikalima na nikawatafuta wafanyakazi na nikawalipa kunipandia minanasi,” asema mkulima huyo.

Aliipanda minanasi 8,000, ambayo aliinunua kwa bei ya Sh6 kila mmoja; ambapo alitumia Sh48,000 kwa jumla, kwa ekari moja ya shamba. Kwa jumla, alitumia Sh240,000 kuinunua minanasi aliyoipanda kwa shamba ekari tano.

“Nilinunua shamba mnamo Juni, 2012, na ilipofika Agosti, nilikuwa nimeshapanda minanasi. Mnamo Juni 2013, wakati nilipokuwa nimeuza mananasi, nikapata pesa na nikafyeka shamba ekari 10 kwa msitu huo. Kwa bahati nzuri, nilikuwa na mbegu za ile mimea ya kwanza, nikapanda kule kwingine, zikawa ekari15,” asimulia mkulima huyo, ambaye ni baba wa watoto wawili.

Anasema kwamba aliuza nanasi moja kwa Sh50, kwa kila ekari, ambapo alipata takribani Sh400,000 kutoka kwa kila ekari, na jumla ya takribani Sh2 milioni kwa ekari tano.

Mkulima huyo anasema kwamba minanasi yake huchukua muda wa mwaka mmoja ili ianze kuzaa matunda.

“Nilisubiri tena mwaka mmoja ili ianze kuzaa. Ile ya kwanza ikawa inachukua miezi minne kuzaa,” adokeza Baya.

Mnamo mwezi Juni, 2014, aliipanda minanasi mingine kwa shamba ekari 10, na akawa na jumla ya ekari 25.

“Kwa kuwa hatununui mbegu kutoka madukani, siwezi nikasema aina ya minanasi tunayoikuza. Lakini hapa, tunaitambua kwa jina la mwanazi. Wasomi hapa wameanza kuipa jina Magarini sweet pineapple,” asema mkulima huyo, ambaye ni mzawa wa kijiji cha Masindeni.

Kwa jumla, Baya ana mimea ya minanasi zaidi ya laki tatu, katika shamba ekari 48. Anasema kuwa hazitumii mbolea zozote au kunyunyizia dawa kwa minanasi yake.Anaongeza kuwa, minanasi huwa haina kazi kubwa mno.

“Sisi huondoa magugu tu mara mbili kwa mwaka mmoja, baada ya mvua,” adokeza.

Kwa mujibu wa Baya ni kwamba, hajawahi kuzipitia changamoto katika ukuzaji wa minanasi. Hata hivyo, wadudu kama vile majongoo hutoboa matundu kwa mananasi yaliyoiva.

“Sina tatizo la kupata wateja, kwa sababu wale wanaotaka huja shambani na kuchukua kwa magari yao. Wafanyakazi wangu huhesabu, nami hungojea kuhesabu hela tu,” afichua mkulima huyo, akiongeza kuwa.

Baya anasema kwamba wateja wake hutoka Malindi, Kongowea (Mombasa) na Kilifi. Aidha, huwauzia wateja walioko katika sehemu nyinginezo.

Mbali na kuyauza mananasi yaliyoiva, yeye pia huiuza miche kwa Sh10 kila mmoja, na wakati wa mahojiano, alikuwa ameiuza miche 30,000.

Ana wafanyakazi watano, ambapo baadhi yao huitwa tu wakati ambapo pana shughuli nyingi shambani.

Mkulima huyo anafichua kuwa, mchanga katika eneo hilo ni mwafaka kwa ukuzaji wa minanasi.

Baya anasema kuwa, kutokana na mauzo ya mazao ya mananasi, ameinunua trekta mpya yenye thamani ya Sh2.4 milioni, ambayo hutumia kuwalimia wakulima wengine mashamba kwa ada fulani.

“Ninamshukuru Mungu ninaishi maisha mazuri. Mananasi yana faida,” afichua mkulima huyo, ambaye anasema kuwa cOVID-19 imeathiri biashara hiyo, japo si sana.

Mbali na ukuzaji wa minanasi, Baya pia huikuza mimea mingine katika shamba tofauti, kama vile mitikitimaji, migomba, na sukumawiki, kati ya mimea mingineyo.

Mkulima huyo anafichua kwamba, ana mipango ya kukiendeleza kilimo hicho katika shamba lake lote, ambalo ni ekari 86, ili kupata faida zaidi.