Makala

AKILIMALI: Kilimo cha ndizi ni rahisi, mapato ni mazuri

May 22nd, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

MAENEO mengi nchini Kenya yana uwezo wa kuzalisha ndizi kwa sababu ya hali yake bora ya hewa na udongo.

Meru, Kisii, Nyeri, Nyamira, Kirinyaga, Kakamega, Embu, Bungoma na Murang’a ndizo kaunti tajika katika ukuzaji wa ndizi.

Maeneo mengine yanayotambulika ni Kerio Valley, Kericho, Makueni na Baringo.

Kulingana na wataalamu wa kilimo, zao hili linastawi katika maeneo yenye joto la wastani na kupokea mvua ya kutosha. James Macharia, mtaalamu wa kilimo Murang’a na ambaye pia ni mkuzaji wa zao hili, anasema ndizi hunawiri maeneo yanayopokea kiwango cha mvua milimita 2,500 au zaidi, kila mwaka.

“Kiwango cha joto kinapaswa kuwa nyuzi 27 sentigredi,” anasema Bw Macharia. Aidha, maeneo hayo yawe yenye urefu wa kati ya mita 0 hadi mita 1800, juu ya ufuo wa bahari (altitude).

Kuna aina mbalimbali ya ndizi, za upishi; Ng’ombe, Nusu Ng’ombe na za kijani zenye asili ya Uganda Green. Zinazokua maeneo kame; William, Grand Naine, Giant Cavedish, Gros Michel maarufu kama Kampala na Apple kwa jina lingine Kasukari.

Ni muhimu kutaja kuwa ndizi pia zinaweza kukuzwa kwa kutumia mfumo wa kunyunyizia maji mashamba (irrigation).

Kulingana na wakulima waliofanikisha kilimo cha ndizi, ni kwamba maji, mbolea na kupogoa matawi yanayochipuka ndivyo vigezo muhimu. Migomba, ambayo ni mbegu, ipandwapo huchukua karibu siku 340 ili kuanza kuzalisha na kuvuna ndizi.

“Msimu wa kiangazi, migomba huhitaji kunyunyiziwa maji mara moja au mbili kwa wiki,” aeleza Bi Mary Wairimu, mkulima Kirinyaga.

Taratibu za kupanda

Miaka ya awali, wakulima walikuwa wakitumia mbegu asili yaani migomba katika uzalishaji. Hata hivyo, muda unavyozidi kusonga teknolojia inaendelea kukua na kuvumbua mbinu za kisasa kunogesha sekta ya kilimo.

Watafiti kupitia taasisi husika za kilimo na ufugaji nchini, wanahimiza wanazaraa kutumia mbegu za kisasa na zilizoimarika kuzalisha ndizi, maarufu kama ‘tissue culture bananas’. Ni mbegu zilizotafitiwa, na kubainika kuwa na uwezo wa kudhibiti athari za magonjwa na wadudu wanaoshambulia matunda.

Mkungu wa ndizi. Picha/ Sammy Waweru

Ekari moja inasitiri wastani wa mbegu 540, moja ikikadiriwa kugharimu Sh120.

Kitaalamu, mashimo ya kupanda yanapaswa kuwa na urefu wa kati ya futi 1.5 hadi futi 2 kuenda chini, kila moja. Upana uwe futi 1.5.

“Nafasi ya shimo moja hadi lingine iwe kati ya mita 2.5 hadi mita 3,” aeleza Bw James Macharia, ambaye ni mtaalamu wa kilimo.

Kulingana na mdau huyu ni kwamba mkulima anapaswa kutia mbolea kwenye mashimo, ikifuatwa na udongo, japo lisijazwe. Mbegu zipandwe, kisha zimwagiliwe maji.

Siri za kufanikisha kilimo cha ndizi ni maji, mbolea na kupogoa matawi. “Nafasi shimo iliyosalia juu ni ya kutunza migomba kwa mbolea ya mifugo au kuku, ambayo huongeza kiwango cha mazao,” asema Bw Macharia.

Mgomba unapotoa migomba midogo kandokando, unahimizwa kuipogoa isalia na kati ya mitatu hadi mitano. Bw Macharia anasema hatua hii huwezesha iliyosalia kuzalisha ndizi kubwa bora na zenye hadhi ya juu, kwa sababu haitakuwa na ushindani wa chakula ambacho ni maji na mbolea.

Palizi pia ni muhimu kwa sababu hudhibiti usambaaji wa wadudu. Makwekwe pia huleta ushindani wa chakula kwa migomba.

Wadudu wanaoshambulia ndizi ni; Nematode na Fukusi. Magonjwa kwa ndizi ni Sigatoka, Fusarium Wilt na Bacterial Wilt.

Virusi vya mimea pia husababisha magonjwa kama banana bunchy top na banana streak. Mkulima anahimizwa kutafuta ushauri kutoka kwa watalaamu wa kilimo au maduka ya kuuza dawa za mimea, ili kukabiliana na changamoto za wadudu na magonjwa.

Kifungu kimoja cha ndizi mbichi kilichovunwa hugharimu kati ya Sh300-350 bei ya kijumla. Maeneo ya mijini, bei hupanda hadi Sh500.

Migomba huzalisha ndizi karibu kipindi cha miaka 10 mfululizo, kabla ya kuing’oa ili kupanda mingine.

Ni muhimu wakulima kuwa na njia mbadala za kuongeza ubora katika mazao wanayozalisha (value addition) ili kuongeza mapato. Ndizi pia husagwa kuwa unga wa kupika uji na ugali. Zilizoiva, huunda sharubati kwa kuchanganya na matunda mengine.