Makala

AKILIMALI: Kilimo cha njugu humletea hadi Sh200,000

May 2nd, 2019 2 min read

Na FRANCIS MUREITHI

Mkulima mahiri wa njugu karanga, Bw Daniel Kiptoo anatazama njugu alizovuna katika katandogo ya Chepsirei, Kaunti ya Elgeyo Marakwet huku akitabasamu na mwingi wa matumaini.

Ana kila sababu ya kufurahia kwani mavuno yake yameongezeka maradufu tangu aanze kupanda mbegu za njugu ambazo zinastahimili ukame aina ya Valencia na kuvuna magunia 15 ya kilo 90 kutoka shamba la ekari moja analolima

Na kwa kuwa gunia moja la njugu huuzwa kwa kati ya Sh10, 000 na Sh15, 000, hii inamaanisha Bw Kiptoo hujiwekea kibindoni kati ya Sh100, 000 hadi Sh225, 000 baada ya kila miezi mitatu.

“Kabla sijaanza kutumia mbegu hizi nilikuwa nahangaika mno shambani kupata angalau magunia matano ya njugu; kisa na maana nilikuwa natumia mbegu ambazo hazikuwa zimeidhinishwa ambazo hapa Chepsiret zinajulikana kama Cheplambus ambazo hukomaa baada ya miezi sita. Hata hivyo mbegu hizi mpya za Valencia ni nzuri kwani hukomaa katika kipindi cha miezi miwili hadi mitatu na hutoa mavuno mengi,” anasema Bw Kiptoo.

Mbali na mbegu hizi za Valancia, wakulima wa Chepsirei hupanda mbegu aina ya Spanish miongoni mwa mbegu nyingine ambazo zimetenegnezwa na taasisi ya utafiti ya kimataifa ya kutengeneza mbegu za maeneo kavu na yasiyo kavu sana (ICRISAT) wakishirikiana na Chuo Kikuu cha Egerton na ufadhili kutoka Marekani kupitia kitengo cha cha kusaidia maendeleo ya kimataifa cha USAID.

“Wakati mavuno yameshamiri mbegu hizi mpya na za kisasa huweza kutoa kati ya magunia 20 hadi 25 ya njugu ambazo hazijatolewa maganda mradi tu mkulima anazigatia mawaidha ya watalamu. Mbegu hizi hutoa mazao mengi katika maeneo kavu na yenye mvua chache kama vile Kerio Valley ambapo wakulima hupata mavuno finyu katika mazao mengine,” anasema Profesa Paul Kimurto wa Egerton ambaye ni mtaalamu wa mazao.

Aidha, Profesa Kimurto anazidi kufichua kuwa mbegu hizi pia zaweza kupandwa katika maeneo kavu ya Nyanza Kusini, Magharibi mwa Kenya na maeneo ya Mashariki mwa kama vile Kitui,Machakos na Makueni.

Wakulima wa eneo hili mbali na kupokea mbegu pia hupokea mafunzo ya kisasa ya upanzi wa njugu na kupelekea kuinua hali ya kilimo hiki kinacho zidi kuwavutia wakulima wengi kutokana na faida kubwa wanayopata.

“Tangu nianze kupanda mbegu hizi za Valencia nimepata mafunzo kemkem na leo hii katika kila ekari nakuza njugu mimi hupanda kilo 30 badala ya kilo 25 nilizokuwa napanda kabla ya kupokea mafunzo haya,” anasema Bw Kiptoo.

Kadhalika, Bw Kiptoo anakiri kuwa ili mkulima apate mazao mengi, utayarishaji mapema wa shamba kabla ya mvua ni muhimu sana kwani huzuia kusambaa kwa wadudu waharibifu kama vile mchwa ambao huadhiri mizizi ya njugu.

Bw Kiptoo anasema pia kabla ya kulima shamba lake yeye hukagua udongo wake ili aweze kujua ni madini yapi njugu zake zinahitaji na pia ukaguzi huuu humwezesha kugundua ikiwa udongo uko na maradhi.

Hata hivyo, kilimo cha njugu sio mteremko na kama vile Bw Kiptoo anafichua kilimo hiki kina panda na shuka zake. ?Mkulima huyu anasema moja ya gharama kubwa ni kupata trakta ya kulima yenye kulipisha gharama ya chini.?Anasema wakulima wengi hulima kwa mikono kutokana na gharama ya kulipa trakta ambayo huwa kati ya Sh3,000 hadi Sh5,000.