Makala

KWAHERI UTAPIAMLO: Majani ya viazi vitamu yanavyovutia watoto shuleni

June 15th, 2018 3 min read

Na FAUSTINE NGILA

JE, wajua kwamba majani ya viazi vitamu yanaweza kupikwa na kugeuzwa mboga yenye nguvu mwilini mara nne kuliko maziwa?

Akilimali ilisafiri hadi kaunti ya Makueni, eneo la Emali ambako kilimo cha mmea huu kinaendeshwa kwa jitihada kuu kwa lengo la kuwalisha wanafunzi wa chekechea na kuwafaidi wakazi kiuchumi.

Lakini si majani ya kila aina ya viazi vitamu yanaweza kupikwa na kuliwa. Meneja Msimamizi wa shirika la Child Fund katika kaunti za Ukambani, Bw Ancelim Gituma anasema kuwa kuna aina fulani ya mmea huu ambayo imependekezwa na wanasayansi kutumika katika mapishi ya vitoweo.

“Aina ya viazi vitamu tunayoipanda hapa ni Orange Fleshed. Aina hii ina nguvu mara nne mwilini kuliko maziwa ya kawaida. Tulipata mbegu zake kutoka kwa Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo nchini (KARLO), tawi la Kakamega,” anaelezea mtaalamu huyu.

Mradi huu ulianzishwa mnamo 2014 kufuatia ushirikiano kati ya Child Fund, Chuo Kikuu cha Kenyatta na Cho Kikuu cha Otago nchini New Zealand.

Baada ya kufanyia utafiti sampuli za damu za watoto katika kaunti ya Makueni na Kajiado, waling’amua kuwa walikumbwa na utapiamlo. Shirika hili liliweka mikakati ya kubadilisha hali hiyo na kuhakikishia wazazi lishe bora.

“Baada ya utafiti, tuliamua kuihamasisha jamii kuhusu kilimo cha viazi vitamu aina ya Orange Fleshed ambayo hatimaye tulifanikiwa kuwashawishi kukuza ili kutokomeza baa la njaa kwa watoto wa umri wa kati ya mwaka mmoja na sita,” anasimulia Afisa Msimamizi wa mradi huo Bw Maclean Egesa.

Wapishi wawapakulia watoto wa chekechea mseto wa githeri, viazi vitamu aina ya Orange Fleshly na majani yake yaliyokaangwa katika Shule ya Msingi ya Emali, kaunti ya Makueni mnamo Februari 8, 2018. Wataalamu wamethibitisha kuwa lishe hii ina nguvu mara nne mwilini kuliko maziwa. Picha/ Faustine Ngila.

Baada ya uhamasisho, waliunda kikundi cha watu 20, wanawake 17 na wanaume 3 ambao wameshirikishwa katika mradi huo wa lishe bora.

Waliingia kwa mkataba na usimamizi wa Shule ya Msingi ya Emali, ambao ulikubali kuwapa kipande cha ardhi ndani ya shule kukuza zao hilo huku shule ikinufaika na lishe ya aina yake bila malipo.

Kilimo cha mmea huu huchukua miezi mitatu na hakihitaji maji mengi kwa kuwa aina hii ya viazi vitamu inastahimili kiangazi. Ni mmea usiopatwa na magonjwa wala kuvamiwa na wadudu kirahisi. Baadhi ya viazi vina uzani wa kilo moja hadi tatu.

“Tulianza kwa kuchimba bwawa la maji lenye kina cha mita 200 ili kuwezesha unyunyiziaji wa maji wa mimea wakati wa ukame na kufanya kilimo nyakati zote,” anasema Bw Simon Kiseli, afisa wa lishe bora katika shirika la Child Fund.

Anachohitajika mkulima ili kuanzisha kilimo hiki ni shamba lenye mchanga laini pamoja na kuwa karibu na mto au bwawa. Anaweza kutumia mfumo wa mabomba ya chini ya mchanga kunyunyizia maji.

Baadhi ya wanachama wa kikundi cha wakulima cha Emali waonyesha viazi vitamu aina ya Orange Fleshly baada ya kuvuna katika shamba la Shule ya Msingi ya Emali, kaunti ya Makueni mnamo Februari 8, 2018. Picha/ Faustine Ngila.

Viazi hivi hulishwa wanafunzi 107 wa shule hiyo, mpango ambao umewavutia wazazi wengi na kuwasukuma kuwahamishia watoto wao katika shule hiyo.

“Wazazi wengi hasa waliokuwa wamewapeleka watoto wao katika shule za kibinafsi walilazimika kuwaleta kwa shule hii baada ya kushuhudia afya njema ya watoto wa hapa ikilinganishwa na wale wa shule zingine,” anasema mwenyekiti wa kikundi cha Emali, Bi Elizabeth Nduto.

Bw Egesa anelezea kuwa aina hii ya viazi vitamu ina virutubisho kadha muhimu mwilini vikiwemo Vitamini A, C na proteni.

Wanafunzi hulishwa mseto mtamu wa githeri, viazi vitamu na majani yake katika vipimo vya kisayansi.

“Kuna kipimo fulani ambacho mtoto hafai kupita kwa kuwa viazi hivi na majani yake vina nguvu nyingi mwilini,” anasema Bw Cyprian Muriuki, mratibu wa mradi huo, anayeongezea kuwa wazazi na wapishi wote wamepokea mafunzo kuhusu vipimo hivyo.

Kila kilimo kina changamoto zake na Bw Egesa anakiri kuwa wakulima wa shamba hili la ekari 2.2 huhangaishwa na chindi (squirrels) ambao hukatakata mabomba ya maji yanayotumika kunyunyizia maji mimea.

“Wakati mwingine umeme hupotea na hivyo kutuzuia kupiga maji kwenye bwawa. Pia kukikauka sana, kiwango cha maji kwenye bwawa hupungua sana na kufika kina ambacho hakiwezi kufikiwa na mashine,” anasema Bi Nduto.

Jamii ya eneo la Emali imevalia njuga kilimo cha viazi hivi kwa kuwa vina vitamini na nguvu mwilini kuliko sukumawiki, huku wazazi wengi sasa wakikosa sababu ya kutowapeleka watoto shuleni. Picha/ Faustine Ngila

Wakulima hawa wamefundishwa jinsi ya kukabiliana na wadudu kwa kutia mchanga dawa ya kuwaua ili kuhakikisha mavuno hayana magonjwa kabla ya kupikwa.

Kando na kuwalisha wanafunzi, kilimo hiki kimewanufaisha wanachama hawa hasa katika ulipaji wa karo ya wanafunzi wao walio shule za upili. Hii ni baada ya kuuza viazi vitamu vya ziada sokoni na kuhifadhi pesa hizo.

Bi Esther Mutiso ambaye ni mwanachama anasema kuwa mradi huo umewafungua macho na kuweza kulipia familia zao bima ya NHIF pamoja na kuhifadhi pesa kwa chama.

“Mtoto wangu alikuwa na ugonjwa wa bato (ringworms) lakini nilipomleta kwa shule hii, ulitoweka kama umande,” anasema.

Wazazi 79 wenye watoto katik shule hii tayari wameaznisha kilimo cha aina hii ya viazi vitamu baada ya kutambua manufaa yake.

Kwa sasa jamii ya eneo la Emali imevalia njuga kilimo cha viazi hivi kwa kuwa vina vitamini na nguvu mwilini kuliko sukumawiki, huku wazazi wengi sasa wakikosa sababu ya kutowapeleka watoto shuleni.