AKILIMALI: Kilimohai ni muhimu katika kuzuia magonjwa hatari

AKILIMALI: Kilimohai ni muhimu katika kuzuia magonjwa hatari

Na SAMMY WAWERU

KWA zaidi ya miaka mitano, Simon Wagura amekuwa katika mstari wa mbele kuhamasisha umuhimu wa kukumbatia mfumo wa kilimohai katika uzalishaji wa mazao.

Kinachomuatua moyo zaidi ni kuona au kusikia watu wakiugua magonjwa yanayodaiwa kuhusishwa na lishe ilhali yanaweza kuzuilika.

Kulingana na Bw Wagura, changamoto za aina hiyo zitadhibitiwa iwapo kila mkulima ataitikia kukumbatia kilimo asilia.

Huu ni mfumo ambapo mkulima anajaribu kadri awezavyo kuepuka matumizi ya kemikali katika kukuza mimea.

Hii ina maana kuwa mbolea inayopaswa kutumika iwe hai kama vile ya mifugo, ndege na mboji – kuchanganya mbolea hiyo na majani na matawi. Hali kadhalika, mkulima anahimizwa kutumia fatalaiza isiyo na kemikali.

Kulingana na Wagura ambaye mbali na kuwa mwanazaraa wa aina yake, ni mtaalamu wa masuala ya kilimo, athari za wadudu na magonjwa hazikosi kushuhudiwa na kwamba dawa dhidi yake isiwe yenye kemikali.

“Katika mfumo wa kilimohai tunapendekeza kudhibiti wadudu ila si kuwaua asilimia 100,” anasema Bw Wagura.

Mdau huyu anasema pembejeo; mbolea na dawa, zinapaswa kuwa sahibu wa karibu wa mazingira kwa kuyahifadhi.

“Zitangamane na kuhifadhi wanyama wanaoishi kwenye udongo,” anaeleza.

Upanzi wa aina moja ya mmea au iliyoko katika familia moja kwa muda mrefu, unalaumiwa kuchangia kuongezeka kwa wadudu na magonjwa shambani.

Hili huchochea mkulima kutumia kemikali kukabiliana na changamoto hiyo, na kwa mujibu wa maelezo ya Bw Wagura, kando na udongo kupoteza rutuba, vimelea wanaosaidia kuuimarisha huwa katika hatari ya kuangamia.

“Nyungunyungu (earthworm) ni mdudu muhimu sana udongoni. Husaidia katika kusawazisha hewa, na unapozoea kupulizia kemikali dhidi ya wadudu unatishia maisha yake.

“Akikosekana, udongo hautapata hewa na utatuamisha maji shamba liwe chemichemi,” anaonya mtaalamu huyu.

Udongo unaotuamisha maji huwa duni katika shughuli za kilimo, kwani husababisha mimea na mazao kuoza.

Kulingana na David Muriuki, afisa wa kilimo, suala la udongo kuwa duni na kuzidi kiwango cha asidi, pH, huchangiwa pakubwa na matumizi ya mbolea yenye kemikali na dawa.

“Udongo wa aina hiyo huwa na changamoto nyingi, na ndiyo sababu baadhi ya wakulima huwekeza fedha nyingi kisha mapato yanakuwa haba.

“Hili litaangaziwa tukierejelea mfumo asilia, wa kutumia mbolea ya mifugo. Ni muhimu mkulima chipukizi pia apimiwe udongo kabla ya kung’oa nanga shughuli za kulima ili ashauriwe namna ya kuutibu iwapo haujaafikia vigezo vifaavyo,” anaelezea Bw Muriuki.

Kilimohai, mbali na kudumisha rotuba ya udongo na kupata mazao salama, Muriuki anaongeza kusema kuwa ni nafuu kwani hupunguza gharama.

Katika mashamba ya Simon Wagura yaliyoko Ruiru kaunti ya Kiambu na Masinga, Machakos, jumla ya ekari 4.25 (ya kukodi) ameyapamba kwa mboga mbalimbali kama sukumawiki, spinachi, za kienyeji kama mnavu (sucha), mchicha (terere), na sagaa.

Pia, mkulima huyu hukuza pilipili mboga (hoho) na kitunguu kinachotumika kuunda samosa (leek onion).

Anasema kinachofanya mazao kupata soko la haraka ni kwa ajili ya kuzingatia mfumo wa kilimohai.

“Ni vigumu kuafikia asilimia 100, lakini ninajaribu kisiende chini ya asilimia 70,” anasema.

Anaendelea kueleza kwamba hili huanzia katika kitalu, ambapo miche ya mimea anayokuza huipanda kwa mbolea.

Ili kudhibiti usambaaji wa wadudu na magonjwa, huandaa shamba wiki kadhaa kabla ya upanzi.

Bw Wagura anasema hili huwezesha makwekwe na masalia ya mimea iliyokuwa awali kukauka.

“Wadudu wakikosa cha kula hufa na wengine kuondoka. Mimea na makwekwe yanapokauka husaidia kudhibiti usambaaji wa wadudu na magonjwa,” anaeleza Wagura, akiongeza kuwa muda huo pia huwezesha udongo kupumua.

Katika shughuli za upanzi, mkulima anahimizwa kutumia mbolea iliyoiva sawasawa (decomposed manure).

Wakati wa mahojiano, Wagura aliambia Akilimali kuwa kumeibuka na mfumo wa kupanda mbegu moja kwa moja shambani hasa zinazohitaji miche.

“Ili kuepuka kitalu na changamoto zinazogubika miche inapohamishwa, shamba linaandaliwa muundo wa kitanda (beds)-udongo kuinuliwa, mbegu za mimea unayopania kulima zinapandwa moja kwa moja na kutunziwa humo hadi kuvunwa mazao,” akasema.

Kuna fatalaiza ya kisasa inayotumika kunawirisha mazao, na Bw Wagura anasema baadhi ya viwanda vimeibuka na malighafi yasiyo na kemikali.

Pia, ni muhimu kukumbatia matumizi ya boji (mulching), mtaalamu huyu akipendekeza kutumia nyasi zilizokauka kwa kuwa hazina wadudu wala magonjwa. Hatua hii husaidia kuzuia uvukizi wa maji jua linapoangaza miale kali au msimu wa kiangazi.

You can share this post!

Serikali yawatuma Israel wanafunzi 96 kufundishwa ukulima...

Manufaa ya Handisheki: Kisumu kupata miradi ya Sh50 bilioni

adminleo