Makala

AKILIMALI: Kilimomseto cha matunda ni tija kuu kwake

October 3rd, 2019 2 min read

Na PETER CHANGTOEK

SHAMBA lake lina mimea aina ainati.

Lina mimea kama vile mipapai, mipera, mikarakara, mikomamanga (pomegranate), miembe, migomba, michungwa, miparachichi, bitruti (beetroot), ‘pepino melon’, miongoni mwa mimea mingineyo izaayo matunda.

Mbali na ukuzaji wa mimea izaayo matunda, Joseph Ndirangu, pia hukuza mboga mbalimbali za kienyeji. Miongoni mwa mboga ambazo mkulima huyo anakuza ni pamoja na mchicha, mnavu, na kabichi.

Ndirangu, ambaye ni mkazi wa eneo la Soy, Kaunti ya Uasin Gishu, anaendeleza kilimo cha mboga na matunda katika shamba lake ambalo ni ekari mbili, lililoko katika kitongoji kiitwacho Msalaba Yello, umbali wa takriban kilomita 25, kutoka mjini Eldoret, karibu na barabara ya Eldoret-Kitale.

Mkulima huyo, mwenye umri wa miaka 50, pia ni mfugaji wa ng’ombe wa maziwa pamoja na mbuzi wa maziwa. Wanyama hao humfaidi kwa hali na mali; yeye hupata mbolea kutoka kwao na hutumia mbolea hizo kwa ukuzaji wa mimea yake.

Kati ya matunda anayozalisha katika shamba lake, mkulima huyo anasema kuwa ‘pepino melon’ ndiyo humpa faida tele. “Ninauza moja kwa Sh30, halafu kuna miche ya miti hiyo pia. Ninauza kwa Sh100 kila mche,’’ afichua mkulima huyo, ambaye ni baba wa wana watatu wa kike.

Awali, mkulima huyo alikuwa akiikuza mimea ya nyanya, lakini alitamaushwa na maradhi ya mmea huo. Mimea yake ya nyanya ilianza kunyauka na kukauka mmoja baada ya mwingine, na hivyo kumshurutisha kukatiza shughuli ya ukuzaji wayo.

Baadhi ya wateja wake huenda kuzinunua mboga nyumbani kwake japo wakati mwingine yeye huzitembeza akiziuza. Baada ya kuyachuma matunda shambani kwake, Ndirangu huyabeba kwa pikipiki yake ili kuwauzia wateja katika sehemu mbalimbali.

“Nilikuwa nikitumia baiskeli mbeleni, lakini sasa ninatumia pikipiki. Si lazima nipeleke mboga sokoni kwa sababu wateja wanajua nyumbani,’’ asema mkulima huyo.

Endapo hana ndizi za kutosha, mkulima huyo huzinunua kutoka kwa wakulima wengine, na baadaye kuziivisha na hatimaye kuzichukua kuwauzia wateja wake. Pia, yeye huwahamasisha wakulima wengine waipande mimea hiyo ili akosapo, anunue mazao kutoka kwao.

Wakati anapoyachuuza matunda hayo, Ndirangu huwafunza waja kuhusu manufaa ya matunda mbalimbali mathalani ‘pelpino’ na bitiruti (beetroot), kwa mwili wa binadamu. Na kwa kufanya hivyo, humfanya kupata mauzo bora kwa kuwa baadhi yao hushawishika na hatimaye kuyanunua kutoka kwake.

Kuuza

Ndirangu anasema kuwa wakati anapokuwa na matunda kwa wingi, yeye huwauzia wale wanaofanya biashara ya kuuza mboga na matunda.

“Ninatembea nayo kwa pikipiki yangu, yakiwa mengi huwauzia wale ambao wanauza pia,’’ adokeza mkulima huyo.

Anasema kuwa wakati mwingine yeye hununua ndizi kwa wakulima wengine kwa bei ya Sh300 kwa mkungu mmoja, na baada ya kuuza, hupata takribani Sh1,200 kutoka kwa mkungu mmoja wa ndizi. Kwa mujibu wa mkulima huyo, yeye huuza ndizi kreti mbili kwa siku.

Mbali na ukuzaji wa mimea hiyo, mkulima yuyo huyo pia huikuza mihindi, japo kwa ajili ya kutumiwa nyumbani tu.

Isitoshe, yeye hukuza mimea ya alizeti ambayo anasema huitumia kwa ajili ya kuwalisha ng’ombe wake wa maziwa.

Maadamu hakuna jambo lisilokuwa na ndaro, yeye pia ana ndaro ambazo amewahi kuzipitia katika safari yake ya ukuzaji wa mimea na ufugaji wa mifugo. Changamoto kuu katika zaraa hiyo, kwa mujibu wa mkulima huyo, ni magonjwa ya mimea.

Licha ya matatizo hayo yanayomtatiza, anawashauri waja kujitosa katika zaraa, hususan ukuzaji wa mboga na matunda. Anaongeza kuwa ukulima huo ni bora kuliko uzalishaji wa mahindi.