Makala

AKILIMALI: Kina mama walemavu wavumbua mbinu ya kuunda siagi ya njugu

February 21st, 2019 2 min read

Na CHARLES ONGADI

KUVUNJIKA kwa mwiko sio mwisho wa kupika.

Hii ndiyo kauli ya kundi la akina mama wanaoishi na ulemavu la Tunaweza Women With Disability lililopo mtaa wa Ziwa la Ng’ombe, Bombolulu, Mombasa waliovumbua aina ya siagi inayoundwa kwa njugu.

Kundi hili la akina mama 15 waliokuwa wafanyakazi katika kituo cha Bombolulu Cultural Centre, Kisauni, Mombasa waliamua kushikana pamoja na kutafuta mbinu mbadala ya kujipatia mkate wao wa kila siku badala ya kuwa ombaomba baada ya kufutwa kazi.

“Wakati wanachama wetu walipofutwa kazi, hatukuweza kukata tamaa kimaisha kulingana na hali yetu ya ulemavu bali tulitafuta mbinu aula ambayo ingetuwekea chakula mezani,” asema Lucy Chesi ambaye ni mratibu wa mipango katika kundi hili.

Bi Lucy Chesi akiwa na baadhi ya akina mama wanaoishi na ulemavu wakionesha siagi wanayounda kwa kutumia njugu maarufu kama ‘Onja Utamu’ katika duka lao lililoko mtaa wa Ziwa la Ng’ombe, Bombolulu, Mombasa. Picha/Charles Ongadi

Ni aina ya siagi (peanut butter) inayojulikana kama ‘Onja Utamu’ inayotengenezwa kwa ustadi mkubwa kwa njugu na ambayo imeanza kupata umaarufu mkubwa katika maduka mengi mjini Mombasa na Pwani kwa jumla.

Kulingana na Bi Chesi, wameanza kupata wateja kutoka kila pembe ya Pwani kutokana na ubora wa siagi hiyo inayopatikana kwa wingi katika maduka makubwa (Super markets) kama Budget, Jambo, Beach Mat miongoni mwa zingine.

Aidha, kinachofanya aina hii ya siagi kupata wateja kila uchao ni kwamba inadumisha afya njema daima dawamu kutokana na kwamba haitengezwi wala kuongezwa aina yeyote ya kemikali.

“Inaweza kumaliza muda wa mwaka mmoja bila kuharibika na wala hatutumii aina yeyote ya kemikali kuihadhi kwa muda mrefu bali tunatumia mafuta tunayopata kutoka kwa njugu kuihifadhi kwa kipindi kirefu,” asema Bi Chesi.

Kundi hili lililoasisiwa mwaka wa 2000 baada ya baadhi yao kuonyeshwa mlango wa kuondokea na kituo cha Bombolulu Workshop Centre, kilianza kwa biashara ya kuuza nafaka (mchele, mahindi, mawele, maharagwe na pojo) eneo la Bombolulu.

Ushonaji

Ni baada ya biashara yao kuzidi kunoga ndipo waliamua kupiga hatua zaidi kwa kuanzisha biashara ya kushona nguo mwaka wa 2008 ambapo walipata oda kutoka shule nyingi za msingi na upili eneo la Kisauni na Mombasa kwa ujumla.

Hata hivyo, baada ya kufanya kazi kwa muda wa miaka mwili pekee wezi walivamia duka lao na kuiba mashine zao za kushona (cherehani) na kuwaacha bila la kufanya.

Kulingana na Bi Chesi, kampuni ya Safaricom ilijitokeza na kufufua matumaini yao kwa kuwanunulia mashine kadha za kushona.

Mwaka wa 2014 Hazina ya Maendeleo ya eneo ubunge la Kisauni (CDF) iliamua kuwanunulia tarakilishi tano na mashine ya kuchapishia baada ya kusikia masaibu waliokuwa wakiyapitia.

Hata hivyo, baada ya siku tatu pekee baada ya kupewa vifaa hivyo, wezi waliwavamia kwa mara nyingine na kufagilia kila kitu na kuwaacha masikini hohehahe.
Na kwa vile Mungu si Athumani, Wizara ya Kilimo ilijitokeza kuwasaidia kulingana na hali yao ya ulemavu kwa kuwanunulia mashine maalum ya kutengeza siagi na kuwapatia mafunzo ya jinsi ya kutumia na pia kutengeza bidhaa hiyo.

“Wataalam kutika wizara ya kilimo walitupatia mashine inayoweza kuunda kilo mbili ya siagi kwa muda wa robo saa na baada ya kuona faida yake tukajikakamua na kununua yetu iliyo na uwezo wa kuunda kilo 4 kwa robo saa,” asema Bi Tabitha Maundu mmoja wa wanachama wa kundi hili ambaye ana ulemavu wa kuongea (bubu).

Aghalabu kundi hili la Tunaweza Women with Disability hupata malighafi (njugu) kutoka magharibi mwa nchi has eneo la Kakamega na hata Nyanza kusini ambako kilimo cha njugu hufanyika wa wingi.

Siagi hii inapatikana kwa viwango tofauti ambapo kuna kiwango cha gramu 60 inayouzwa kwa Sh70 wakati gramu 100 inaenda kwa Sh100.
Kipimo cha gramu 200 inauzwa Sh180 huku gramu 500 ikienda kwa Sh280 huku kilo 1 ikiuzwa Sh750 katika madukani.