Makala

AKILIMALI: Kinyozi mwanadada ambaye wateja wake wa mwanzo walikuwa mamake na nduguze

March 28th, 2020 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

@maggiemainah

BI Irene Wambui ni kinyozi ambaye ameifanya kazi hii kwa miaka minne.

Kwa kawaida watu wengi wamezoea kinyozi mwanamume lakini Bi Wambui mwenye umri wa miaka 29, amekuwa akiifanya kazi hii kwa ustadi mkuu.

Ingawa ubaguzi upo katika karibu kila sekta, lakini umekuwa ukizidi katika tasnia ya urembo ambapo inakuwa kawaida wanawake kwenda kwa wasusi wanaume lakini ifikapo kwenye kinyozi mwanamke, baadhi ya wanaume wanakuwa hawawaamini na nywele au ndevu zao.

Tunapomtembelea Bi Wambui tunampata anavalia aproni yake uso ukionyesha kujiamini. Anachukua vifaa vyake tayari kwa kazi.

Katika chumba kinachoongozwa na wanaume wanaokata nywele na kunyoa, Wambui, mhitimu wa diploma katika usafiri na utalii kutoka Taasisi ya Amboseli na mtaalam wa mafunzo ya kilimo AMIRAN, anamnyoa mteja wake taratibu tena kwa weledi mkuu.

“Nilizaliwa mjini Eldoret lakini baadaye tulihamia Nyahururu baada ya wazazi wangu kutengana. Nilianza usanii tangu umri mdogo ambapo ningeweza kutengeneza vikuku, pete na mikeka, Baada ya chuo niliona ni bora nitumie talanta yangu ya kisanii kupata pesa kwani kazi za ofisi hazikuwa nzuri kwangu,” anasema Wambui.

Bi Wambui ambaye alikuwa ameshafanya kazi katika kampuni tofauti, alitumia akiba yake ya Sh3,500 kunua mashine yake ya kwanza ya kunyoa mwaka wa 2016.

Kinyozi mwanadada Irene Wambui akiwa kazini. Picha/ Margaret Maina

Mamake na ndugu zake walikuwa wateja wake wa mwanzo.

“Nilianza kunyoa wateja wangu wakiwa nyumbani kwao na pia ofisini huku nikiwatoza ada ya Sh50 kila mmoja lakini nikaongeza hadi Sh500 kila mmoja wateja walipokuwa wengi na nikawa pia nimeboresha huduma,” anasema akiongeza kuwa alijifunza kwenye YouTube huduma ya waxing na ambapo analipisha mteja Sh6,000 mwili mzima.

Baada ya muda aliajiriwa katika Spa jijini Nairobi ambapo alilipwa Sh35,000 kwa mwezi lakini baadaye alikosana na mwajiri kwa sababu ya maswala ya kibinafsi ambayo yalimfanya Bi Wambui kuhamia Nakuru ambapo mama yake anaishi.

Rafiki yake alimsisitizia kwamba anapaswa kukutana na mmojawapo wa vinyozi mashuhuri zaidi mjini Nakuru anayejulikana kama Jimmy Jey.

Mwanzoni alisita akihisi hajafika kiwango cha kufanya kazi na kutosha kufanya kazi na kinyozi mtaalamu.

Kinyozi mwanadada Irene Wambui akiwa kazini. Picha/ Margaret Maina

 

“Nilikutana na Jimmy tuliongea lakini aliahidi kunipigia lakini hakuwahi hadi miezi nane baadaye. Kwa kweli nilidhani hakuamini kazi yangu na ndiyo sababu alichelewa kuwasiliana nami. Hakujua kazi yangu, wala kunijua mimi kibinafsi kwa hivyo alihatarisha biashara yake na akaniajiri,” alisema.

Bi Wambui anasema kuwa mwanzoni kazi yake haikua nzuri sana kwani mwajiri wake ni mtaalam aliye na wateja wengi kwenye kinyozi yake lakini mwajiri wake hakuchoka naye. Alibaki kuwa mshauri wake mkuu na kumuunga mkono.

“Jimmy amenifundisha mengi, angeacha mteja wake na kuniita kando na kunionyesha jinsi ya kushikilia mashine vizuri. Ananikosoa sana na lazima nikubali nimekua na nimepata wateja wengi. Biashara ikiwa nzuri, napata hadi Sh4,000 kwa siku,” anasema.

Mmoja wa wateja wake anakiri kuwa yeye hunyolewa kila mara na Bi Wambui, na anapenda huduma zake.

Changamoto kubwa ambayo amekumbana nayo ni ubaguzi ambapo anasema ni vigumu kuwashawishi baadhi ya wateja kumruhusu kuwanyoa.

Amepambana na ubaguzi wa kijinsia kwa kuwa kinyozi mwanamke anayepata wateja wapya ambao hawana uhakika mwanzoni lakini baadaye hurejea baada ya kuona ubora wa kazi yake.

“Nina bahati kupata motisha kutoka kwa wanaume ninaofanya nao kazi.”