Makala

AKILIMALI: Kiwanda chasifiwa kwa kuboresha maisha vijijini

September 10th, 2020 2 min read

NA FRANCIS MUREITHI

KIWANDA cha maziwa cha Chama cha Ushirika cha Wakulima cha Mumberes, Kaunti ya Baringo, hupokea maelfu ya lita za maziwa kila siku.

Ingawaje barabara inayoelekea kwa kiwanda hiki katika barabara kuu ya Nakuru-Eldoret, inateleza na kujaa maji msimu wa mvua, wafugaji ng’ombe wa maziwa bado hujikaza na kukifikia kwa kuwa wametambua faida yake kwao.

Wafanyakazi hupokea maelfu ya lita za maziwa huku malori yakipiga foleni nje ya lango kuu.

Wafanyakazi ambao huvalia magwanda ya kuhakikisha ubora wa maziwa, huyakagua na kuhakikisha kuwa ni salama kwa matumizi ya binadamu.

Kiwanda hiki huwapa tabasamu washirika wake zaidi ya 3,000 na wauzaji zaidi ya 1,700 wa maziwa kutoka Kaunti ya Baringo na kaunti jirani za Nakuru na Kericho.

Kiwanda kimewafaidi wakulima wengi Kaunti ya Baringo.

Elizabeth Barchok ni mmoja wa wafugaji ng’ombe wa maziwa ambao wanafurahia matunda ya kiwanda hiki. Anasema kuwa hajawahi kujuta uamuzi wake wa kujiunga na kiwanda hicho.

“Faida ninayopata kila mwisho wa mwaka imeniwezesha kununua ng’ombe wengine wawili na hili limesaidia kuongeza kiwango cha maziwa ninayopeleka katika kiwanda hiki kutoka lita 20 had lita 50 kila siku,” anaeleza.

Mama huyu anasema kuwa alikuwa akiishi kwa nyumba iliyoezekwa kwa nyasi lakini sasa amebadilisha na kujenga nyumba nzuri ya mabati kutokana na mapato ya maziwa kwa kiwanda cha Mumberes..

Elizabeth hayuko pekee yake, kwani hata Luka Kigen amejaa tabasamu kwa kuwa kimempa fursa ya kuelimisha wanawe wawili wakifikia vyuo vikuu bila kuchukua mkopo.

“Kutokana na malipo ninayopata kutoka kiwanda cha Mumberes nimeweza kuwasomesha watoto wangu wawili katika chuo kikuu kwani malipo hayacheleweshwi baada ya kupeleka maziwa yangu katika kiwanda hiki,” anaeleza Kigen.

Mwenyekiti wa bodi ya kiwanda hicho cha maziwa, Benjamin Barno, anaeleza kuwa kilianza kubobea baada ya wakazi kutambua kuwa kitawaletea matumaini ya kuwatoa kwa umaskini.

Wafugaji ng’ombe wa maziwa pia walikuwa wakiteseka kwa sababu ya barabara mbovu ambapo maziwa yao yaliishia kuharibika.

“Huku Mumberes wakulima ndio huamua bei ya maziwa bila kushauriana na wenye viwanda na hii imebadilisha sekta hii na kufanya kiwanda hiki kuwa bora katika Kaunti ya Baringo kwa uzalishaji wa maziwa,” anaeleza Barno.

Kiwanda hiki kimeingia katika soko lenye maziwa mengi na tayari kinavutia wafugaji zaidi wa ng’ombe wa maziwa.

“Tunataka wafugaji wetu wa ng’ombe wa maziwa wafurahie jasho lao na kupambana na umaskini uliokithiri kwani kilimo cha viazi na mahindi kimekuwa kikididimia kutokana na bei finyu,” anasema mmoja wa viongozi wa wakulima kutoka eneo hili, David Sawe.

Kiwanda hiki kilizinduliwa na wanachama 72 ambao walichanga Sh20,000 kila mmoja na kufanya uwekezaji wa jumla kuwa zaidi ya Sh25million.

“Kiwanda hiki cha kisasa kina uwezo wa kuboresha lita 16,000 za maziwa kwa siku lakini kutokana na idadi ndogo ya wafugaji ng’ombe wa maziwa katika eneo hili ni lita 11,000 hufikishwa katika kiwanda hiki kila siku,” anasema mmoja wa wakurugenzi wa bodi, Isaac Tubei.

“Katika miezi michache ijayo tuna mipango madhubuti ya kuongeza kampeni yetu ya kuwaandikisha wakulima zaidi ili kuongeza uzalishaji wetu kwani ‘yoghurt’ tunayotengeneza inauzwa kama keki moto na hatuwezi kukidhi mahitaji yanayoongezeka,” anasema Tulbei.

Kiwanda hiki huuza bidhaa zake katika shule na maduka mbali mbali eneo hilo.

Kutokana na harakati zake za kujiimarisha pamoja na kusaidia wakulima na wafugaji waweze kuboresha uzalishaji maziwa, wamepokea misaada na hata fursa ya kupata mikopo.

Wakulima pia wanakisifu kiwanda kwa kuwasaidia kupata mikopo kutoka kwa masharika tofauti.

Hata hivyo, Ili kuongeza mapato yake, kiwanda hicho kimeanzisha upanzi wa miti na huleta faida ya Sh100,000 kila mwaka.Pia kimechimba kisima na huuza lita 3,000 za maji kila siku, na huingiza Sh1milioni kwa mwaka.